Walichokisema wadau wa elimu ufaulu matokeo kidato cha nne

January 11, 2020 7:29 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wamesema ni wakati sasa Serikali ianze kufikiri juu ya kubadili lugha ya kufundishia
  • Japo ufaulu umependa, wameshauri wanafunzi kufundishwa kujitambua na stadi za maisha. 
  • Wataka waliofeli wasibezwe bali wasaidiwe kutimiza ndoa za elimu.

Dar es Salaam. Kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2019, wadau wa elimu wamesema licha ya ufaulu kuongezeka kidogo, ipo haja ya kuboresha mfumo wa utoaji elimu Tanzania kupunguza idadi ya wanafunzi wanaofeli kila mwaka na kushindwa kuendelea na masomo. 

Matokeo hayo yaliyotangazwa Januari 9, 2020 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde yanaonyesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa kutoka asilimia 79.27 mwaka juzi hadi asilimia 80.65 mwaka jana.

Pia watahiniwa 340,914 sawa na asilimia 48.6 ambayo ni takriban nusu ya ya watahiniwa wote wamefaulu kwa daraja IV huku shule za Serikali zikipata upinzani mkali na kushindwa hata kuingiza shule hata moja katika 10 bora kitaifa. 

Licha ya kuwa kipindi hiki ni kigumu kwa wazazi na wanafunzi waliofeli na shangwe kwa wale ambao wamefanya vizuri ambao wataendelea na masomo ya kidato cha tano, wachambuzi wa masuala ya elimu wamesema matokeo hayo yanafikirisha sana. 

Mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Shule Direct, Iku Lazaro amesema anafurahishwa na jinsi watoto wa kike walivyofanya vizuri hasa kuingia wengi kwenye 10 bora ya wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa.

Amesema bado jitihada zinahitaji kuboresha elimu ya wasichana nchini ikizingatiwa kuw akatika mtihani huo wasichana 45,311 ambao ni sehemu ya asimia 19.35 ya watahiniwa waliopata daraja sifuri yaani wamefeli kabisa. 

Hiyo ina maana kuwa wasichana hao hawatapata fursa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka huu.

“Bado kuna njia ndefu kuelekea kupata matokeo mazuri. Tunaona watahiniwa asilimia 48.6 wamepata daraja la IV jambo linaloonyesha kuwepo kwa hatihati ya wao kutojiunga na elimu ya juu na hata ya ufundi,” amesema Lazaro ambaye anaamini elimu ya sekondari ni muhimu kwa wote na kuna haja ya kuweka mikakati ili iwanufaishe walengwa.

Naye Mwandishi wa vitabu na mdau wa elimu, Richard Mabala amesema ipo haja ya kufanya mabadiliko kwenye sekta ya elimu ikiwemo kuboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji ili kuokoa wanafunzi ambao wameshindwa kufanya vizuri. 

Hata hivyo, Serikali imesema itaendelea kuboresha mfumo wa elimu nchini ili kuongeza kiwango cha ufaulu. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa elimu kwa kuboresha Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule kwa lengo la kuhakikisha Elimu inatolewa kwa kiwango ili kupata matokeo na wahitimu bora. pic.twitter.com/YgulvF0sw0

Ipo haja ya kubadilisha lugha ya kufundishia

Mabala ambaye ameonyesha kusikitishwa na wimbi kubwa la watahiniwa waliofeli amesema anaiona haja ya wanafunzi kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili ili kusaidia kuongeza ufaulu wao.

“Tunawatesa watu ambao wanaishi katika mazingira ambapo hakuna Kiingereza kabisa. Halafu wanaingia form one (kidato cha kwanza) hawana Kiingereza lakini bado tunawalazimisha kusoma masomo yote kwa Kingereza,” amesema mabala.

Mdau huyo wa elimu amesema msingi wa elimu ni lugha na endapo wanafunzi watafundishwa kwa lugha ambayo hawaielewi, ni vipi nchi itegemee matokeo mazuri.

