Wasomi waanika mbinu zitakazosaidia Tanzania kuwa nchi ya viwanda

May 3, 2019 8:26 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Washauri iachane na mipango isiyotekelezeka na viongozi wajikite katika kutengeneza falsafa na itikadi ya kuendesha uchumi.
  • Juhudi zielekezwe katika kuongeza watalaam na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya nishati ili kupunguza upotevu wa umeme.
  • Waeleza kuwa uchumi wa viwanda utafanikiwa ikiwa Serikali itaimarisha mfumo wa utoaji wa haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na haki za kijinsia.

Dar es Salaam. Wasomi nchini wameshauri mambo mbalimbali yatakaiyosaidia Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kufikia adhma ya kujenga uchumi wa viwanda ikiwemo kuimarisha mfumo wa utoaji haki, taarifa, uwajibikaji na ujenzi wa miundombinu.

Wanazuoni hao waliokuwa wakiongea katika kongamano kuhusu hali ya uchumi na siasa nchini lililofanyika leo (Novemba 1, 2018) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) lililolenga kutathmini miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza sera ya viwanda, adhma ya kuwa nchi ya viwanda itafikiwa iwapo kutakuwepo na mikakati imara inayotekelezeka.

Profesa wa masuala ya uchumi nchini Humphrey Moshi amesema ili Tanzania ifanikiwe katika ujenzi wa viwanda iachane na mipango isiyotekelezeka na viongozi wajikite katika kutengeneza falsafa na itikadi ya kuendesha uchumi kwa kuimarisha utendaji wa sekta ya umma na binafsi.

Amesema msingi imara wa kujenga viwanda lazima uende sambamba na sera za kitaifa ambazo zinalenga kuimarisha taasisi zinazohusika na viwanda ili kutumia vizuri fursa za masoko na teknolojia za kimataifa zitakazochochea maendeleo kwa wananchi.

“Serikali ni lazima ikae mstari wa mbele wakati wa kuendeleza viwanda, tulikaa miaka 25 tukisubiri sekta binafsi ituletee umeme, kilimo cha miwa. Tumarishe mahusiano na nchi hizo tupunguze utegemezi kwa nchi za magharibi,” amesema Prof. Moshi ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushindani nchini (FCC).

Mhadhili wa UDSM, Prof. Hudson Nkotagi, ambaye ametoa mada ya nishati na miundombinu, amesema kuna haja ya kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa nishati ikizingatiwa kuwa umeme unaozalishwa kwa sasa nchini haukidhi mahitaji yaliyopo. 

Amesema juhudi zielekezwe katika kuongeza watalaam na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya nishati ili kupunguza upotevu wa umeme ambao unaweza kutumika kuendesha viwanda vidogo vidogo. 

“Napendekeza Serikali iweze kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati, kuongeza wataalam wa nishati, kufanya tafiti zaidi na kuwawezesha watafiti katika sekta ya nishati,” amesema Prof. Nkotagi. 

   

Kwa sasa uwezo wa nchi kuzalisha umeme umefikia megawati 1,560 ambapo chanzo kikubwa ni umeme unaotokana na maji, gesi na makaa ya mawe lakini Serikali inakusudia kujenga wa mradi wa Stiegler’s Gorge katika Pori la Akiba la Selous kuzalisha megawati zaidi ya 2,100 ili kumaliza tatizo la umeme.


Zinazohusiana:


Mbali na sera za kiuchumi, aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM, Prof. Rwekaza Mukandala amesema uchumi wa viwanda utafanikiwa ikiwa Serikali itaimarisha mfumo wa utoaji wa haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na haki za kijinsia. 

Prof. Mukandala ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kuelewa changamoto za kisiasa na kijamii zinazowakabili wananchi ili kuweka mipango thabiti ya kitaasisi katika kushughulikia vipaumbele vya ujenzi wa viwanda. 

Uchumi wa viwanda unategemea zaidi muunganiko wa sera na falsafa za sekta mbalimbali. Picha| Mwananchi.

“Tunahitaji kukipeleka Kiswahili nchi za nje kwenye balozi zetu. Mabalozi wafundishwe Kiswahili. Google wanasema Kiswahili Kenya, kwanini sio Kiswahili Tanzania? Tunarudi nyuma kwa kukataa vitu vyetu,” amesema Profesa Profesa Martha Qorro ambaye ni mtaalamu wa lugha.

Prof Qurro amesema kuna umuhimu kuangalia upya matumizi ya lugha ya Kiswahili  na kuhimiza falsafa za mawasiliano ya maendeleo ili kutengeneza mfumo mzuri wa upatikanaji wa taarifa zitakazosaidia kuunganisha nguvu kazi ya Taifa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ambaye amezungumzia huduma za jamii amesema utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na washiriki wa kongamano hilo unategemea zaidi uwajibikaji katika taasisi za umma na viongozi kufanya maamuzi sahihi bila kujali gharama za kisiasa.

Kongamano hilo limewakutanisha wasomi na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini ambapo limebeba kauli mbiu ya Miaka mitatu ya ya Serikali ya Awamu ya Tano: “Tunatoka wapi, Tuko wapi na Tunakwenda wapi”

Enable Notifications OK No thanks