Wavuvi Ziwa Victoria kufaidika na mpango maalum wa hali ya hewa

July 19, 2019 12:17 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Utawawezesha kupata kwa wakati taarifa za hali ya hewa mbaya na kuchukua tahari pale inapotakiwa.
  • Mamlaka za hali ya hewa Afrika Mashariki kushirikishwa ili kuongeza tija kwa wananchi wao. 

Dar es Salaam. Huenda wavuvi wa Afrika Mashariki wanaotumia Ziwa Victoria wakaongeza uzalishaji na kutanua soko la samaki, baada ya kuzinduliwa kwa mpango kabambe utakaohakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Anga (NCRA) imeandaa mpango maalumu wenye lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji wa tahadhari za hali ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Victoria. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, Mpango huo umewekwa wazi wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusaidia shughuli za kijamii na kiuchumi katika Ziwa Victoria (Highway Project to Support Lake Victori Socio Economic activities)  leo jijini Dar es Salaam. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a TMA amesema wanashirikiana na wadau mbalimbali kuongeza ufanisi wa uandaaji na usambazaji kwa wakati wa taarifa za hali ya hewa hususan za hali mbaya ya hewa kwa watumiaji wa Ziwa Viktoria.

“Wadau wa mradi huu wakiwemo wataalam kutoka TMA watakaa pamoja na kufanyia maboresho taarifa zinazoatolewa na Mamlaka na hivyo kufanikisha utoaji wa huduma bora zaidi na kusaidia Serikali katika jitihada za kuhakikisha huduma za hali ya hewa nchini zinachangia katika kufanikisha mikakati na jitihada za nchi kufikia uchumi wa kati na uchumi wa viwanda,” amesema Chang’a.


Zinazohusiana: 


Uvuvi ni moja ya shughuli kuu katika mikoa ya ukanda wa Ziwa Victoria ambapo Shirika la chakula Duniani (FAO)  linakisia kuwa zaidi ya Watanzania 280,000 wameajiriwa katika shughuli za uvuvi zikiwamo wavuvi, waanika samaki, wakaanga samaki, wanunuzi na wachuuzi wa samaki, watengeneza nyavu, wajenzi wa mitumbwi na wafanya matengenezo ya mitumbwi.

Viwanda  zaidi ya kumi vimejengwa kuchakata samaki kwenye Ziwa Victoria ambao huwasafisha, kuwakata kwenye minofu, kuwaweka kwenye maboksi  na kuwasafirisha samaki nje, 

Kwa mujibu wa Taasisi ya Uvuvi wa Ziwa Viktoria (LVFO) iliyopo chini ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zaidi ya Dola za Marekani 650 milioni (takribanSh1.48 trilioni) hupatikana kutokana na mauzo ya samaki na mzao yake kila mwaka.

Akizungumzia mradi huo uliozinduliwa jana, Mtaalam wa Miradi kutoka NCRA, Rita Roberts amesema utasaidia Kanda ya Afrika Mashariki kupitia taasisi zake za hali ya hewa kufanikisha utoaji endelevu wa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa wakati pamoja na kuongeza kiwango cha usahihi na uhakika wa taarifa za hali ya hewa na hivyo kupunguza athari za vifo na upotevu wa mali.

Mradi huo unahusisha taasisi za Hali ya Hewa za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na NCRA kutoka Marekani na Taasis ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UKMet Office) kwa ufadhili wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) ya Uingereza.

Enable Notifications OK No thanks