Sababu za chui kuwa mwindaji mashuhuri

August 3, 2021 1:13 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Chui ana uwezo wa kuona gizani mara saba zaidi ya binadamu. Wanyama kama swala, pundamilia na nyumbu hupoteza uwezo wa kuona pale giza linapoingia hivyo kumrahisishia chui zoezi la uwindaji. PIcha| KonnectHQ.


  • Anatumia mazingira yake vizuri ikiwemo kuwinda peke yake.
  • Hutumia muda wake wa mchana kupumzika na usiku kuwinda.
  • Hupenda kuacha haja ndogo ili kuweka alama ya himaya yake.

Huenda umekuwa ukisimuliwa au kuangalia makala za wanyama hasa chui na umashuhuri wake wa kuwinda ili kujipatia chakula.

Wengine wamefika hadi mbugani na kumuona mnyama huyo jamii ya paka lakini wanawaweza kuwa hawamfahamu kwa undani mnyama huyo. 

Chui ni mwindaji mzuri kuliko wanyama wengine kama simba, fisi na mbwa mwitu na sifa hiyo anaipata kutokana na muonekano wake, tabia zake na mazingira anayoishi. 

Twende pamoja kuangazi kwa undani kuhusu chui ili tuweze kujifunza kwa undani kuhusu maisha yake hasa ya uwindaji:

Muonekano wa kuvutia

Chui ni mnyama mkubwa, jamii ya paka mwenye ngozi yenye mvuto kuliko wanyama wote kwenye kundi hilo. Ngozi yake ina rangi ya njano mpauko yenye madoa meusi, ingawa chui wengine wana rangi ya dhahabu na madoa meusi.

Kipindi cha kiangazi mbugani, nyasi hukauka na kupoteza rangi yake ya kijani na kuwa ya njano na ni kwenye nyasi ndefu ndipo chui hupenda kulinyatia windo lake.

Hiyo ni kwa sababu ngozi yake hufanana sana na mazingira hayo, hivyo wanyama kama swala hushindwa kumuona mapema na pindi pale wanapomuona wanakuwa wamechelewa sana.

Chui hutofautiana uzito baina ya majike na madume, majike huwa na uzito wa wastani wa kilo 60 huku madume wakiwa na kilo 70. Chui ana urefu wa mita mbili toka kichwani hadi mkiani na mkia wake pekee unaweza kuwa na urefu wa mita moja.

Uzito wa chui ni zaidi kidogo ya ule wa fisi na mbwa mwitu ambao humpa uwezo wa kuwinda wanyama wenye miili mikubwa kama pundamilia na twiga akiwa peke yake.

Tabia zinazomtofautisha na wanyama wengine

Chui ana uwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilomita 58 kwa saa na hii inamaanisha kwamba akiamua kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro anaweza kuchukua takriban saa tatu na nusu.

Chui ni moja kati ya wanyama wasiri na wapweke zaidi duniani. Tofauti ilivyo kwa simba, mbwa mwitu na fisi, chui hupendelea kuishi peke yake na hufanya tendo la kujaamiana mwaka mzima ingawa kipindi cha mvua shughuli hiyo huongezeka zaidi.

Hubeba uja uzito kwa miezi mitatu na huzaa hadi watoto wanne ambao huwaficha chini ya miamba, vichuguu au kwenye vichaka ili kuwaepusha na wawindaji wa kukufuru kama fisi.

Chui ni hodari wa kukaa juu ya miti, sifa ambayo ni tofauti na wanyama wengine jamii ya paka akiwemo simba na mbwa mwitu. Picha| Wild Planet Magazine.

Kwa kuwa chui siyo mnyama mwenye kasi kuliko vitoweo vyake lakini mbinu yake kubwa ni kunyata na kumkamata mnyama pale ambapo hategemei. Tabia yake ya kuwinda peke yake humsaidia kwa sababu hakuna siri ya wengi.

Anapowinda peke yake hupunguza kokoro kokoro kelele na inakua rahisi kuwadaka wanyama kama swala ambao wana hisia kali hasa  wakiona tu majani yanacheza basi wanajua pale kuna mnyama mkali na kuanza kukimbia.

Mnyama huyu mwenye kuishi miaka isiyozidi 23, hutumia muda wake wa mchana kupumzika huku kazi yake ya uwindaji ikianzia muda ambao jua linapoanza kuzama mpaka jua linapochomoza.

Chui ana uwezo wa kuona gizani mara saba zaidi ya binadamu. Wanyama kama swala, pundamilia na nyumbu hupoteza uwezo wa kuona pale giza linapoingia hivyo kumrahisishia chui zoezi la uwindaji.

Chui huonekana sana akiwa mtini kuliko ardhini kwa kuwa hupanda mtini kuangalia fursa za uwindaji, kuhifadhi windo lake na pia kupumzika baada ya kuwinda.

Tabia hiyo ya kukaa kwenye miti humpa fursa ya kuwakamata kwa urahisi tumbili na nyani wakiwa wamelala mtini.

Ana uwezo wa kulipandisha windo lake mtini ili kulificha toka kwa wanyama wengine wasiyoweza kukwea miti kama fisi, mbwa mwitu na baadhi ya simba. 

Lakini simba wa Ziwa Manyara hapa Tanzania ni mashuhuri wa kupanda miti pia na ndiyo moja ya sababu kubwa chui ni adimu kwenye hifadhi hiyo.

Wanyama wengi wawindaji wanapata changamoto ya kupokonywa mawindo na wanyama wengine au kushindwa kumaliza kula lakini chui anachoweza kuwaachia wanyama wengine ni harufu tu.

Sifa nyingine ni kuunguruma, kukohoa, kupiga chafya na hupenda kuacha haja ndogo ili kuweka alama ya himaya yake.

Ni mnyama asiyeonekana kirahisi na ukitaka kumuona basi itabidi ufunge safari kwenye hifadhi za Taifa ikiwemo Serengeti ili ujionee chui kwa macho yako.

Ndugu wa karibu wa chui ni mnyama duma. Kwa taswira ya nje ya mbuga, duma anaonekana kuwa mwindaji bora zaidi kutokana na kwamba ndiye mnyama mwenye kasi zaidi ardhini lakini ukweli ni kwamba duma hutegemea kukimbiza mpaka apate lakini chui ana mbinu mbadala za kupata chakula chake.

Mwandishi wa makala haya ni Nasibu Mahinya, Afisa Mahusiano wa jukwaa la masuala ya utalii la Tenten Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika katika hifadhi za Taifa.

Enable Notifications OK No thanks