Shule 10 bora kidato cha sita 2020, Kisimiri kama kawaida
- Shule ya Sekondari ya Kisimiri imeendelea kuongoza orodha hiyo ya dhahabu Tanzania.
- Kati ya shule zilizoingia 10 bora, tatu zinatoka mkoa wa Arusha.
Dar es Salaam. Ni mwaka mwingine wa furaha kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyopo mkoani Arusha baada ya kuongoza kitaifa katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Dk Charles Msonde amewaambia wanahabari leo (Agosti 21 2020) visiwani Zanzibar kuwa Kisimiri iliyokuwa na wanafunzi 53 waliofanya mtihani huo imeongoza kitaifa ikifuatiwa na Kemebos ya mkoani Kagera.
Mwaka jana shule hiyo iliingoza pia kitaifa.
Kisimiri ni miongoni mwa shule nane za Serikali zilizoingia katika 10 bora mwaka 2020, ikiwa ni kiwango kikubwa kuliko hali zilivyo katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi na kidato cha nne.
Zinazohusiana:
- Matokeo ya kidato cha sita 2020 sasa hadharani
- Tunayoyafahamu kuhusu Kisimiri, shule iliyoongoza kitaifa kidato cha sita
Shule nyingine zilizotoboa katika orodha hiyo ya dhahabu kwa mujibu wa Dk Msonde, ni Ahmes ya Pwani katika nafasi ya tatu huku shule kongwe ya Mzumbe ikishika nafasi ya nne.
Shule nyingine katika 10 bora ni Tabora Girls’ katika nafasi ya tano wakifuatiwa na kaka zao Tabora Boys ambazo zote ni shule kongwe nchini zilizopo katika mkoa wa Tabora.
Shule ya Sekondari Kisimiri iliyopo mkoani Arusha imeongoza tena katika mitihani ya kidato cha sita mwaka 2020. Picha|Shule ya Sekondari Kisimiri.
Ilboru ya mkoani Arusha yenyewe imeendelea kubaki katika orodha hiyo ikiwa nafasi ya saba wakati vijana wa Shule ya Sekondari ya Kibaha iliyopo Pwani wakifuatia kwa karibu.
Katika nafasi ya tisa wapo vijana kutoka shule ya kata ya Mwandet wakati wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dareda wakiisaidia shule yao kuingia kwenye 10 bora.
Kati ya shule 10 vinara katika matokeo ya kidato cha sita 2020, tatu zinatoka katika mkoa wa Arusha huku mikoa ya Pwani na Tabora ikiingiza shule mbili kila moja. Mikoa ya Morogoro, Kagera na Manyara kila moja imeingiza shule moja.