LHRC: Kukosekana kwa umeme kunakwamisha upatikanaji wa haki

February 20, 2024 4:41 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Haki hizo ni pamoja na haki ya kuishi, kufanya kazi na kupata ujira.
  • LHRC yaitaka Serikali kubuni vyanzo vya uzalishaji umeme visivyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) kimeitaka Serikali kuandaa mikakati madhubuti itakayoleta suluhu ya kudumu ya tatizo la umeme nchini kwa kuwa jambo hilo linakwamisha upatikanaji wa baadhi ya haki za wananchi.

Kwa mujibu wa LHRC kumekuwepo na tatizo la kukatika kwa umeme bila taarifa kamili nchini tangu mwaka 2022, licha ya mabadiliko kadhaa ya viongozi wa Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amebainisha kuwa tatizo la kukatika kwa umeme linaathiri haki mbalimbali za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ikiwemo ibara ya 22 na 23 inayobainisha haki ya kufanya kazi na kujipatia ujira, ibara ya 14 haki ya uhai kwa kupata afya bora, na ibara ya 18 haki ya kupokea na kutoa taarifa.

“Kuendelea kwa tatizo la mgao wa umeme kwa kujirudia rudia kumesababisha usumbufu mkubwa sana kwa wananchi, hususan katika shughuli za kila siku za maisha kama vile uzalishaji, biashara, huduma za afya na elimu.

“Mbali na changamoto zote hizi wanazopitia Watanzania hakuna mtu aliyewajibika kwa ukosefu wa umeme. Wakati Serikali ilishatoa ahadi ya kuhakikisha umeme unapatika Machi 2024,” amesema Henga katika taarifa yake kwa wanahabari aliyotolewa jijini Dar es Salaam leo Februari 19, 2024.

Henga amesema ukosefu wa umeme unasababisha ongezeko la gharama za maisha kwa kuwa vyanzo mbadala vya nishati hiyo kama jenereta au umemejua  hupatikana kwa gharama kubwa na huhitaji fedha zaidi kwa ajili ya kuendesha mitambo yake.  

“Hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama za maisha na kupungua kwa ufanisi wa kiuchumi kwa wananchi,” amesisitiza  Henga.

Jinsi ya kupata umeme wa uhakika

Wakati wanachi wakiendelea kuugulia maumivu ya mgao wa umeme ambapo awali ulitangazwa kukoma Machi 2024, na baadae Spika wa Bunge Tulia Ackson kuongeza muda hadi Juni 2024, LHRC wametoa mapendekezo yatakayoisaidia Serikali kushughulikia tatizo la kukatika kwa umeme.

LHRC wamesema Tanesco inapaswa kupanga ratiba ya matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme kwa kuzingatia sayansi ya mabadiliko ya tabianchi.

Tanesco wameshauriwa kutoa taarifa zisizokuwa na mkanganyiko kwa umma ambapo awali ukame ulitajwa kama sababu ya kutokuwepo na umeme wa uhakika ingawa changamoto imeendelea kuwepo hata baada ya mvua nyingi kunyesha hususan katika maeneo yenye mabwawa ya kusalisha maji.

Itakumbukwa  Novemba 23, 2022, Tanesco ilitoa taarifa kwa umma juu ya hali ya upungufu wa umeme na mpango wa kukabiliana nao, ambapo shirika hilo lilibainisha kupitia kipindi kigumu cha upungufu wa umeme kwa sababu ya ukame na matengenezo ya mitambo.

Sambamba na hilo Serikali imetakiwa kuongeza uwekezaji katika vyanzo vya uzalishaji wa nishati ya umeme isiyoathirika kirahisi na mabadiliko ya hali ya hewa ili kuwa na umeme misimu yote ya mwaka.

“Pendekezo hili linalenga kuongeza upatikanaji endelevu wa nishati ya umeme kwa kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi huathiri kwa kiasi kikubwa upungufu wa uzalishaji wa umeme,” amesema Henga.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW