Nusu ya Watanzania hawana nyaraka muhimu za kumiliki ardhi – Ripoti

June 12, 2019 9:12 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ripoti mpya iliyotolewa na NBS inasema asilimia 55 ya Watanzania hawana nyaraka zinazothibitisha kuwa wanamiliki ardhi au makazi.
  • Wataja sababu ni gharama kubwa, mchakato mrefu wa kupata nyaraka hizo. 
  • Wataalamu wa mipango miji wamedai kuwa hali hiyo inawakosesha wananchi fursa nyingi ikiwemo mikopo katika taasisi za fedha.

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya haki na umiliki ardhi imeeleza kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wanaomiliki ardhi na makazi hawana nyaraka muhimu zinazoonyesha umiliki, jambo linalowaweka katika hatari ya kupoteza haki zao na kuendeleza migogoro ya ardhi nchini.

Ripoti hiyo ya utafiti ulioangazia tathmini ya haki na usalama wa ardhi kwa ajili ya makazi (Tanzania Baseline Survey Report on Assessment of Land Rights And Tenure Security 2018) imetolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mei mwaka huu. 

Utafiti huo uliofanyika kati ya Septemba na Novemba 2018, unaeleza kuwa zaidi ya nusu ama asilimia 55 ya wananchi waliohojiwa hawana nyaraka muhimu kuthibitisha haki yao ya kutumia au kumiliki makazi au ardhi wanayoikalia. 

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila Watanzania 10 basi takriban sita hawana nyaraka kuonyesha wanamiliki ardhi au makazi licha ya ukweli kwamba wanaweza kuwa wanamiliki kihalali au wamevamia. 

Nyaraka zinazotambuliwa na Sheria ya Ardhi namba nne ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Kijiji namba tano ya mwaka 1999, ni pamoja na vyeti vya haki ya makazi katika ardhi ya kijiji (CCROs), hati ya ardhi, mikataba ya usajili ya kukodisha, gazeti la Serikali na hati za vikundi. 

Nyingine ni nyaraka za idhini, vibali vya ujenzi, vibali vya  makazi, barua na leseni ya makazi ambapo kwa pamoja nyaraka hizo zimegawanyika katika makundi mawili ya nyaraka rasmi na zisizo rasmi.

Hata hivyo, karibu nusu ya watanzania wanamiliki nyaraka rasmi zinazotambulisha umiliki wa ardhi wanayoikalia. 

“Asilimia 42 ya wananchi waliohojiwa wanamiliki nyaraka rasmi kuthibitisha haki ya kutumia au kumiliki kwa aina yoyote ya ardhi, asilimia 3 ya wahojiwa wana nyaraka zisizo rasmi angalau kwa ardhi moja,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Pia Matokeo ya utafiti huo ambao ulishirikisha sampuli ya watu 4,000 yanaonyesha kuwa wananchi wanaoishi mjini ndiyo wanaoongoza kwa kuwa na nyaraka rasmi za ardhi kwa asilimia 53 ukilinganisha na wale wa vijijini. 


Soma zaidi:


Sababu za Watanzania kutokuwa na nyaraka za ardhi

Utafiti huo ambao pia ulifanyika katika nchi 33 duniani umebainisha kuwa sababu kuu tatu ambazo zimekuwa zikikwamishwa watanzania kuwa na nyaraka muhimu zisizothibitisha umiliki wa ardhi au makazi ni pamoja na gharama kubwa za kupata nyaraka hizo. 

Pia mchakato wa kuziandaa huchukua muda, kupotea kwa nyaraka hizo na migogoro katika familia jambo linalowakatisha tamaa wananchi kuwa na shauku ya kuwanazo. 

Kutokana na sababu hizo ambazo nyingine zinaweza kuwa zina mashiko, ndiyo kumekuwa chanzo cha migogoro isiyoisha ya ardhi na makazi katika jamii na kuleta changamoto ya maendeleo ya rasilimali ardhi Tanzania. 

Karibu nusu ya watanzania wanamiliki nyaraka rasmi zinazotambulisha umiliki wa ardhi wanayoikalia.Picha|Mtandao.

Athari na mikakati ya Serikali  

Mtaalamu wa mipango miji kutoka mkoa wa Singida, Rachel Essau ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kutokuwa na nyaraka muhimu za umiliki wa ardhi kunatoa tafsiri nyingi ambapo mtu anaweza kupoteza ardhi au makazi yake wakati wa upimaji kwa sababu anaweza kuonekana kama ni mvamizi wa eneo husika. 

Amesema hali hiyo pia inachangia mmiliki kukosa utambulisho rasmi katika Serikali ya kijiji au Halmashauri ambao wanahusika na upimaji na uendelezaji miji nchini. 

“Kama barabara itapita sehemu husika (shamba, kiwanja) wakati wa ujenzi mtu hatapata fidia yoyote mana hana kitu cha kumlinda yaani hati,” amesema Essau. 

Amebainisha kuwa watu wengi wanakosa fursa ya kupata fedha na mikopo kutoka taasisi za fedha kwa sababu ya kutokuwa na dhamana, na kuwakwamisha kukamilisha shughuli za maendeleo. 

Hata hivyo, Serikali imeendelea hatua mbalimbali za kuhakikisha ardhi yote inapimwa nchini na watu wanamilikishwa maeneo yao kwa gharama nafuu ili kupunguza migogoro ya ardhi. 

Aprili 18 mwaka huu, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema gharama za urasimishaji makazi haitazidi Sh150,000 badala ya Sh250,000 iliyopangwa awali ili kurahisisha umiliki. 

‘’Tunataka kuwa na database (kanzidata) ya nani anamiliki ardhi kiasi gani na kila mwananchi lazima awe na leseni ya makazi au hati kwa lengo la kushiriki kulipa kodi’,’ alisema Lukuvi.

Enable Notifications OK No thanks