Fahamu marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge leo Januari 29, 2025
- Ni pamoja na Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji Fedha Haramu pamoja na Sheria ya Tasnia ya Pamba.
Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limepitisha Miswada miwili ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3 na Na. 4) ya mwaka 2024 katika kikao kilichofanyika leo, Januari 29, 2025, jijini Dodoma ili kuimarisha utekelezaji wake na kuhakikisha zinakidhi mahitaji ya sasa.
Akiwasilisha miswada hiyo bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, alisema kuwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) unapendekeza marekebisho katika sheria sita.
Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji Fedha Haramu (Sura ya 423), ambayo ilitungwa mwaka 2006 kwa lengo la kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na silaha za maangamizi.
Tangu kutungwa kwake, sheria hiyo imefanyiwa marekebisho mara sita ili kuhakikisha Tanzania inafuata viwango vya kimataifa vya udhibiti wa fedha haramu.
Marekebisho mapya yanahusu kifungu cha 19(a), kinachompa mamlaka mdhibiti kuweka vikwazo vya kiutawala pale ambapo sheria haijaainisha mamlaka hiyo.
Sheria nyingine iliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Vyama vya Ushirika (Sura ya 211), iliyotungwa mwaka 2013 kwa madhumuni ya kuanzisha mfumo wa maendeleo ya vyama vya ushirika.
Marekebisho yaliyopendekezwa katika sheria hii yanahusisha kifungu cha 12, ambacho kinawapa wasajili wasaidizi uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, kifungu cha 19 kinapendekezwa kufutwa na kuandikwa upya ili kuboresha muundo wa vyama vya ushirika na kuimarisha ushirikiano kati ya wanachama wake.
Vifungu vingine vinavyopendekezwa kurekebishwa ni kifungu cha 20, 31, 55, 72, 73, 74, 75, 81, 141, pamoja na kuongeza kifungu kipya cha 21(a).
Pia, marekebisho yanahusisha Sheria ya Tasnia ya Pamba (Sura ya 201), ambayo ilitungwa mwaka 2001 kwa lengo la kuanzisha Bodi ya Pamba Tanzania ili kusimamia udhibiti, uboreshaji na uendelezaji wa sekta ya pamba nchini.
Tangu kutungwa kwake, sheria hiyo imefanyiwa marekebisho mara moja, ikiwa na lengo la kuimarisha shughuli za maendeleo ya tasnia ya pamba, hususan katika maeneo ya ukaguzi wa mbegu za pamba, nyuzi za pamba na viwanda vya uchakataji wa pamba.
Miongoni mwa marekebisho yaliyopendekezwa ni kubadilishwa kwa cheo cha Cotton Inspector na kuwa Agriculture Officer, ambapo wajumbe wa Bunge walikubaliana kukiacha kama kilivyo.
Vifungu vingine vinavyopendekezwa kurekebishwa ni kifungu cha 11, 26, 29(a), 38(a), 37, na kuongeza kifungu kipya cha 38(b).
Muswada huo pia unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji wa Kiuchumi (Sura ya 386), iliyotungwa mwaka 2005 kwa lengo la kuanzisha Baraza la Taifa la Uwezeshaji wa Kiuchumi.
Sheria hii inalenga kukuza na kuwezesha shughuli za uzalishaji wa mapato na mali kwa Watanzania, kuweka mfumo wa kisheria na kitaasisi kwa Baraza, kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji wa Kiuchumi, na kuweka utaratibu wa udhibiti wa masuala ya fedha katika halmashauri na mfuko huo.
Hadi sasa, sheria hii haijawahi kufanyiwa marekebisho, na hivyo hii ni mara yake ya kwanza. Miongoni mwa vifungu vinavyopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni kifungu cha 3, ambacho kinaboresha tafsiri ya baadhi ya misamiati iliyotumika lakini haikufafanuliwa katika sheria.
Vifungu vingine ni kifungu cha 5, 27, 28, 38 na 39.
Sheria nyingine inayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji (Sura ya 435), iliyotungwa mwaka 2013 kwa lengo la kuweka masharti ya kuanzishwa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, pamoja na kuweka utaratibu wa uendelezaji, uendeshaji na matengenezo ya mifumo ya umwagiliaji ili kutekeleza Sera ya Taifa ya Umwagiliaji.
Johari alibainisha kuwa sheria hii haijawahi kufanyiwa marekebisho tangu kutungwa kwake, na hivyo marekebisho mapya yanalenga kuboresha masharti ya utekelezaji wake.
Kifungu cha 2 kimependekezwa kurekebishwa kwa kuongeza tafsiri ya misamiati mbalimbali iliyotumika lakini haikufafanuliwa katika sheria ya awali.
Vifungu vingine vinavyopendekezwa kurekebishwa ni kifungu cha 3, 4, 5, 29 na 31, ambapo marekebisho haya yanahusisha pia marekebisho ya makosa ya kiuandishi na kuongeza uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umwagiliaji.
Marekebisho pia yanahusisha Sheria ya Ukaguzi wa Umma (Sura ya 418), iliyotungwa mwaka 2018 kwa lengo la kumpa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali uwezo wa kufanya ukaguzi wa hesabu za umma.
Sheria hii inalenga kukuza uwajibikaji katika taasisi za serikali kwa kuzuia ubadhilifu wa fedha, rushwa, na utoaji wa taarifa kwa walipa kodi kuhusu utekelezaji wa sera na programu za serikali.
Marekebisho yaliyopendekezwa katika sheria hii yanahusisha kuongeza kifungu kipya cha 4(a), ambacho kinalenga kuweka masharti kuhusu namna ya kuamua na kulipa malipo na stahili za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Kupitishwa kwa miswada hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa sheria nchini na kuhakikisha utekelezaji wa sera za maendeleo unafanyika kwa ufanisi zaidi.