Mikakati itakayowainua wanawake kiuchumi Tanzania

March 5, 2021 9:15 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutolewa kwa pato la msingi la muda mfupi (TBI) kwa mamilioni ya wanawake masikini katika nchi zinazoendelea duniani.
  • Litahakikisha wanaweza kuishi wakati huu mgumu na kupata kipato cha familia.
  • Pato hilo linatakiwa litoke kwenye pato la Taifa (GDP). 

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imeeleza kuwa pato la msingi la muda mfupi (TBI) likitolewa kwa mamilioni ya wanawake katika nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Tanzania linaweza kuzuia kuongezeka kwa umasikini na pengo la usawa wa kijinsia wakati huu wa janga la corona. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya “Kuwalinda wanawake katika kipindi cha majanga”, wanawake wameathirika zaidi na janga la COVID-19  kuliko wanaume kwa sababu wamepoteza mapato.

Pia wameondolewa kwenye soko la ajira kwa kiwango kikubwa na kisha kugeukia kazi za malezi au kutoa huduma.  

Ili kuokoa jahazi la wanawake, ripoti imetoa wito kwa nchi wa kuanzishwa mara moja kwa pato la msingi la muda kwa misingi ya kijinsia kwa ajili ya wanawake masikini na wasiojiweza katika nchi zinazoendelea.

Imesisitiza kuwa hatua hiyo ya dharura ni muhimu ili kuhakikisha wanawake walioathirika kiuchumi na janga hilo wanaweza kumudu maisha wakati huu wa corona. 

“Serikali zinaweza kuchukua hatua sasa hivi kuelekeza asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kila mwezi kwa wanawake wanaokabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii, kwa sababu pato la msingi la kila mwezi litahakikisha wanaweza kuishi wakati huu mgumu,” amesema Mtawala Mkuu wa UNDP Achim Steiner wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Faida za uwekezaji huo hazitowasaidia wanawake tu na familia zao kumudu athari za corona bali zitawawezesha wanawake hao kufanya maamuzi huru kuhusu fedha na chaguo la maisha yao. 

Ripoti hiyo iliyotolewa kuelekea Siku ya Wanawake Duniani itakayoadhimishwa Machi 8, imependekeza mkakati huo kwa wanawake wenye umri wa kufanya kazi kuanzia miaka 15 hadi 64 katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. 


Zinazohusiana:


Imeongeza kuwa kwanza unaweza kutoa usalama na uhakika wa kipato kwa muda mfupi kwa  wanawake milioni 613 wenye umri wa kufanya kazi ambao sasa wanaishi katika umasikini huku wakitengeneza njia ya uwekezaji kwa siku zijazo, na pili utapunguza madhila kwa wanawake hadi bilioni 2 katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa ripoti faida nyingine kubwa ya TBI ni kwamba itapunguza pengo baina ya wanawake na wanaume wanaoishi katika umasikini kwa kuwapa wanawake uhuru wa kiuchumi na kuleta uwiano katika kudhibiti rasilimali ndani ya familia. 

“Pengo la usawa wa kijinsia linaendelea kupitia kutokuwepo uwiano wa kipato na mgawanyo wa kazi, na ingawa TBI sio suluhu ya moja kwa moja, lakini itawasaidia wanawake kuongeza haki ya chaguo wakati huu wa COVID-19,” amesema Raquel Lagunas, Mkurugenzi wa timu wa masuala ya jinsia kwenye shirika la UNDP. 

Ameongeza kuwa TBI inatoa fursa ya utulivu wa kiuchumi kwa wanawake ili waweze kupanga maisha yao kwa ajili ya matakwa yao, mahitaji yao na kushiriki kikamilifu katika jamii zao.

Enable Notifications OK No thanks