Zawadi pendwa kwa “mshua” msimu wa sikukuu

Rodgers George 0039Hrs   Disemba 09, 2021 Maoni & Uchambuzi
  • Washua wengi husahau kujinunulia viwalo.
  • Unaweza kumpunguzia gharama za umeme kwa kumwekea mifumo ya umeme jua.
  • Endapo mfuko wako hausomi, muda wako tu unatosha.

Dar es Salaam. Kwa baadhi ya baba zetu, unahitaji kuwa mfuatiliajji ili umpatie zawadia ambayo itamfaa na ataitumia. Nakumbuka niliwahi kumpatia baba yangu zawadi ya shati lakini hakuwahi kulivaa kwa sababu hapendi mashati ya mikono mifupi.

Inauma eh?

Haya kabla haujanunua zawadi kwa ajili ya baba yako kwenye msimu huu, ni vema ukawa na uhakika wa kuwa zawadi hiyo ataipenda na atafurahishwa nayo.

Kati ya zawadi ambazo unaweza kumpatia baba msimu huu wa sikukuu ni hizi:


Mavazi

Wanaume hawasifiki sana kwa kuwa na nguo nyingi. Kwa baadhi jozi mbili za viatu na mashati, suruali kadhaa inatosha kabisa.

Na hata kwenye ngazi ya familia, baba huhudumia familia na kununulia nguo watoto lakini mara nyingi yeye hujisahau. 

Mpatie zawadi ya mavazi msimu huu wa sikukuu. Unaweza kumpeleka kwa ajili ya kufanya mahemezi na kwa ambao wapo mbali, unaweza kumnunulia na kuhakikisha zinamfikia.

Hata hivyo, kumbuka kujua mapendeleo ya mzee wako ikiwemo rangi, muundo na mtindo kabla ya kufanya manunuzi.

Pamoja na viwalo, unaweza kununua viatu vya wazi au vya kufunika, saa na vitu vingine.

Mshua wako kule kijijini anaweza kupata changamoto, msaidie ili amalize uzee wake vizuri. Picha| Gift Mijoe.

Mawasiliano ya kisasa

Mzee wako anatumia simu gani? Jibu unalo. Katika msimu huu wa sikukuu unaweza kusasisha kifaa cha mawasiliano cha mshua.

Huenda anatumia simu ambayo herufi za batani hazionekani tena au simu ambayo kioo kimepasuka na hana dalili za kukitengeneza.

Kama zawadi ya sikukuu, unaweza kununua simu ambayo mzee wako anaweza kuifurahia. Inaweza kuwa simu ya kawaida na hata simu janja.

Simu hiyo mbali na burudani itamsogeza mzee wako karibu na baadhi ya vitu anavyovipenda ikiwemo redio, televisheni na hata  magazeti.


Umemejua

Siyo kila kona ya Tanzania imefikiwa na umeme. Zipo sehemu ambazo umeme wa gridi ya taifa haujafika bado, hivyo wakazi wa maeneo hayo wanatumia mafuta ya taa na betri.

Katika msimu huu wa sikukuu, endapo mzazi wako yupo katika maeneo hayo, unaweza kumnunulia taa zinazotumia umemejua ili aweze kuachana na matumizi ya mafuta ya taa na mabetri.

Taa za sola pia zitamwepushia mshua gharama anazopitia kila mara kununua betri. Pia unaweza kuunganisha nyumba ya mzee na mfumo wa umemejua kabisa ili giza libaki historia.

Endapo uzito wa mfuko wako hausomeki, siyo mbaya, wakati mwingine wazazi wanachopenda kuona ni tabasamu la watoto wao. Funga safari nenda nyumbani na umsalimie mshua wako. Kukuona ukiendelea vema ni zawadi tosha.

Related Post