Samia ampongeza Mutharika kushinda Urais Malawi, aahidi kuendeleza ushirikiano

September 25, 2025 12:21 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Rais mteule Peter Mutharika kushinda kwa asilimia 57 katika uchaguzi mkuu Malawi.

Arusha. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amempongeza Rais Mteule wa Malawi Arthur Peter Mutharika kwa kuchanguliwa tena kuongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mutharika ambaye pia aliwahi kuongoza nchi hiyo kwa kipindi kimoja kuanzia mwaka 2014 hadi 2020 ameshinda uchaguzi dhidi ya mpinzani wake ambaye ni Rais anayemaliza mida wake Lazarus Chakwera.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi, Mutharika amepata jumla ya kura milioni 3.03 sawa na asilimia 56.8 ya kura zote zilizopigwa. 

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Samia ametoa pongezi hizo zilizoambatana na ahadi ya kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili zenye historia pana.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Profesa Arthur Peter Mutharika, Rais mteule wa Jamhuri ya Malawi, kwa ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa Malawi wa mwaka 2025.

Natarajia kushirikiana kwa pamoja ili kuendeleza zaidi uhusiano wetu wa kihistoria,” amesema Samia kupitia ukurasa wake wa Instagram leo Septemba 25, 2025.

Ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ulianza tangu enzi za kupigania uhuru ambapo kwa sasa unaendelezwa kupitia vyombo vya kikanda kama Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).

Pamoja na mahusiano hayo, nchi hizo pia zinashirikiana katika nyanja nyingine muhimu kama biashara hususani za mipakani zinazohusisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kutoka bandari ya Dar es Salaam jambo linalochangia ukuaji wa ukuaji wa uchumi pande zote mbili.

Sekta za kilimo, nishati na miundombinu ni miongoni ya maeneo mengine ambayo nchi hizo zinashirikiana hatua inayochagiza maendeleo ya pande zote mbili , huku wananchi wake wakibadilishana maarifa, mila na tamaduni katika maeneo ya mpakani.

Hata hivyo, uhusiano kati ya Tanzania na Malawi umekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa, ambao ulitatuliwa kwa amani kupitia mazungumzo ya kidiplomasia.

Aidha, Rais Samia amempongeza Rais wa awamu iliyopita Lazarus Chakwera, na wananchi wa Malawi, kwa kufanya uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW