Sababu kuu za kuhifadhi rasimali misitu, nyuki

May 17, 2020 11:21 am · Dk Felician
Share
Tweet
Copy Link
  • Ina mchango mkubwa kwa usalama wa chakula na kuongeza uzalishaji wa mazao.
  • Ni chanzo cha mapato kwa Watanzania. 
  • Udhibiti wa shughuli za kibinadamu utasaidia uhifadhi wa misitu.

Tanzania imebahatika kuwa na eneo lenye misitu takribani hekta milioni 48 ambalo ni rasimali muhimu kwa matumizi mbalimbali ya maendeleo.  

Suala la ikolojia na umuhimu wake kwa maisha ya kila siku bado halieleweki vizuri. Mathalani, misitu inachangia sana kwa usalama wa chakula hususani kuboresha udongo na kuzuia mmomonyoko kwa kuongeza mbolea kupitia majani na mizizi.

Wakati huo huo, nyuki huongeza uzalishaji wa mazao (mavuno kuwa mengi) kupitia huduma ya kurutubisha maua (pollination) kwa kutembelea maua mbalimbali wakati wakitengeneza asali ambayo pia hutumiwa na binadamu kwa chakula na mengineyo.

Misitu na nyuki ni rasilimali muhimu kwa sababu tunapata manufaa ya mbao, nguzo, kuni, mkaa na chakula (matunda, mboga asilia, mafuta), wadudu waliwao na asali.

Pia hutupatia uyoga mizizi (kwa chakula na dawa), nyama ya porini (wanyama na ndege) na vingine vingi. Vilevile, rasilimali misitu na nyuki ni chanzo cha kipato kwa Watanzania wengi. 

Mnyororo mzima wa mazao  ya misitu unahusisha wafanyabiashara wakubwa, kati na wadogo. Walio wengi mijini na vijijini wanajihusisha na usambazaji/uuzaji wa mazao ya misitu. 

Upatikanaji wa mkaa, kuni, nguzo, mbao, fito, asali kirahisi katika mitaa na sehemu tunazoishi ni matokeo ya wasambazi wa chini kabisa. 

Kutokana na rasilimali misitu kuwa chanzo muhimu cha bidhaa na hatimaye kutupatia kipato ndiyo maana misitu  hujulikana kama “Misitu ni Mali”.

Misitu imegawanyika sehemu kuu mbili: Uhifadhi na Uzalishaji mali kwa maana kwamba kupitia misitu-hifadhi tunapata huduma za kiikolojia na misitu-uzalishaji tunapata bidhaa kwa matumizi mbalimbali. 

Misitu ni mali. Ni lazima tuiitunze ili itunufaishe katika shughuli za maendeleo. Picha|Mtandao.

Upatikanaji wa huduma za kiikolojia kwa njia endelevu ni jambo la msingi kwa maendeleo yetu na Taifa zima. Mathalan, misitu na uoto wa asili kwa ujumla, husaidia kuhifadhi udongo ambao ni muhimu kwa uzalishaji wa chakula. 

Vilevile, misitu/uoto asilia husaidia maji ya mvua kupenya ardhini kirahisi hivyo kuhifadhi maji ambayo hupatikana mwaka mzima kupitia chemichemi na mito. Kadhalika hurutubisha udongo kutokana na majani, matawi na baadhi ya miti kuanguka na kuoza hatimaye kuchanganyikana na udongo na kuwa mbolea. 

Isitoshe kupitia baadhi ya miti yenye mizizi inayofyonza gesi-naitrojeni na kuiingiza ardhini (nitrogen fixation) na kuimarisha ukuaji wa mazao na mimea. 

Kimsingi misitu huweka mazingira mazuri kwa bioanuai (biodiversity) mbalimbali kuweza kuishi kwa mfano, wanyamapori, nyuki na baadhi ya mimea na wanyama wasiopatikana sehemu nyingine duniani isipokuwa Tanzania tu.


