Ripoti Maalum: Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu
- Wataalamu wanaeleza kuwa wengi huwa wamelegea na hugeuka rangi.
- Ulaji wa samaki waliovuliwa kwa mabomu husababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani.
- Serikali imesema inaendelea na operesheni ya kuwakamata wanaohusika huku uvuvi haramu ukipungua kwa asilimia 85.
Dar es Salaam. Licha ya kufanya biashara ya samaki jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka nane sasa, Halima Nyundo ana siri moja aliyoificha kwa wateja wake.
Pamoja na kwamba hujitahidi kutafuta vitoweo bora kukidhi mahitaji ya wateja wake, Halima (49) hawezi kuwasaidia wateja wake kutofautisha samaki waliovuliwa kwa njia haramu ya mabomu na wale waliovuliwa kawaida.
“Mimi huwa siwezi kabisa kuwatambua samaki wanaovuliwa kwa mabomu,” amesema Halima ambaye huuza samaki wa rejareja Vijibweni katika wilaya ya Kigamboni jijini hapa.
Halima ni miongoni mwa wachuuzi na walaji wa samaki nchini ambao hushindwa kubaini sifa za samaki halali na wale waliovuliwa kwa njia haramu zikiwemo za mabomu, jambo linalofanya wawe hatarini kula vitoweo vyenye athari kiafya.
Uchunguzi wa Nukta umebaini kuwa licha ya mamlaka kupunguza uvuvi wa mabomu katika ukanda wa pwani kwa asilimia 85, baadhi ya wachuuzi wenye uzoefu wa miaka mingi katika biashara hiyo kama Halima na walaji wana tatizo la kubaini samaki waliovuliwa kwa mbinu hiyo.
Utambuzi wa samaki waliovuliwa kwa mabomu unasaidia kupunguza hatari ya kula vitoweo visivyofaa na kutokomeza kabisa soko la bidhaa hizo zilizovuliwa kwa njia haramu.
Uvuvi haramu wa kutumia mabomu au baruti hutumika na wavuvi ili kurahisisha upatikanaji wa samaki wengi bila kujali madhara yatakayojitokeza kwa walaji, viumbe bahari na mazingira.
Katika uvuvi huo, vilipuzi vya kisasa vilivyotengenezwa kiwandani au vya kienyeji kama mafuta ya petroli ambayo huchanganywa na mbolea katika chupa ya plastiki yenye utambi hulipuliwa baharini ili kupata samaki wengi.
Wavuvi hao haramu huigonga miamba iliyoficha samaki kwa kitu kigumu na huwalipua na mabomu hayo mara baada tu ya kutawanyika.
Zinazohusiana:
- Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar
- Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
- Waziri Mpina aagiza kuvunjwa kwa bodi ya soko kuu la samaki Feri
Wataalamu wanaeleza kuwa kemikali zinazotumika kutengeneza mabomu hayo zina athari kubwa kwa viumbe waliopo baharini na walaji wa samaki na vilevile uharibu makazi ya samaki na mazalia yaliyopo baharini na kusabisha viumbe hao kuhama na baadhi ya samaki kutoweka.
“Nikiangalia samaki nawaona wote sawa tu. Kutambua waliovuliwa kwa njia ya mabomu kama watakuwepo sokoni ni ngumu sana ila Mungu anatuepusha,” anasema Annamaria Kiame (37), ambaye ni miongoni mwa wamiliki wa maduka makubwa ya samaki Kariakoo.
Mkazi wa Vijibweni, Sharifa Mohammed (34) anasema pamoja na kuwa aliwahi kununua samaki kipindi ambacho kulikuwa na samaki wengi waliovuliwa kwa mabomu bado inamuwia vigumu kubainisha tofauti na wale halali.
“Kipindi cha uvuvi haramu, walikuwa wanapatikana samaki wengi ila kwa sasa hivi ni wachache na siwezi kuwatofautisha,” anasema Sharifa.
Baadhi ya walaji ambao hupata tabu kutofautisha samaki hao waliamua kupunguza kula kitoweo hicho muhimu kwa afya wakihofia kuwa huenda wangeuziwa waliovuliwa kwa mabomu ama sumu.
“Mimi ndiyo maana huwa sipendi kula samaki,” anasema Nelson Macha mkazi wa Kariakoo jijini hapa akionesha kukata tamaa.
