Ripoti:Tanzania yapiga hatua kuendeleza ujasiriamali wa kidijitali Afrika
- Iko miongoni mwa nchi sita za Afrika zinazomiliki asilimia 20 ya shughuli za ujasiriamali wa kidijitali.
- Shughuli hizo ni pamoja na vituo vya ubunifu na teknolojia ambapo Tanzania viko zaidi ya 40.
- Kodi, ukosefu wa mitaji, rasilimali na usawa vinakwamisha Afrika kufaidika na uchumi.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNCTAD) imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zilizo mstari wa mbele katika kuchagiza ukuaji wa ujasiriamali wa kidijitali, lakini kodi, ukosefu wa mitaji na usawa vinakwamisha kufaidika na uchumi huo.
Ripoti hiyo iliyopewa jina la Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy Report 2019) iliyozinduliwa jana (Septemba 4, 2019) inaeleza kuwa Tanzania iko katika kundi la pili lenye nchi sita (Ghana, Morocco, Senegal, Tunisia, Uganda) ambazo zimepiga hatua kubwa katika kuhimiza shughuli za ujasiriamali wa kidijitali ambao unabebwa zaidi na maendeleo ya teknolojia na matumizi ya intaneti.
Nchi hizo sita zinashikilia asilimia 20 ya shughuli zote za ujasiriamali wa kidijitali katika bara la Afrika au sawa na kusema kwa kila shughuli 10 za ujasirimali huo mbili zinafanyika katika mataifa hayo.
Shughuli za ujasiriamali wa kidijitali hujumuisha vituo atamizi na ubunifu (Innovation hubs) vinavyendeleza mawazo yenye mlengo wa teknolojia ili kutatua changamoto za jamii kwa kutoa huduma na bidhaa zinazorahisisha maisha.
Asilimia 60 nyingine inashikiliwa na nchi nne tu za Kenya, Misri, Afrika Kusini na Nigeria ambao zinatajwa kama nchi za mwanzo kabisa barani Afrika kupokea na kuendeleza kwa kasi ujasiriamali wa kidijitali.
Na asilimia 20 iliyobaki imegawanywa katika nchi 44 ambazo bado zinajikongoja katika matumizi ya teknolojia.
Zinazohusiana:
- Mgawanyiko usio sawa vituo vya ubunifu unavyoathiri ukuaji wa teknolojia Tanzania.
- Apps za elimu zinazoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
- Wiki Ya Ubunifu inavyoangaziwa kuleta mabadiliko Tanzania
Ripoti nyingine ya utafiti wa mtawanyiko wa vituo vya ubunifu Tanzania (A mapping of Tanzanian hubs and innovation spaces) iliyotolewa Novemba 2018 na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) inaeleza kuwa Tanzania ina vituo vya ubunifu 43 ambapo hutofautiana kutokana na utendaji wake, makundi yanayokusudiwa, huduma zinazotolewa na mfumo wa kibiashara.
Vituo hivyo 39 vinapatikana Tanzania Bara katika mikoa tisa tu huku vinne vilivyosalia vikiwa visiwani Zanzibar. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa kuna mikoa 19 kati ya 26 ya Tanzania Bara haina vituo hivyo.

Tanzania inafaidika na ujasiriamali wa kimtandao?
Licha ya Afrika kuelezwa kuwa ni eneo muhimu ambalo linaibukia kwa ujasiriamali wa kidijitali bado kasi yake hairidhishi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji na rasilimali nyingine za ujasiriamali ukilinganishwa na mabara mengine.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa uwepo wa kodi kubwa katika taasisi za teknolojia na huduma za kidijitali ikiwemo matumzi ya intaneti na miamala ya pesa kwa njia ya simu hasa katika nchi za Tanzania, Zambia, Uganda, Kenya na Zambia bado ni changamoto kubwa.
“Wakati aina hii ya kodi inayopendelewa zaidi na Serikali, inaweza kuwa yenye tija lakini itasababisha kupungua kwa shughuli za kiuchumi kwa kupunguza idadi ya watumiaji wanaofanya kazi kwenye mtandao,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Sababu nyingine inayokwamisha Afrika isifaidike na uchumi wa kidijitali ukosefu wa usawa duniani ambao ukiendelea utaongeza pengo kati ya nchi zilizo mbele kimtandao na zile zisizo na mtandao.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyochambua ripoti hiyo, inazitaja Marekani na China kuwa ndiyo zinanufaika zaidi na uchumi wa kidijitali, ambapo mataifa hayo mawili yanagawana asilimia 75 ya faida zote zinazohusiana na teknolojia za miamala bila kuhitaji huduma za kibenki.
Pia zinanufaika kwa asilimia 50 ya mapato ya biashara ya intaneti na zaidi ya asilimia 75 ya soko la kuweka takwimu kwenye mitandao.
Wadau wakishikamana na kuongeza vituo vya ubunifu ili kuwapatia nafasi na fursa wabunifu kuendeleza kazi inaweza kusaidia kupunguza la kidijitali Tanzania. Piacha|Mtandao.
Ripoti hiyo inasema kuwa kwa maeneo mengine, hususan Afrika na nchi za Amerika ya Kusini, bado zinajikongoja na iwapo mwelekeo huu utaendelea, utazidi kusababisha zaidi ukosefu wa usawa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye dibaji ya ripoti hiyo.
“Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa pengo la kidijitali katika dunia ambayo nusu ya dunia ina mkwamo kwenye mtandao wa intaneti au haina kabisa mtandao huo. Ujumuishi ni muhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali ambao unanufaisha kila mtu,” Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwenye dibaji ya ripoti hiyo.
Mdau wa teknolojia, Mohamed Shellimoh ambaye amekuwa akisimamia vituo vua ubunifu amesema ili kupunguza pengo la kidijitali kuna kila sababu ni kutoa fursa kwa vijana wenye mawazo ya kibunifu hasa kuwapatia eneo (space) ambalo wataeleza kazi zao zilete matokeo kwenye jamii.
Shellimoh amebainisha kuwa ushirikiano wa wadau katika kuzisaidia kampuni changa (startup) kusimama kimtaji na kupata masoko ya uhakika wa huduma na bidhaa wanazotoa inaweza kusaidia kukuza uchumi wa kidijitali kwa nchi kama Tanzania.
Latest