Wasafirishaji vyakula wanavyoweza kujikinga na Corona

July 14, 2020 7:13 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka pamoja na kuzingatia umbali wa mita moja wanapowasilisha chakula kwa mteja.
  • Hata hivyo, ugonjwa wa Corona unaambukizwa kwa njia ya mfumo wa upumuaji na siyo chakula.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa ugonjwa wa virusi vya Corona upo katika maeneo mbalimbali duniani, lazima maisha na shughuli zingine ziendelee. 

Hata hivyo, hiyo haiondoi hofu kwa baadhi ya watu ambao wanashindwa kufanya vitu fulani kwa kuhofia kupata maambukizi ya COVID-19. 

Kati ya vitu hivyo ni pamoja na huduma za chakula na usafiri ambazo zinazohusisha muingiliano wa watu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo kwa watoa huduma za chakula ambao utasaidia kujikinga na COVID-19 wakati wakitoa huduma hizo kwa wateja wao.

WHO imesema wafanyakazi wanaosafirisha na kusambaza vyakula kwa wateja wao wanatakiwa kuzingatia tahadhari ya usafi kwa sababu wanakutana na watu tofauti. 

Wakati wanatoa huduma hizo wanapaswa kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya na kuitupa mahali salama baada ya matumizi. 

Pia, wanatakiwa kuvaa barakoa, kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja na mwingine na kutakasa vifaa vya kazi yakiwemo magari ili kuepuka maambukizi. 

Nawa mikono kabla na baada ya kutoa huduma.


Zinazohusiana


Chakula hakiambukizi Corona

Kwa upande wa hofu ya watu kuogopa chakula kinachosambazwa au kuuzwa migahani, WHO imesema hadi sasa hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa chakula kinaweza kuambukiza Corona.

Pia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) limesema ugonjwa wa Corona unaambukizwa kwa njia ya mfumo wa upumuaji na siyo chakula.

“Virusi vya Corona haviwezi kuongezeka kwenye chakula. Vinahitaji mwili wa mnyama au binadamu kuongezeka. Uwezekano wa mtu kupata virusi vya corona kutoka kwenye vyakula na vifungashio ni mdogo,” imeeleza sehemu ya taarifa ya FAO. 

Kama ulikuwa ukihofia chakula unachonunua, ondoa shaka na endelea kukitumia kama kawaida.

Enable Notifications OK No thanks