“Elimu msingi wanatumia Kiswahili ni lugha ambayo wanafunzi wanaielewa. Kama wanalazimishwa kusoma kwa lugha ambayo hawaielewi, lazima watu watafeli halafu tunaharibu maisha yao,” amesema Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika la HakiElimu.

Wanafunzi wafundishwe stadi za maisha

Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa, Joan Ritte amesema ili kuongeza ufaulu siku zijazo, ipo haya kwa Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafundishwa juu ya changamoto za ukuaji hasa zile zinagusa mabadiliko ya maumbile na mahusiano.

Amesema wakati mwingine wanafunzi wanajichanganya na makundi yasiyofaa, jambo linalowapotezea muda na mwelekeo wa kuwekeza nguvu zao kwenye masomo. 

“Vijana tuna changamoto nyingi sana na baadhi yake ni ukuaji. Itapendeza kama vijana watapewa elimu yakupambana na changamoto za ukuaji na hasa kama ikianzia kwenye ngazi ya familia,” amesema Joan.


Zinazohusiana


Naye Modester Cosmas mhitimu wa kidato cha nne 2019 kutoka shule ya Bright Future  ya jijini Dar es Salaam amesema wapo wanafunzi ambao hawajafundishwa kujitegemea ambao huhitaji mtu wa kuwakumbusha kusoma kana kwamba siyo kwa manufaa yao.

“Unakuta mtu akiwa shuleni hasomi, yeye ni michezo tu, sasa ukichanganya hilo na akakutana na mwenzake mwenye hulka hiyo basi hawamwambii kitu. Mwisho wake wote wanafeli,” amesema Modester ambaye yeye ana ufaulu wa Daraja la I.

Kuandaa mifumo inayoruhusu kuendeleza vipaji

Mabala amesema ipo kasumba iliyojengeka kuwa mtu ni lazima aingie kidato cha tano, cha sita na kisha chuo kikuu ili kufanikiwa malengo yake lakini ipo haja ya Watanzania kubadilisha mtazamo kama Kenya ilivyofanya kupitia baadhi ya vyuo vikuu kutoa elimu ya ufundi. 

“Kuna umuhimu wa kuangalia mambo mengine ya kufanya. Tuna vyuo vya veta ambazo vinahitaji kuboreshwa. Tusione kwenda form V na VI kama njia pekee ya kufanikiwa.

“Haina maana ya kuwa sipendi kuona watu wanaenda kidato cha V na VI,” amesisitiza Mabala ambaye anatamani kuona wanaosimamia elimu wakifanya uchunguzi kwenye matokeo haya ili kuibua matatizo yanayohitaji suluhu kwa maendeleo ya elimu ya Watanzania.

Mdau huyo pia amesema kuna haja ya kuangalia jinsi ya kuendeleza vipaji walivyo navyo kwa sababu walioferi “elimu waliyoipata ni ndogo. Hilo ndilo tatizo. Hawana maarifa ya kutosha na ndio maana wameshindwa kujibu maswali ya mitihani na kufaulu. Hilo ndilo tatizo kuu.”


Wanafunzi waliofeli wasibezwe

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Jesca Laurent amesema wapo wazazi ambao watawachukia watoto wao kwasababu wamefeli kidato cha nne. Zaidi wapo ambao watawapeleka shamba kulima wakidai kuwa watoto hao hawana msaada kwao.

“kwa watoto hao maisha ndiyo yanaanza. Ukimbeza na kumshtumu huku hata wewe hukumnunulia vitabu wala kumfuatilia alipokuwa shuleni ni sawa na kazi bure. Kama ana mdogo wake basi hakikisha haurudii makosa uliyofanya hapo awali,” amesema Jesca ambaye ni mama mzazi wa Modester ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa kidato cha nne 2019,

Mzazi huyo amesema hata kwa ambao watoto wamefaulu, wasibweteke kwani sifa siku zote hulevya. 

Enable Notifications OK No thanks