Safari zote za treni ya TRC kuishia Kamata Dar

August 10, 2018 7:59 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Shughuli zote za TRC kuhamishiwa Kamata.
  • Abiria watalazimika kutumia kituo cha Kamata mpaka ujenzi wa kituo kipya ukamilike.
  • TRC yakusudia kuongeza mabahewa mengine kukidhi mahitaji ya wasafiri.

Dar es Salaam. Shirika la Reli nchini (TRC) linakusudia kuhamisha kituo cha Stesheni Kuu ya reli kilichopo katikati ya jiji na kukipeleka katika eneo la Kamata Kariakoo ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa (Standard Gauge Railway line).

Mabadiliko hayo ya kituo sasa yatafanya abiria wote wa treni za mjini kuanzia wale wa Ubungo, Gongo la Mboto na Pugu kupanda na kushukia eneo hilo la Kamata tofauti na sasa ambapo wanashukia katika kituo hicho cha Stesheni.

Hatua hiyo inayotarajiwa kutekelezwa baada ya mwezi mmoja ujao kuanzia sasa, itawahushu pia abiria wanaotoka katika mikoa ya Tanzania bara ambao nao watalazimika kupanda na kushuka kwenye kituo hicho cha muda ili kumpa nafasi Mkandarasi Yepi Merkez kutoka Uturuki kukamilisha kazi yake kwa wakati. 

Baada ya kukamilisha ujenzi wa reli hiyo katika eneo la stesheni kwa mujibu wa TRC, huduma zote za abiria zitarejea katika Stesheni Kuu ya Posta.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli, Fokasi Sahani amesema uhamisho huo utahusisha pia huduma zote za treni zinazotolewa Stesheni Kuu Posta kupelekwa katika eneo hilo ili  kurahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri na ugavi.

“Watu wote watapandia hapa (Kamata) kwa maana ya huduma zote zitahamia hapa, tutakuwa na treni za kwenda bara hata zile treni zetu za mjini zitakuwa zinaanzia hapa Kamata,” amesema.

Sahani amefafanua mabadiliko hayo hayataathiri ratiba ziilizopo za usafiri wa treni zinazoenda mikoani ambapo zitaendelea kufanya safari zake kama kawaida na kuwataka abiria kuzingatia utaratibu huo mpya ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza. 

“Tutakuwa na treni kwa ajili ya kwenda bara ambazo ziko kama zilivyopangwa Jumanne, Alhamisi na Ijumaa na pia Jumapili, kwahiyo hata zile treni zetu za mjini zitakuwa zinaanzia hapa,” amesema Sahani katika video iliyorushwa mtandaoni leo (Agosti 10, 2018) na chaneli ya Reli Tv. 

Meneja wa Treni za Mjini wa TRC, Mhandisi Ringo Mboma ameleeza kuwa kwa siku moja treni hizo husafirisha abiria zaidi ya 25,000 ambapo ni sawa na abiria 125,000 hadi 130,000 kwa wiki  katikati ya jiji la Dar es Salaam na maeneo ya pembezoni. 

“Kwa mwezi tunasafirisha zaidi ya 600,000. Tunawasafirisha watu wengi sana kuwawaisha makazini kwa hiyo tunachangia kuhakikisha watu wanafanya kazi katika masaa yale yanayohitajika  kufanya kazi,” amesema Mboma.

Anabainisha kuwa TRC inakusudia pia kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuongeza mabehewa mengine ili kukidhi ongezeko la idadi ya watu wanaotumia usafiri huo. 

Ujenzi wa reli ya hiyo ya kisasa yenye urefu wa kilomita 400 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma unaendelea ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali ya Rais John Magufuli kukuza biashara na uchumi kupitia sekta hiyo ya uchukuzi. Sehemu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo hadi Morogoro inatarajiwa kukamilika mwanzoni mwaka 2019. 

Mradi huo wa SGR unaotarajiwa kufika hadi Mwanza siku za usoni utaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na DR Kongo na kuchagiza ukuaji wa biashara baina ya nchi hizo.

Enable Notifications OK No thanks