Sababu zilizofanya Tanzania iporomoke viwango vya ufanyaji biashara duniani

November 16, 2018 3:45 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeshika nafasi ya 144 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani ikiwa imeshuka nafasi 7 kutoka 137 mwaka 2018.  
  • Tanzania imeangushwa na utendaji usioridhisha wa vipengele vya mchakato wa ufanyaji biashara na nchi jirani, ulindaji wa wawekezaji wadogo, changamoto za ulipaji kodi, usajili wa mali na mchakato wa kufilisi.
  • Yashauriwa kuboresha sera na sheria zinazosimamia sekta ya biashara ili kuongeza wigo wa uwekezaji.

Dar es Salaam. Ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia inaonyesha kuwa Tanzania inazidi kuporomoka katika viwango vya urahisi wa kufanya biashara duniani na kufikia kiwango cha chini kuwahi kuripotiwa ndani miaka mitano.

Ripoti hiyo inayoitwa Urahisi wa kufanya Biashara (Doing Business 2019) imeeleza kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 144 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani ikiwa imeshuka nafasi 7 kutoka 137 mwaka 2018.  Na ndiyo mwaka ambao imefanya vibaya zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Pia katika ripoti iliyotolewa mwaka jana, Tanzania pia ilishuka hadi nafasi ya 137 kutoka 132 iliyorekodiwa katika ripoti ya mwaka 2017. 

Katika ripoti hii mpya iliyotolewa mwishoni mwa Oktoba 2018, Tanzania imepata alama 53.6 ikiwa ni juu kidogo ya wastani wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa alama 51.6. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo alama 100 ni sawa na ‘Frontier score’ inayotambulisha nchi zenye utendaji mzuri zaidi kwenye uchumi hasa urahisi wa  kufanya biashara na sifuri maana yake ni vibaya sana.

Upangaji wa kuupa nafasi uchumi wa nchi katika urahisi wa kuanzisha na kufanya  biashara unapatikana kwa kuangalia umbali wake kufikia ‘Frontier score’ ambapo ni kiwango bora kinachoshikiliwa na nchi zilizoendelea ambazo zina mazingira mazuri ya uwekezaji.

Ili kutimiza malengo ya mradi huo, utafiti huo uliangazia mambo mengine muhimu  ikiwemo  mitaji  ya kuanzisha  biashara,  vibali vya ujenzi, upatikanaji wa umeme, hati ya ardhi na nyumba, mikopo, ulinzi kwa wawekezaji, biashara nje ya mipaka, utekelezaji wa mikataba na ufilisi wa mali. 

Pia ulitumia njia mbalimbali kupata matokeo ikiwemo viashiria vya urahisi wa kuanzisha biashara kama muda, gharama, mtaji na mchakato unaotumika kupata vibali vya biashara.

Kulingana na vigezo hivyo, Tanzania imeangushwa na utendaji usioridhisha wa vipengele vya mchakato wa ufanyaji biashara na nchi jirani, ulindaji wa wawekezaji wadogo, changamoto za ulipaji kodi, usajili wa mali na mchakato wa kufilisi. 

Katika kigezo cha ufanyaji biashara nje ya mipaka, Tanzania imefanya vibaya zaidi kwa kushika nafasi ya 168 duniani ikiwa na alama 20.21 na kufuatiwa na changamoto za ulipaji kodi katika nafasi ya 167. 

Mabadiliko ya sera na sheria katika sekta ya biashara ni muhimu katika kukuza uchumi. Picha | BW Disrupt

Mapendekezo ya ripoti hiyo kwa Tanzania ni kuboresha mfumo wa upatikanaji wa hati za ardhi na majengo ya kufanyia biashara ili kuvutia wawekezaji wengi kwa muda mfupi  na kurekebisha mifumo ya kodi na kuongeza wigo wa biashara na nchi jirani. 


 Zinazohusina: Kiswahili ndiyo mpango mzima kusaka wateja Tanzania: Ripoti


Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa Tanzania imeanza kuchukua hatua muhimu kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ikiwemo kuanzisha mfumo wa kijiditali (online platform) kwa ajili ya usajili wa biashara na kampuni unaoratibiwa na Wakala wa Usajili Kampuni (BRELA).

“Tanzania imeanza kurahisisha mchakato wa kuanzisha biashara kwa kuzindua usajili wa kampuni mtandaoni,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Mfumo huo utasaidia katika kupunguza muda na gharama za usajili wa kampuni zenye malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji, jambo linaloweza kuisadia Tanzania kupanda katika viwango vya ufanyaji biashara duniani siku zijazo. 

Kupitia makubaliano ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika biashara, Tanzania imeimarisha mfumo wa kodi na forodha kwa shughuli zote za manunuzi ya bidhaa na huduma maeneo ya mpakani yanayounganisha hasa nchi za Rwanda, Uganda na Kenya.

Pamoja na yote hayo bado ina kazi kubwa ya kurekebisha mfumo wa sera na sheria zinazoongoza sekta ya biashara ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji na kuongeza idadi ya wawekezaji nchini.

Hali ilivyo Afrika

Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Tanzania haijafanya vizuri sana ikiwa nyuma ya Burundi ambayo iko nafasi ya 168 ulimwenguni huku ikipitwa kwa mbali na Rwanda iliyoshika nafasi ya 29. 

Jirani na mshindani mkubwa wa Tanzania,  Kenya inashika nafasi 61 baada ya kufanya mageuzi makubwa kwa mujibu wa ripoti hiyo katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara huku Uganda ikikamata nafasi ya 127.

Mgeni mpya wa jumuiya hiyo Sudan Kusini yupo kwenye kundi la nchi 10 za mwisho zilizofanya vibaya ikiungana na nchi kama Somalia, Eritrea, Venuzuela, Yemen, Libya, Congo DRC na Afrika ya Kati ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na migogoro ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. 

Katika ngazi ya bara la Afrika, Tanzania imezipita nchi za Ethiopia, Angola na Nigeria ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi. Ripoti hiyo inazitaja kutokuwa na mifumo ya uwazi ya usajili na utoaji wa leseni za biashara jambo linalozuia uwajibikaji wa watendaji waliopewa dhamana ya kutoa huduma hizo kwa jamii.

Pamoja na yote hayo, nchi za Afrika zimeanza kuchukua hatua muhimu za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara tangu mwaka 2012 jambo linaloliweka bara hilo katika nafasi ya kuvutia wawekezaji wengi kutoka nchi za Asia kuingia katika maeneo mbalimbali ili kuendeleza rasilimali ambazo hazijatumika kikamilifu.  

“Mwaka huu, Ufanyaji biashara umerekodi mabadiliko 107 katika nchi 40 za Kusini mwa Jangwa la Sahara na sekta binafsi imeanza kuona matokeo ya maboresho hayo. Wastani wa muda na gharama za kusajili kampuni umepungua kutoka siku 59 mwaka 2006 hadi siku 23,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Enable Notifications OK No thanks