Ufuta, alizeti vyachangia kuporomosha uzalishaji mazao ya mafuta Tanzania
- Uzalishaji wa mazao hayo ulishuka kwa asilimia 75.9 hadi tani milioni 1.6 mwaka juzi kutoka tani milioni 6.6 zilizorekodiwa mwaka 2017.
- Mabadiliko ya bei, hali ya hewa vyachangia kushusha uzalishaji.
- Serikali yasema imeongeza nguvu ya uzalishaji wa mbegu bora na itatumia minada ya pamoja kuuza mazao hayo ili kumfaidisha mkulima.
Dar es Salaam. Uzalishaji wa mazao ya mafuta umeshuka kwa zaidi ya mara nne hadi kufikia tani milioni 1.6 mwaka 2018 ukichagizwa na ukosefu wa soko la uhakika na bei ya kuridhisha kwa mazao hayo ambayo yamekuwa yakitumika katika uzalishaji mafuta ya kula nchini.
Mazao ya mafuta hujumuisha alizeti, karanga, ufuta, michikichi (mawese) na soya ambayo yakivunwa huzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta ya kula yanayotumika katika shughuli za mapishi.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kinaeleza kuwa uzalishaji wa mazao hayo ulishuka kwa asilimia 75.9 hadi tani milioni 1.6 mwaka juzi kutoka tani milioni 6.6 zilizorekodiwa mwaka 2017.
Kushuka kwa uzalishaji wa mazao hayo kulichangiwa zaidi na zao la ufuta ambalo ulishuka kwa asilimia 89.7 likifuatiwa na alizeti kwa asilimia 75.3 na karanga (asilimia 71).
Hata wakati uzalishaji wa mazao manne ya mafuta ukishuka kwa kasi katika kipindi hicho, ni soya pekee ambayo uzalishaji wake uliongezeka.
Kitabu hicho kinaeleza kuwa uzalishaji wa soya ulipanda zaidi ya mara tatu kutoka tani 6,135 mwaka 2017 hadi tani 21,321 mwaka juzi ikiwa ni ongezeko la asilimia 247.5.
Licha ya uzalishaji wa soya kuongezeka kila mwaka, mchango wa soya ni mdogo kwa kuwa ndiyo zao ambalo uzalishaji wake uko chini zaidi kuliko mazao yote ya mafuta ambayo yameanishwa katika kitabu hicho.
Mathalan, uzalishaji wa alizeti ambao ulishika nafasi ya kwanza mwaka 2018 kati ya mazao ya mafuta ulikuwa mara 36 ya ule wa soya ambayo mwaka huo zilizalishwa tani 21,321 pekee.
“Uzalishaji wa zao la soya uliongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji yake na hivyo wakulima kuhamasika na kuzalisha kwa wingi,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho.
Kuporomoka kwa uzalishaji mazao ya mafuta katika kipindi cha mwaka mmoja kwa asilimia 75.9, ni jambo linaloibua maswali mengi ikizingatiwa kuwa uzalishaji wake umekuwa ukipanda kila mwaka tangu mwaka 2012.
Mwaka 2012 uzalishaji wa mazao hayo ulikuwa tani milioni 2.5 zikapanda hadi kufikia tani milioni 6.6 mwaka 2017 kabla ya kushuka kwa kasi mwaka uliofuta hadi tani milioni 1.6, kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa ndani ya miaka nane iliyopita.
Mazao hayo yamekuwa yakiuzwa katika masoko mbalimbali nchini na kusafirishwa nje ya nchi isipokuwa zao la michikichi ambalo linazalisha mafuta ya mawese.
Sababu za kushuka kwa uzalishaji
“Upungufu huo ulitokana na ukosefu wa soko la uhakika na bei ya kuridhisha kwa mazao hayo,” inasomeka sehemu ya kitabu hicho ambacho kilichochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Serikali imesema kuwa mabadiliko ya hali hewa na bei ya mazao hayo zilichangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa uzalishaji katika kipindi hicho, jambo lililowavunja moyo wakulima kuwekeza nguvu zao katika aina hiyo ya mazao.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa mbali na hali hewa kuna tatizo la kutokuwepo ‘price discovery’ (uwezo wa kung’amua bei halisi kulingana na gharama za uzalishaji na yenye manufaa kwa mkulima).