Licha ya baadhi ya wachuuzi na walaji kushindwa kutambua samaki waliovuliwa kwa mabomu wapo wengine wenye uwezo huo licha ya kuwa hutumia njia za kienyeji kama ladha na mwonekano wa samaki.
Watalaamu hawashauri kutumia ladha kama kipimo kwa kuwa hufanywa baada ya mtu kula samaki jambo linaloweza kuhatarisha afya yake.
Mbinu za kutambua samaki aliyevuliwa kwa mabomu
Mwajuma Mpendu (42) ambaye amekuwa akiuza samaki kwa miaka minne sasa anasema njia za awali za utambuzi wa samaki waliovuliwa kwa mabomu ni pamoja na ulegevu.
“Wanakuwa wamelegea na hata ukiwakaanga wanakuwa wachungu,” anasema Mpendu.
Ukiachana na utambuzi wa kiasili, Afisa Uvuvi Msaidizi wa Soko la Kimataifa la Samaki la Ferry, Ahmed Mbarouk (39) anasema samaki waliovuliwa kwa vilipuzi hubadilika rangi kama alikuwa mwekundu hubadilika na kuwa bluu.
“Ukijaribu kumbinya kwa kidole hudidimia na kuacha alama ya kidole hicho kwenye samaki,” anasema Mbarouk na kuongeza kuwa “samaki wa mabomu wanakuwa na matamvua yaliolainika.”
Mbarouk anasema tangu ameanza kufanya kazi katika soko hilo mwaka 2014 amekuta elimu ikitolewa kwa wavuvi na wananchi na bado wanaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya uvuvi haramu kwa watu na njia za kuwatambua samaki waliovuliwa kwa mabomu.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayesomea masuala ya sayansi ya viumbe bahari, Kaijage Laurian anasema “samaki anakua na macho mekundu kwa kuwa mlipuko unasababisha damu kuvilia machoni”.
“Pia, anakua amelegea kwa sababu mlipuko wa bomu unavunja mifupa hasa uti wa mgongo,” anasema Laurian ambaye ameshiriki katika moja ya miradi ya kukabiliana na uvuvi haramu baharini.
Tamaa ya wavuvi haramu katika kuongeza kipato ndani ya muda mfupi ina gharama ya muda mrefu kwa afya za walaji ikiwemo kusababisha vifo.
Baadhi ya wavuvi hao hutumia vilipuzi bila ya kujua mchanganyiko wa kemikali zilizopo ndani ya vifaa ambavyo wataalam wanaeleza kuwa vina athari kubwa kwa viumbe bahari na wanadamu.
Samaki aliyevuliwa kwa mabomu anakuwa mlegevu, mifupa yake imevunjika na hubadilika rangi hasa kwenye mapezi, jambo linaloweza kuhatarisha afya za walaji. Picha| Moving Sushi.
Kitabu cha mbinu za kubaini uwepo wa vilipuzi (Existing and Potential Standoff Explosives Detection Techniques) kilichochapishwa na Baraza la Utafiti la Wanataaluma wa Marekani (NAS) mwaka 2004 kinaeleza kuwa vilipuzi vingi hutengenezwa na kemikali zinazojumuisha Naitrojeni (Nitrogen), Amonia (Ammonium), risasi (Lead) na unga mweusi (Black powder) ambao hutengenezwa na Salfa (Sulphur) na makaa ya mawe.
Mafuta ya petroli yanayotumiwa na wavuvi wa kienyeji katika vilipuzi vyao nayo hujumuisha kemikali ya zebaki (Mercury) ambayo mtandao wa Live Science, unasema ni hatarishi kwa samaki na mlaji kwasababu husababisha magojwa licha ya kuwa madhara yake huchukua miezi hadi miaka kutokea.
“Kwa akina mama wajawazito wakila sumu ya ‘mercury’ (zebaki) huweza kumsabababishia mimba kuharibika,” anasema Mtaalam wa lishe, Debora Esau kutoka taasisi inayojihusisha na masuala ya lishe ya Partnership For Nutrition Tanzania (Panita).
Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Community Support Initiatives Tanzania (COSITA) mkoani Manyara, Filibert Mwakilambo anasema ulaji wa samaki waliovuliwa kwa njia za mabomu unaweza kuleta tatizo la kukakamaa kwa misuli na matatizo ya upumuaji kwa watu wenye pumu.
