Usawa wa kijinsia unavyojipambanua katika sekta ya ajira Tanzania

January 28, 2022 7:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza kuwa hakuna mabadiliko makubwa ya mgawanyo wa ajira kisekta kwa kutumia tafsiri ya kitaifa kati ya mwaka 2014 na 2020/21 japokuwa ajira katika Serikali Kuu una Serikali za Mitaa zilisinyaa. 

Mabadiliko makubwa ya mgawanyo wa ajira yameonekena miongoni mwa watu walioajiriwa katika sekta ya kilimo (66.8% 2014 na 58.4% 2020/2021) na shughuli nyingine binafsi za kiuchumi zisizo za kilimo (mwaka 2014 asilimia 26.6, na mwaka 2020/21 asilimia 22.7).

Ripoti hiyo ya Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi ya mwaka 2020/21 imesema kuwa kusinyaa kwa kiwango cha waajiriwa Serikalini kunatoa taswira kamili ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kati ya mwaka 2015 na 2020 ambapo zilitolewa ajira mpya chache. 

“Pamoja na hatua hizo kusaidia kupunguza kukua kwa kiwango cha mishahara ya Serikali, kunaweza kuathiri utekelezaji wa sera kama zilivyopangwa kutekelezwa katika mikakati na mipango ya Serikali,” imeeleza ripoti hiyo. 

Aidha, kupungua kwa kiwango cha ajira katika sekta binafsi za kiuchumi zisizo za kilimo kunaashiria uwekezaji mdogo katika sekta hizo ama uwekezaji umejikita katika maeneo yanayohitaji nguvu kazi kidogo. 

Hali hii inatoa ujumbe kwamba zinahitajika juhudi kubwa kuvutia uwekezaji na biashara zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hasa kwa wanawake ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Enable Notifications OK No thanks