Waziri Nape aahidi kuboresha maslahi ya wanahabari 2023

Daniel Samson 0300Hrs   Disemba 17, 2022 Habari

Washiriki wa Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 lililofanyika leo Disemba 17, 2022 jijini Dar es Salaam. Picha | Nuzulack Dausen.


  • Asema Serikali itaweka nguvu katika eneo hilo.
  • Pia kuboresha uchumi wa vyombo vya habari ikiwemo kulipa madeni.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mwaka 2023 Serikali itaweka nguvu kubwa katika kuboresha maslahi ya waandishi wa habari ikiwemo mishahara ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Nape aliyekuwa akizungumza leo Desemba 17, 2022 wakati wa Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 jijini Dar es Salaam amesema hakuna maendeleo, amani na furaha katika jamii husika kama uhuru wa habari katika jamii hiyo haupo.

Ili uhuru huo upatikane, amesema moja ya mambo ya kushughulikia ni kuhakikisha maslahi ya waandishi wa habari yanapewa kipaumbele kama ilivyo kwa taaluma nyingine.

“Mwaka unaofuata tutaweka nguvu za kutosha kwenye suala la maslahi ya waandishi wa habari na uchumi wa vyombo vya habari ikiwemo mikataba ya waandishi wa habari ili kuongeza ari katika utendaji wa kazi,” amesema Nape. 

Hata hivyo, Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi amasema maslahi mazuri ya wanahabari yanategemea uchumi na uimara wa vyombo habari wanavyofanyia kazi na kuagiza hilo nalo liangaliwe.

“Ukitaka maslahi ya waandishi yakae vizuri lazima uhakikishe uchumi wa vyombo vya habari unakaa vizuri ikiwemo kulipa madeni,” amesisitiza Waziri huyo. 

Awali akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema vyombo vya habari vinazidai taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali kiasi cha Sh18 bilioni.

Amesema licha ya Serikali kuahidi kulifanyia kazi suala hilo la madeni, mpaka sasa madeni hayo hayajalipwa, jambo linalorudisha nyuma jitihada za vyombo vya habari kutimiza majukumu yao kikamilifu. 

Aidha, Waziri Nape amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha tasnia ya habari nchini ikiwemo sheria, sera na kanuni ili ziendane na hali ya sasa.

"Uhusiano wa Serikali na vyombo vya habari umeendelea kuimarika na zile kelele za hapa na pale kwa kweli zimepungua sana. Hamna watu wanaofungua midomo, hamna watu wanaofuata fuata nyuma, wanaofinywa hivi," amesema Nape. 

Hata hivyo, amewataka wanahabari kutimiza wajibu wao kuhabarisha wananchi kwa uhuru, kuibua mambo ambayo wanaona hayako sawa na kutoa taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya nchi ili kupunguza upotoshaji.

"Wananchi wasipopata taarifa sahihi kwa wakati sahihi unaweza kuwa mwanya kwa wapotoshaji na kuwaaminisha Watanzania kuwa hakuna kinachotekelezwa," amesema.

Related Post