Sababu za umeme kukatika mara kwa mara
- Umeme hukatwa kama kuna matengenezo yanafanyika.
- Shughuli za kibinadamu na mazingira huchangia.
- Umeme ukikatika katika eneo lako toa taarifa ufumbuzi ufanyike.
Dar es Salaam. “Huoooo” ni kati ya sauti ambazo ni maarufu miongoni mwa Watanzania. Ni sauti za kuashiria kuwa umeme uliokuwa umekatwa, umerudi.
Kwa wengi, kukatika kwa umeme kunaathiri shughuli zao hasa zinazotegemea nishati hiyo. Biashara kama saluni, majokofu ya kugandishia barafu, utotoreshaji wa mayai ya kuku na matumizi ya kompyuta ni kati ya shughuli zinazokwama kwa umeme kukatika.
Kukatika kwa umeme hutokea kwa sababu mbalimbali ikiwemo matengenezo yanayofanywa katika gridi ya Taifa ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) au uharibifu katika msongo wa usambaji umeme.
Tanesco imesema pale kunapokuwa na matengenezo, huwa wanatoa taarifa kwa wananchi. Picha| Mwananchi Mzalendo.
Ni sababu gani zingine zinazosababisha umeme kukatika?
Matengenezo
Kwa muda ambao Tanesco wanahitaji kufanya matengenezo ya mitambo au miundombinu ya umeme, nishati hiyo hukatwa kwa muda mfupi ili kukamilisha zoezi hilo.
Matengenezo hayo yanapofanyika taarifa hutolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Meneja Uhusiano Tanesco Kanda ya Mashariki, Johary Kachwamba amesema leo Septemba 21, 2021 wakati akifanya mahojiano na kituo cha redio cha Clouds.
“Mfumo wetu wa kusafirisha umeme, tunatumia mfumo mmoja lakini sasa hivi kwenye uwekezaji, kuna mfumo ambao unajengwa tunasema “ring circuit” au umeme wa mzunguko ambao hata kama kutakuwa na athari sehemu fulani, inaweza kutoka laini ambayo ina tatizo…” amesema Kachwamba.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mfumo huo upo kwenye utekelezaji ambao unaendelea.
Shughuli za kibinadamu
Kwa kuwa miundombinu ya Tanesco ipo katika mazingira ya binadamu, shughuli za watu pia huweza kuathiri miundombinu hiyo na kusababisha umeme kukatika hata kama Tanesco haikupanga.
Kachwamba amesema, matukio yasiyotarajiwa kama ajari za barabarani ambapo mtu anaweza kugonga nguzo ya umeme na hivyo kusababisha hitilafu kwenye usafirishaji wa umeme, ni kati ya sababu ya umeme kukatika mara kwa mara.
“Wakati mwingine unakuta eneo labda ni gari imegonga nguzo na inaathiri eneo fulani kwa maana hiyo, hapo umeme ukikatika, lazima kwasababu mtu ana mahitaji, atawasilisha malalmiko yake,” ameeleza Kachwamba.
Ajali za barabarani ni sehemu ya sababu za umeme kukatika mara kwa mara. Picha| kamanda wa matukio.
Hitilafu za mazingira
Wakati mwingine, umeme unakatika kutokana na hirafu za kimazingira ambazo hazizuiliki ikiwemo miti kudondokea nyaya.
Mhandisi wa Tanesco Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Fred Tweve amesema asilimia 80 ya umeme kukatika wilayani humo inachochewa na hirafu za kimazingira, kuu ikiwa ni matawi ya miti ya mnazi au miti ya mikorosho kudondokea kwenye nyaya na kusababisha umeme kukatika.
“Yaani tawi tu likigusa nyaya lazima umeme ukatike. Tukitaka kukata miti, wananchi hufukuza wakandarasi na mapanga,” amesema Tweve kwenye kongamano la wadau wa nishati wilayani humo lililofanyika wiki iliyopita.
Siyo kwamba umeme hautoshi, upo wa kutosha
Kukatika kwa umeme hakuhusiani na uwezo wa Tanesco kuzalisha umeme nchini kwani wataalamu wa nishati kutoka shirika hilo wameweka wazi kuwa Tanesco inazalisha hadi ziada ya mahitaji ya Tanzania.
Meneja Mwandamizi Tanesco kanda ya Mashariki, Mhandisi Hassan Said amesema “uwezo wa kuzalisha kwa Tanesco nchi nzima ni Megawati 1,574 kwenye gridi ya Taifa.”
Mtaalamu huyo amesema mahitaji ya juu kabisa kwa Tanzania ni Megawati 1,200 ambapo kuna zaidi ya Megawati 300 inayobaki kama ziada.
Mtaalam huyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwa uongozi wa Tanesco mara umeme unapokuwa umekatika katika eneo lao ili kupatiwa ufumbuzi kuliko kutoa lawama bila kujali ni sababu ipi imesababisha umeme kukatika.
Latest