Serikali bado inahakiki taarifa, watumishi wa umma watakiwa kuvuta subira
- Imesema kukamilika kwa uhakiki huo wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma kutaiwezesha Serikali kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
- Watumishi waagizwa kuendelea kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Dar es Salaam. Serikali imesema imedhamiria kuboresha maslahi ya watumishi wote wa umma wakiwemo wa kada ya afya kupitia Bodi ya Mishahara na Motisha baada ya kukamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi.
Imesema kukamilika kwa uhakiki huo wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma kutaiwezesha Serikali kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, (Novemba 29, 2018) alipozungumza na watumishi wa kituo cha Afya cha Ushirombo wilayani Bukombe baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa uboreshaji miundombinu wa kituo hicho uliogharimu Sh 500 milioni.
Amesema Serikali inaendelea kushughulikia maslahi ya watumishi na kuwataka waendelee kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
“Tunataka mwananchi akifika kwenye maeneo ya kutolea huduma apokelewe, asikilizwe na ahudumiwe,” amesema Majaliwa
Pia Majaliwa ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kujenga zahanati katika kila kijiji kwa kuwa wilaya hiyo imebakisha vijiji 2 kati ya 52 kumalizia ujenzi huo.
Zinazohusiana: Dk Mpango atoa onyo kali watumishi TRA
Kwa sasa wananchi wa Ushirombo hawana sababu ya kusafiri umbali mrefu hadi Geita mjini au wilayani Kahama kwa ajili ya kufuata huduma za afya kwa kuwa huduma zote zitakuwa zikipatikana kituoni hapo.
Huduma ambazo zitakuwa zikipatikana kwenye Kituo hicho ni pamoja na za mama na mtoto, huduma za upasuaji wa aina zote mdogo na mkubwa, maabara na chumba cha kuhifadhia maiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Dionis Myinga amesema ukarabati wa kituo cha Afya cha Ushirombo ulianza Juni 22, 2018 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Disemba mwaka huu.
Amesema lengo la mradi huo ni kukiwezesha Kituo cha Afya cha Ushirombo kutoa huduma bora za upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito pindi wapatapo matatizo yatokanayo na uzazi ambapo majengo yamekamilika kwa asilimia 99.
“Mradi huu ambao tunaujenga kwa kutumia force account, pamoja na lengo la kutatua matatizo yatokanayo na uzazi kwa akinamama mradi huu utakapokamilika, Kituo cha Afya cha Ushirombo kitaweza kuhudumia watu wapatao 54,271,” amesema Myinga.
Ukarabati wa kituo hicho cha afya unakadiriwa kutumia Sh436.933 milioni hadi utakapokamilika na Sh63.066 milioni zilizosalia kwenye ukarabati huo zitatumika kujenga njia za kuunganisha wodi na kukarabati majengo ya zamani.