“Ile sumu iliyopo kwenye mabomu ina madhara makubwa sana kwenye mwili wa binadamu kwa sababu husababisha ‘paralysis’ (uharibifu wa mfumo wa neva), kufeli kwa seli mwilini na mzio sugu (Chronic Allegy),” anasema Dk Reuben Paul kutoka hospitali ya Hollistic iliyopo Sinza.
Ukiachana na magonjwa mengine, ulaji wa samaki waliovuliwa kwa njia haramu kama mabomu na sumu unaweza kusababisha saratani ambayo pamoja na kusababisha vifo hugharimu fedha nyingi wakati wa matibabu jambo ambalo siyo rahisi kwa mwananchi wa kipato cha chini kulimudu.
“Mlaji wa samaki hao waliovuliwa kwa mabomu au sumu huweza kupata ‘cancer’ (saratani) au magonjwa ya ngozi inategemeana na ‘reaction’ (madhara) ya kemikali,” anasema Dk Ramadhan Mvungi wa Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge jijini hapa.
Licha ya madhara ya kiafya kwa walaji, uvuvi wa mabomu huchangia kuadimika kwa samaki na kupandisha bei ya kitoweo hicho jambo linalofanya watu wakose lishe muhimu mwilini.
“Samaki wa baharini wana madini mengi muhimu ambayo husaidia katika kuimarisha mifupa, meno na katika uzalishaji wa mbegu za kiume,” anasema Mwakilambo huku akibainisha kuwa kukosekana kwa kitoweo hicho kutafanya watu kukosa virutubisho na madini.
Madini hayo muhimu ni pamoja na zinki (zinc), fosforasi (Phosphorus), kalsiamu (calcium), shaba (copper) pamoja na mafuta masafi au fati safi inayoitwa Omega-3 ambayo hayagandi katika mfumo wa damu na ni muhimu kwa afya ya moyo.
“Samaki ni wazuri kwa sababu ni nyama nyeupe ambazo hazina Lehemu (Cholesterol) hivyo wana afya zaidi kuliko nyama nyekundu,” anasema Dk. Ramadhani Mvungi kutoka hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge.
Ili kuwaepusha walaji na uoga wa kuacha kula samaki wa baharini, Mwakilambo anasema ni muhimu kwa wavuvi kuvua samaki kwa njia halali kutokana na umuhimu wake katika lishe.
Kutokomeza uvuvi huo haramu, Serikali imefanya operesheni mbalimbali katika ukanda wa pwani ikiwemo Dar es Salaam ambapo maeneo ya Kimbiji na Kigamboni watu waliokuwa wanafanya shughuli hizo wameacha na wengine wakiyatelekeza makazi yao wakihofia kukamatwa na mamlaka.
“Sasa hivi uvuvi wa kutumia baruti kwa asilimia 90 umekomeshwa, kuna watu walikamatwa na kufungwa,” anaeleza Mbarouk.
Waziri wa Mifugo wa Uvuvi, Luaga Mpina wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ilieleza kuwa katika ukanda wa pwani uvuvi haramu wa kutumia mabomu ulikuwa umeshamiri ambapo “mabomu yalilipuliwa kila kona”.
Kutokana na uvuvi huo hatari, rasilimali za uvuvi zilipungua sana katika maeneo hayo kwa kuwa mabomu huua viumbe vyote vikiwemo mayai, vifaranga na mazalia na kuharibu mfumo mzima wa ikolojia na mazingira. Inakadiriwa kuwa bomu moja likipigwa lina uwezo wa kuharibu eneo la mzunguko wa mita kati ya 15 hadi 20.
Mkurugenzi wa Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi ameiambia nukta.co.tz kuwa Serikali imeweka nguvu za pamoja za taasisi zake ili kupambana na uvuvi huu kupitia kikosi kazi maalum kinachojulikana kama MATT (Mult Agency Task Team) kilichofanya operesheni mbalimbali katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani na Lindi na Mtwara.
“Matokeo yake ni makubwa kwa kukamatwa vifaa vingi vya uvuvi wa mabomu na watuhumiwa/wauzaji wa vifaa hivyo haramu,” anasema.
Ripoti hii maalum imeandaliwa na Nuzulack Dausen, Daniel Mwingira, Rodgers George, Daniel Samson, Tulinagwe Malope na Zahara Tunda.