Soma zaidi: 


Kupitia mfumo huo tunanufaika kwa utalii pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha, kupata asali na nta kupitia huduma ya nyuki. Kadhalika,  mito yenye maji ya kutosha tunapata chakula zaidi kupitia umwagiliaji na kuzalisha umeme utokanao na nguvu ya maji (hydropower) ambao ni muhimu kwa shughuli za viwanda, usafirishaji, biashara na uchumi kwa ujumla. 

Maji pia ni nyenzo muhimu kwa maisha ya wanyama kama viboko na mamba pamoja viumbe wengine kama samaki, vyura na wengineo waishio majini. 

Rasilimali zote hizo ni muhimu kwa manufaa yetu na maendeleo ya Taifa letu. Kadhalika misitu na mimea husaidia kuboresha tabianchi (climate change) kupitia uwezo wake wa kufyonza gesi ukaa (carbon dioxide-CO2) kuitoa kwenye mfumo wa hewa na kuitumia kutengeza chakula kinachowezesha ukuaji wake na wakati huo kuingiza oksijeni (O2) hewani kwa matumizi ya binadamu na viumbe hai wengine.  

Pamoja na huduma zote hizo muhimu, binadamu tumekuwa mwiba kwa misitu kutokana na shughuli mbalimbali tunazozifanya bila kuzingatia matumizi endelevu kwa rasilimali misitu.

Takwimu za 2015 zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii zilionyesha kuwa tunapoteza misitu ya asili kwa kasi ya hekta 372,000 kwa mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu zisizozingatia uhifadhi na kilimo kijani. 

Vilevile, mwaka 2017 Kituo cha Taifa cha Kufuatilia mwenendo wa gesi kaboni (carbon) na madhara ya tabianchi (National Carbon Moniting Centre-NCMC) kilichopo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilibaini kuwa kasi ya kutoweka misitu ilifikia hekta zaidi ya 469,000 kwa mwaka. 

Misitu ni kivutio cha nyuki ambao wanaweza kutupatia asali inayotumika katika shughuli mbalimbali. Picha|Mtandao.

Hali hii inatokana na usimamizi usioridhisha kwa misitu ya asili hasa kwenye maeneo ya vijiji; hivyo kutokana na kilimo cha kuhama hama, kuvuna miti kiholela, kuchoma moto mapori, ufugaji usiozingatia wingi na uwezo wa eneo la malisho na kutokuwepo matumizi bora ya ardhi vijijini ni visababishi vya misitu kuharibika haraka. 

Kutokana na ripoti tajwa hapo juu inaaminika kuwa misitu ya Tanzania inaweza kutupatia meta za ujazo milioni 42.5 bila kuathiri ukuaji na kuendelea kutoa huduma za kiikolojia ipasavyo.

Lakini kiasi kinachovunwa kila mwaka ni takribani meta za ujazo 62 milioni kuashiria kuwa tunakata miti zaidi kwa meta za ujazo 19.5 milioni kuliko kiwango kinachotakiwa kuvunwa bila kuathiri misitu.Sasa inabidi tujizatiti tuweze kuisimamia misitu kwa nia ya kuhakikisha tunavuna kiwango kinachotakiwa kuvunwa na siyo kinyume chake.

Kinachotakiwa ni kuhakikisha huduma za kiikolojia zinadumishwa kwa faida ya wote. Mkazo uwe kwa upatikanaji, utumiaji sahihi na uendelezaji wa huduma husika kila mahali.

Kilimo kiwe kijani na endelevu. Ufugaji uzingatie uwezo wa malisho na panapowezekana wafugaji wamilikishwe maeneo ya kuchungia na wayaendeleze kwa kufuata ushauri wa wataalamu. 

Ili kufanikisha yote ni vizuri kukawepo ushirikiano wa karibu kwa sekta na taasisi husika kuanzia Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) hadi utawala wa vijijini bila kusahau wadau wengine muhimu na jamii.

Kiuhalisia misitu ni kiwanda cha dawa tuitunze na iweze pia kututunza. Wiki ijayo tutaangazia umuhimu wa rasilimali ya misitu kwa maendeleo ya viwanda vya kutengeneza dawa.

DkFelician Kilahama ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki mstaafu Tanzania.

Enable Notifications OK No thanks