“Hii inamfanya mkulima akate tamaa kurudi shambani,” amesema.
Licha ya kuwa mazao hayo kuwa na umuhimu mkubwa nchini Tanzania, bado mchango wake ni mdogo katika upatikanaji wa mafuta ya kula, jambo linaloilazimisha Serikali kuagiza mafuta ya kula hasa mawese nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya walaji.
Soma zaidi:
- Kigoma kinara wa usajili mashamba Tanzania bara
- Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika
- Fursa zilizojificha uzalishaji wa michikichi Tanzania
Fursa iliyojificha
Inakadiriwa kuwa Tanzania inaagiza tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese na hutumia takriban Sh600 bilioni kila mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kufidia pengo la uhaba wa mafuta hayo.
Kitabu namba 5 cha Utayarishaji, Usindikaji na Hifadhi ya Mazao ya Mbegu za Mafuta baada ya kuvuna kilichotolewa na Wizara ya Kilimo kinaeleza kuwa uzalishaji mdogo wa mazao haya umetokana na wakulima wengi kutozingatia kanuni za kilimo bora kama vile kupanda aina ya mbegu zenye kutoa mafuta mengi, jambo ambalo linafanya mafuta yanayozalishwa kutotosheleza mahitaji ya walaji.
Pia wakulima wengi hutegemea kuuza mazao ya mbegu za mafuta kwa wasindikaji wadogo wanaotumia mashine ndogo ndogo zilizosambaa katika maeneo mengi yanayozalisha mazao hayo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka Dkt. Filson Kagimbo (wa pili kushoto) kuhusu uoteshaji wa miche bora ya michikichii alipotembelea kitalu cha kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga kilichopo wilayani Kigoma, Februari 21, 2020. Kushoto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba na wanne kushoto ni Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Serikali kunusuru hali
Serikali imeeleza kuwa imeanza kufufua mazao ya mbegu za mafuta ikiwemo kuhimiza kilimo cha michikichi kwa uzalishaji wa mbegu bora za mazao hayo katika vituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) ili kusambaza wakulima.
“Sasa hivi tuna programu ya kuhakikisha kwamba taasisi yetu ya Tari inasambaza miche ya kutosha ya mazao ya pamba na michikichi. Miche mingi ya michikichi iliyopo Kigoma imezeeka, kwa hiyo tunafanya replacement (tunabadilisha) kwenye maeneo ya uzalishaji na tumeanzisha vitalu vipya vya miche kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo katika maeneo hayo kuongeza idadi,” amesema Bashe.
Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini amesema wanashirikiana na sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu bora na ununuzi wa mazao hayo bila kuingilia soko ili kuwafaidisha wakulima waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Ili kuhakikisha wakulima wanapata bei inayolingana na uzalishaji wa mazao yao, Serikali imesema itatumia mfumo wa minada kuuza mazao ya mafuta ikiwemo ufuta kuwezesha wakulima kunufaika na kilimo chao.
“Kwa hiyo kwa sasa mazao yote haya ya ufuta, soya…tumeenda mbali zaidi tunataka tuyauze kwa mfumo wa minada katika vijiji vya kula kwa mfumo wa stakabadhi gharani. Tunafanya jitihada hizo kuhakikisha mkulima anapata bei stahiki ya zao lake,” amesema Bashe.
Amebainisha kuwa mwelekeo wa wizara yake kwa sasa ni kuongeza nguvu katika uzalishaji wa michikichi na alizeti utakaosaidia kupunguza uagizaji na bei ya mafuta toka nje ya nchi ili kuwawezesha wananchi kupata mafuta ya kula kwa bei nafuu.