Wajasiriamali 5 kuiwakilisha Tanzania jukwaa la uwekezaji Afrika

September 18, 2018 6:04 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  •  Lengo la jukwaa hilo ni kutafuta njia mbadala za kukabiliana na tatizo la lishe katika nchi za Afrika.
  •  Viwanda hivyo vimeonyesha uwezo mkubwa wa kibunifu katika sekta ya lishe nchini.
  •  Watakutanishwa na wenzao wa nchi za Afrika ili kubadilishana uzoefu wa teknolojia ya chakula na lishe.

Dar es Salaam. Wamiliki 5 wa viwanda vidogo na kati nchini wamechaguliwa kushiriki katika jukwaa uwekezaji linalotarajiwa kufanyika nchini Kenya ikiwa ni sehemu ya kutafuta njia sahihi za kuondokana na tatizo la lishe katika nchi za Afrika. 

Waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania ni  wamiliki wa  viwanda vya East Africa Fresh Fruits, Crop Bioscience, AFCO Investment, Health Maisha na Kibaigwa Flour ambavyo vinajihusisha na masuala ya kilimo na lishe.

Hatua hiyo ni matokeo ya shirika la kimataifa katika masuala ya kukuza lishe (Global Alliance for Improved Nutrition(GAIN)) wakishirikiana na  SUN Bussiness Network waliandaa mashindano ya ndani ya nchi kupata washindi watano watakaoiwakilisha Tanzania katika Jukwaa la wawekezaji Afrika ili  kukuza viwanda vidogo na vya kati kwenye sekta ya lishe  na kuwaandaa kuwa wawekezaji wakubwa.

Lengo ni kutumia teknolojia na ubunifu wa kuunda viwanda vitakavyoweza kupambana na changamoto za lishe katika nchi za Afrika ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao wanaathirika zaidi kutokana na ukosefu wa usalama wa chakula.  

Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula (WFP) inaonyesha asilimia 34 ya watoto Tanzania wamedumaa kutokana na  utapiamlo, huku wanawake wakiwa wahanga wa anaemia na tatizo la kuongezeka kwa uzito wa kupitiliza pamoja na unene linazidi kuongezeka. 

Wafanyabiashara viwanda vidogo na wabunifu katika lishe walipata nafasi ya kuwakilisha mawazo yao kwa majaji kama moja ya njia ya kufuzu mafunzo ya kuwasilisha wazo la kiuwekezaji katika lishe. Picha| Arnold Tibaijuka

Mchakato wa mashindano hayo ulipatikana kwa kuitumia taasisi ya Sahara Ventures ambayo inatoa jukwaa kwa vijana na kampuni zenye mawazo ya kibunifu kufaidika na fursa mbalimbali zinazojitokeza duniani. 

Taasisi hiyo aliratibu zoezi la kupata wajasiriamali wenye mawazo na maandiko bora ambapo walichuja watu 52 kutoka kampuni ndogo na za katika kupitia maombi yaliyotumwa Julai 2018 na kuwapata 20 waliopewa mafunzo ya siku 10 ya kuandaa mawazo yao ya biashara katika mlengo wa uwekezaji katika sekta ya lishe .

“Sisi tulipewa jukumu la kuwafundisha wajasiriamali hao ambao kuhusu mbinu za biashara na masoko,” anasema Emmanuel Senzige kutoka Sahara Venture.


Zinazohusiana: Wavuvi watahadharishwa kupungua samaki Ziwa Victoria

                            Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara


Wajasiriamali 20 ambao waliwasilisha bidhaa zao na mawazo yao katika masuala ya lishe baada ya mafunzo walichujwa mbele ya majaji na kufanikiwa kupatikana wajasiriamali watano ambao wataiwakilisha Tanzania kwenye jukwaa la uwekezaji litakalofanyika Nairobi nchini Kenya.

Licha ya kupatikana kwa wajasiriamali hao lakini bado kuna changamoto kwa wabunifu wengi na wajasiriamali kutokutumia fursa nyingi zilizopo katika mitandao ambazo zingewapelekea kufanya vizuri zaidi na kupatiwa mafunzo ya kuboresha biashara zao na hata kupewa mtaji.

“Tanzania kuna fursa nyingi kupitia mitandao ya kijamii, wabunifu watumie nafasi hii,” amesema Senzige.

Enable Notifications OK No thanks