Zanzibar yazuia ndege kutoka Italia kujikinga na corona

Nuzulack Dausen 0710Hrs   Machi 06, 2020 Habari
  • Yasema zuio hilo la ndege kutoka katika nchi hiyo ya Ulaya litaondolewa hadi hali ya kusamba virusi hivyo itakapotengemaa.
  • SMZ imesema asilimia 40 hadi 60 ya watalii wanaoingia visiwani humo wanatoka Italia.

Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesitisha safari za ndege kutoka na kwenda Italia ikiwa ni moja ya hatua za kujihami dhidi ya kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya corona vinavyosambaa kwa kasi ulimwenguni.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa usitishaji wa ndege hizo unaanzia kesho kwa kuwa tayari leo kuna ndege moja ipo visiwani humo kutoka Italia.

“Ni sahihi kuwa tumesitisha safari za ndege za Italia. Kimsingi ndege tatu zile chartered flights (ndege za kukodi) ambazo hufanya safari zake kuja huku. Sisi hatuna commercial flights (ndege za biashara) zinazotoka moja kwa moja kutoka Italia,” amesema Mohamed.

Mohamed amesema SMZ imesitisha safari hizo mpaka hali ya ugonjwa wa virusi vya corona itakapotengemaa ulimwenguni.

“Waitaliano wanachukua kati ya asilimia 40 hadi 60 ya watalii wanaoingia Zanzibar na ndiyo investors (wawekezaji) wakubwa wa hoteli hapa,” amesema.

Waziri huyo amesema Italia ni moja ya nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo na kwamba ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinabainisha kuwa kesi zinazidi kuongezeka na nyingi ni za ndani.

“Pia, kuna Muitali mmoja amedai amepata virusi vya corona akitokea Zanzibar lakini ukweli ni kwamba sisi hatuna rekodi za kuwa kesi za ugonjwa huo,” amesema Mohamed.


Soma zaidi: 


Mohamed amesema hatua imechukuliwa ikiwa ni moja ya njia ya kudhibiti uwezekano wa kusambaa ugonjwa huo ulioua watu 3,015 hadi jana (Machi 5, 2020) na kuathiri watu zaidi 95,300 katika nchi 86 ulimwenguni huku kesi nyingi zikiwa ni kutoka China.

Amesema Zanzibar haina uwezo mkubwa wa ndani kudhibiti ugonjwa huo hivyo wameona waanze kuchukua hatua mepema wakihofia kuwa ikitokea umefika visiwani humo wasije kuzidiwa.

“Ripoti za WHO zinaonesha ugonjwa huu umesambaa katika mataifa 86 duniani hivi ni bora tukajihadhari mapema. Sambamba na hatua za kuzuia ndege, tumesitisha kongamano la waislamu lililotakiwa kuanza leo na kuhusisha washiriki zaidi 12,000 kutoka nchi mbalimbali duniani,” amesema.

Ripoti ya WHO ya jana inaonyesha kuwa hadi jana Italia ilikuwa ina watu 3,089 walioathirika na virusi vya corona huku watu 107 wakiwa wamepoteza maisha. Kesi zote hizo kutoka nchini humo, kwa mujibu wa WHO, zinasambaa kutoka ndani.

Related Post