Rais Samia: Wanafunzi wapewe ujuzi mpya kukidhi ukuaji wa teknolojia
- Amesema wanafunzi wapatiwe ujuzi unaoendana na mapinduzi ya nne ya viwanda.
- Aagiza shule, vyuo vikuu kutoa masomo yanayohusisha teknolojia mpya.
Dar es Salaam. Rais Samia amewaagiza mawaziri wanaosimamia Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano na ile ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuweka mipango ya kuwapatia ujuzi mpya wanafunzi wa shule za msingi hadi vyuo vikuu unaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema kwa sasa dunia inapita katika wimbi la nne la mapinduzi ya viwanda ambao unahusisha zaidi matumizi ya teknolojia za kisasa katika utendaji na uzalishaji.
Amesema, kutokana na hali hiyo, wanafunzi wa Tanzania wanatakiwa kupata ujuzi unaendana na mabadiliko hayo ili wasiachwe nyuma.
“Napenda kuzikumbusha wizara za Mawasiliano na Teknolojia, Wizara ya Elimu na vyuo vikuu vyote kuwa tupo katika wimbi la nne la mapinduzi ya viwanda.
“Wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu wanahitaji ujuzi mpya. Ujuzi ambao ni tofauti na ule wa wahitimu wa miaka iliyopita kama alivyosema Jaji Mkuu (Profesa Ibrahim Juma) hapa,” amesema Rais Samia.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika kilele cha Wiki ya Sheria nchini Tanzania leo Februari 2, 2022 jijini Dodoma amesema wanafunzi wanatakiwa kutayarishwa kufanya kazi zinazohitaji ujuzi unaolingana na matakwa ya mabadiliko ya teknolojia.
“Mawaziri mpo hapo nadhani mmenote (mmeshaandika) agizo langu,” amesisitiza Rais.
Rais Samia amesema Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mwaka 2019 lilibashiri kuwa maendeleo makubwa katika nyanja ya teknolojia yatahitaji mabadiliko makubwa sana ya masomo yanayofundishwa katika vyuo huku na hivyo lazima Tanzania ikubali mabadiliko hayo.
Zinzaohusiana
- Emanuel Feruz: Mtaalam wa Tehama aliyegeukia ujasirimali wa kupigaji picha
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
Mapinduzi ya nne ya viwanda ni nini?
Kwa mujibu wa Jukwaa la Uchumi Duniani, mapinduzi ya kwanza ya wiwanda yalitumia nguvu za maji na mvuke kutengeneza mitambo huku ya pili yakitumia nguvu za umeme kufanya uzalishaji kwa wingi.
Mapinduzi ya tatu yalitumia teknolojia ya kielektroniki na habari kubinafsisha uzalishaji lakini mapinduzi ya nne ya viwanda ni mapinduzi ya kidijitali ambayo yamekuwa yakitokea tangu katikati ya karne 20.
Mapinduzi hayo yanaangaziwa kuwa ni muunganiko wa teknolojia ambayo inatia ukungu kati ya nyanja za kimwili, dijitali na kibayolojia.
Jukwa hilo linaeleza zaidi kuwa yanahusisha mabilioni ya watu waliounganishwa na vifaa vya rununu, vilivyo na nguvu ya usindikaji isiyo na kifani, uwezo wa kuhifadhi, na ufikiaji wa maarifa.
“Na uwezekano huu utazidishwa na mafanikio ya teknolojia yanayoibuka katika nyanja kama vile akili bandia, maroboti, intaneti, magari yanayojiendesha, uchapishaji wa 3-D, teknolojia ya kibayoteknolojia, sayansi ya nyenzo, uhifadhi wa nishati, na kompyuta ya kiasi,” limeeleza jukwaa hilo.
Mapinduzi ya nne ya viwanda yanatoa fursa pana ya kuinua viwango vya mapato ya kimataifa na kuboresha hali ya maisha ya watu duniani kote.
Latest



