SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI: Wasichana waache kulialia, kujificha katika mwamvuli wa uanamke
- Wasichana wanahitaji vitu vikubwa vinne ambavyo ni pesa, elimu, afya nzuri na nafasi ya kufaidika na fursa zinazowazunguka.
- Wadau wanena wasichana waache kulialia na kujificha katika mwamvuli wa uanamke.
- Kujiamini na kutokata tamaa ni silaha muhimu ya kufikia malengo waliyojiwekea.
Dar es Salaam. Wakati maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yakiendelea, wasichana wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kuacha kujificha katika mwamvuli wa uanamke ili wajiendeleze kimaisha.
Wakizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Asasi za kiraia tisa, wadau mbalimbali wamesema wasichana wengi bado wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi lakini wakijitokeza na kusimamia maslahi yao wanaweza wakafaidika na fursa zilizopo kwenye jamii.
Wadau hao ambao wamekusanyika katika viwanja vya Nafasi Arti Mwenge Jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 11, 2018 kutoka mashirika ya Msichana initiative, Global Peace Foundation, Her initiative, Binti salha foundation, SADAKA, Mwanamke na uongozi, Najivunia kuwa binti, Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Victorious Women Empowerment.
Baadhi ya washiriki wamewaasa wasichana kutokukaa nyuma katika kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ili waweze kufanya vizuri katika kujiendeleza kiuchumi na kijamii.
“Dunia ya leo inahitaji watu wachangamfu, na wenye maarifa ya kutosha na sio watu wa kulialia na kujificha katika mwamvuli wa uanamke,” amesema Irene Ishengoma kutoka shirika la Global Peace Foundation.
Amesema kuwa mabinti wana nia, nguvu na uwezo wa kufanya mambo makubwa kama wataamua na kuweka wazi vipaumbele vyao ikiwemo elimu itakayowasaidia kupata maarifa na ujuzi wa maisha.
“Tunafanya makubwa sana kama watoto wa kike bila shuruti kuanzia ngazi ya nyumbani, kumbe tunaweza kufanya makubwa zaidi katika sekta yoyote tutakayoamua kujikita,” amesema.
Baadhi ya wadau walioshiriki mdahalo wa kutambua na kupongeza mafanikio ya mtoto wa kike Tanzania leo Jijini Dar es Salaam. Picha | Veronica Kipingu.
Hata hivyo, mafanikio ya wasichana wengi yanakwamishwa na changamoto ya kutokujiamini na kukatishwa tamaa ya kufanya mambo yanayoleta tija katika kazi zao.
“Siku hii ni muhimu kuonesha yale tunayopitia lakini pia tukiwasheherekea wasichana ambao wamefanya vizuri katika jamii yetu,” amesema Viola Massawe, Meneja Mradi kutoka taasisi ya SADAKA.
Mkurugenzi wa shirika la Najivunia Kuwa Binti, Veronica Kipingu amesema wakati wasichana wakipambana kufikia malengo ya maisha yao, bado wanalazimika kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia unaotokana na vitendo vya ubakaji, mimba za utotoni na kukosa mtu wa usimamizi mzuri kutoka kwa jamii inayowazunguka.
“Tuangalie sababu zinazopelekea upatikanaji wa mimba za utotoni, kwa kuongea nao huko mitaani walipo na changamoto za kimazingira,” amesema Kipingu.
Kipingu ametofautiana na watetezi wa masuala ya jinsia na kuwataka wasichana kutotumia muda mwingi kupiganiA maslahi ya usawa badala yake wajikite kupata mambo manne muhimu ambayo ni pesa, elimu, afya nzuri na nafasi ya kuitumikia jamii, “Tupambane kuhakikisha tunatengeneza uwezo wa kupata vitu hivyo vinne.”
Tanzania inaungana na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike inayofanyika t11 Oktoba 11 kila mwaka ikiwa ni mwitikio wa Azimio la Umoja huo lililopitishwa Desemba 2011.