Zanzibar yaripoti kifo cha kwanza cha corona, wagonjwa wakiongezeka

April 15, 2020 9:01 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mgonjwa huyo alikuwa mkazi wa Kijichi, Zanzibar mwenye miaka 63 alifariki dunia Aprili 11 nyumbani na kuzikwa siku hiyo hiyo.
  • Wagonjwa wengine sita wabainika visiwani humo na hivyo kufikisha wagonjwa 18 wa Corona.
  • Mpaka leo (Aprili 15, 2020) Tanzania ina wagonjwa 59.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed amesema mgonjwa mmoja wa virusi vya Corona amefariki dunia huku wagonjwa wa ugonjwa huo wakifikia 18 visiwani humo. 

Mohammed katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili 15, 2020) amesema mgonjwa huyo aliyekuwa mkazi wa Kijichi, Zanzibar alifariki dunia Aprili 11 nyumbani na kuzikwa siku hiyo hiyo.

Kifo cha mwanaume huyo mwenye miaka 63 kinafanya Tanzania kuwa na jumla ya watu wanne waliofariki kwa COVID-19 mpaka sasa. 

Mgonjwa huyo aliyefariki ni miongoni mwa wagonjwa sita wapya ambao Mohammed amewatangaza leo na kufikisha wagonjwa 18 kutoka 12 waliotangazwa Aprili 13, 2020.

Visiwa vya Zanzibar ni vya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa corona walioripotiwa nchini ikiwa nyuma ya Dar es Salaam yenye wagonjwa 36. 

Waziri huyo amesema mgonjwa wa kwanza ni mwanaume, Mtanzania (37) mkazi wa Fuoni na wa pili ni mwanaume, Mtanzania (45) mkazi wa Pangawe huku watatu akiwa mwanaume pia, Mtanzania mwenye umri wa miaka 63 aliyefariki Aprili 11.


Zinazohusiana:


Wengine ni mwanaume (60) mkazi wa Kwamchina; mgonjwa mwanaume, Mtanzania (48) mkazi wa Migombani huku wa mwisho akiwa ni mwanamke, raia wa Misri (33) aliyeingia nchini Machi 15 akitokea nchini mwake kupitia Dubai na shirika la ndege la Fly Dubai. 

“Wagonjwa wote ambao ni raia wa Tanzania hawana historia ya kusafiri nje ya nchi hivi karibuni. Wagonjwa wote wamelazwa katika vituo maalum kwa ajili ya kuendelea na matibabu,” amesema Mohammed katika taarifa hiyo.

Kwa idadi hiyo ya wagonjwa wa Zanzibar, Tanzania mpaka sasa ina wagonjwa 59 wa virusi hivyo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

Pia wanakumbushwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima hasa katika masoko na vituo vya daladala na watu wenye dalili za ugonjwa huo wametakiwa kufika katika vituo vya afya ili wafanyiwe uchunguzi. 

Enable Notifications OK No thanks