‘Sadaka Network’ jukwaa la mtandaoni lililopania kurejesha tabasamu usoni mwa Watanzania

August 10, 2019 9:37 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Linatoa fursa kwa watu kusaidiana na kuinuana ili kuondokana na changamoto za maisha.
  • Pesa zinazochangishwa na wadau hutumika kuanzisha miradi ya kijamii.
  • Linatumia lugha ya Kiswahili kuwakutanisha wadau, watu maarufu na vyombo vya habari kutafuta suluhisho kwa watu wenye uhitaji.
  • Ni njia nyingine ambapo teknolojia inatumika katika shughuli za misaada.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa teknolojia inazidi kupenya katika jamii na kuzifikia sekta zote za huduma na bidhaa duniani, ikilinganishwa na hapo awali ambapo ilikuwa inatumika katika masuala ya kitaalamu. 

Lakini sasa teknolojia inatoa fursa kwa watu wa jamii mbalimbali kutumia rasimali zinazowazunguka ikiwemo fedha kusaidiana na kuinuana ili kuondokana na changamoto za maisha na kuhakikisha dunia inakua sehemu nzuri ya kuishi. 

Kwa kutambua hilo, wadau wa maendeleo wamebuni jukwaa la Sadaka Network  linalowezesha watu kukutana pamoja mtandaoni kuelewa na kusaidiana kutatua changamoto zao kwa kuchangishana kiasi kidogo cha pesa. 

Pia linawaleta pamoja wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari, watu maarufu na wabia maendeleo  ili kutengeneza ufahamu na kutoa msaada unaohitajika katika jamii kulingana na mipango ya miradi iliyopo.

Baadhi ya watu maarufu ambao wako katika jukwaa hilo kama mabalozi ni pamoja na mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu, Hasheem Thabeet; Muandaaji wa filamu, Yvonne Cherrie maarufu kama Monalisa; na Mwanaharakati, Doris Mollel.  

“Tunalenga kuwa na jamii endelevu ndani ya Tanzania, ambazo zitaweza kuanzisha, kusimamia na kusaidia miradi ya jamii na kujiendeleza kimaisha kwa uwajibikaji wao wenyewe ili kuwa na mstakabali mzuri wa baadaye,” Mkurugenzi Sadaka Network, Michael Msengi ameiambia www.nukta.co.tz.


Soma zaidi: 


Jukwaa hilo linalenga kuvunja vikwazo vinavyozuia maendeleo ya jamii na kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano mazuri na yenye ufanisi kati ya viongozi, wadau na jamii ili kuzipatia suluhisho changamoto badala ya kuisubiri Serikali iwafanyie kila kitu. 

Kupitia Sadaka Network, ambayo kwa sasa inahusika na miradi ya kuwasaidia watoto, uwezeshaji wanawake kiuchumi na kutafuta vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya baadhi ya magonjwa katika hospitali za Tanzania, wadau huchangishana pesa na kufahamu kwa uwazi zinavyotumika hasa kwa watu waliojiunga na jukwaa hilo. 

Msengi anasema uchangishaji wa pesa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi na taasisi za fedha kutegemeana na mahitaji ya mradi husika ili kuhakikisha uwajibikaji na uwazi unakuwepo wakati wote katika matumizi ya pesa. 

Kwa sasa inatekeleza kampeni ya ‘rudisha tabasamu kwenye nyuso zao’ kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya Society for Plastic Reconstructive Aesthetic Surgery na hospitali ya Aga Khan na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kampeni hii imelenga kurudisha tabasamu kwenye nyuso za wahanga wa ajali na ukatili wa kijinsia ambao umewaachia makovu si tu ya kimwili bali hata kiakili. Fedha zinazochangwa kupitia kampeni zinatumika katika upasuaji wa urekebishaji kwa waathirika hao.

Kwa mujibu wa Msengi, mwaka jana waliwasaidia watoto 46 na mwaka huu wanaendelea kupanua wigo wa kuwafikia watu wengi zaidi kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akiwa na Mkurugenzi wa Sadaka Network, Michael Msengi baada ya kukabidhi vitabu kwa ajili ya wanafunzi wa Wilaya hiyo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za “Kutokomeza Zira Kisarawe” Mei, 2019. Picha|Sadaka Network.

Pia jukwaa hilo hutengeneza maudhui ya kila mradi wanaoutekeleza na kusambazwa kwa vyombo vya habari ili kutoa fursa kwa wadau kufahamu mahitaji na hatua zilizochukuliwa kuleta mabadiliko kwenye jamii. 

Tofauti na majukwaa mengine ya kimataifa, Sadaka Network imejikita katika bara la Afrika pekee huku ikiweka msisitizo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kufanikisha mawasiliano na kuwafikia Watanzania wengi. 

Angella Karashani ambaye anasimimia shughuli za habari katika jukwaa hilo ameiambia www.nukta.co.tz kuwa jukwaa hilo limejitofautisha na mifumo mingine inayotumika kuchangisha pesa kwa ajili ya maendeleo, kutokana na kuwapa wanachama wake nafasi ya kushirikishana uzoefu na mawazo chanya kwa ajili ya kuendeleza jamii inayowazunguka.

Anasema uwazi katika mipango umesaidia jukwaa hilo kupenya katika maeneo mengi wanayofanya kazi. 

Wakati jukwaa hilo likiwaleta pamoja wadau mbalimbali, bado watendaji wake watakua na kibarua kigumu cha kuendelea kubadilisha fikra za Watanzania kupenda kujitoa na kushughulikia changamoto zao kwa kutumia  rasilimali walizonazo. 

Ili kuongeza hamasa, Oktoba mwaka huu wanakusudia kufanya tamasha kubwa la mchezo wa mpira wa kikapu ambapo Thabeet ataungana na mashirika mbalimbali ili kufanikisha upatikanaji wa fedha na kutanua wigo wa jukwaa hilo Tanzania. 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...