Mfumuko wa bei wang'ang'ania kiwango cha Januari

Mwandishi Wetu 0801Hrs   Machi 08, 2019 Biashara
  • Ripoti ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2019 inaeleza kuwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma ilibaki asilimia tatu kama ilivyokuwa Januari.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Februari 2019 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa Januari mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.

Taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Februari 2019 ulikuwa asilimia tatu ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Januari 2019.

“Udumavu wa mfumuko wa bei unaonyesha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei ya bidhaa kwa mwaka ulioishia Februari 2019 umebaki kuwa sawa kabisa kama ilivyokuwa Januari 2019,” inaeleza sehemu hiyo ya ripoti ya mfumuko wa bei ya NBS na kuongeza;

“Hata hivyo, faharisi ya bei ilipanda hadi 114.63 Februari 2019 kutoka 111.33 iliyorekodiwa Februari 2018.

Kiwango cha mfumuko wa bei kama hicho pia kilirekodiwa katika mwaka ulioshia Novemba 2018 na ndiyo kidogo kuliko vyote katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 




Related Post