Mastercard ilivyomuwezesha mkimbizi kusoma chuo kikuu
Raba Hakim amepitia vikwazo vingi mpaka kitimiza ndoto yake. Picha| UNHCR.
- Ni Raba Hakim, msomi mkimbizi kutoka Sudan aliyekulia katika kambi ya wakimbizi nchini Ethiopia.
- Avuka viunzi kufikia ndoto yake ya kusoma chuo kikuu.
- Akihitimu ataitumia elimu yake kuwasaidia wanawake na watoto.
Dar es Salaam. Wakati wakimbizi katika maeneo mbalimbali duniani wakikumbana na changamoto za kupata elimu, wapo baadhi ambao wanaipambania elimu kwa gharama kubwa ili kutimiza ndoto zao.
Raba Hakim, msomi mkimbizi kutoka Sudan aliyekulia katika kambi ya wakimbizi nchini Ethiopia hatimaye ndoto yake ya kujiunga na chuo kikuu imetimia baada ya kuanza masomo ya Saikolojia katika Chuo Kikuu nchini Kenya chini ya ufadhili wa wakfu wa Mastercard.
‘’Nilikotokea wasichana hawapati elimu kama wavulana, kama binti ukienda shuleni akili yako inahama kutoka kwenye masomo kwenda kwenye majukumu ya nyumbani,” anasema Raba ambaye anaanza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani cha Afrika (USIU-Africa) jijini Nairobi.
Binti huyo mwenye miaka 22 amepitia changamoto nyingi mpaka kufikia ndoto hiyo ikiwemo ndugu wa karibu kumzuia kusoma na kulazimisha aolewe.
“Mimi ndiyo nilipata fursa ya kuendelea na darasa la 11, mimi pekee, msichana mmoja tu, na wasichana wengine, wameolewa. Baba yangu alituambia, asingependa msichana yeyote aolewe kabla hajafika Chuo Kikuu,” amesema Raba wakati akitoa ushuhuda wake kupitia Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR)
Kwa mujibu wa UNHCR, asilimia 5 pekee ya wakimbizi duniani ndiyo hupata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kwa wasichana takwimu ni chini zaidi.
Shirika hilo na wadau wake wanashirikiana kuhakikisha wasichana wengi zaidi wanasoma chuo kikuu wakilenga kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2030 kama anavyoeleza Linet Aguko kutoka programu ya ufadhili wa Mastercard.
“Wito wangu ni kwa watu walio tayari kujitokeza na kuwasaidia vijana hawa kwa namna yoyote ili waweze kunufuika na fursa ya kupata elimu ambayo ipo kwa kila mtu,” amesema Aguko katika mahojiano na UNHCR.
Akiwa chuoni, Raba anapata elimu ya saikolojia ambayo anaamini itaenda kusaidia jamii yake hasa wakimbizi ambao wanakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na kutengwa na familia au makazi katika nchi zao.
“Nimechagua kozi hii kwa sababu nafanya kazi na wanawake na wasichana. Nyumbani nchini Ethiopia, nimeshuhudia madhila wanayopitia, na ndiyo maana nimeamua kusoma kozi ya Saikolojia,” amesema binti huyo.
Raba amesema amewaacha wasichana wengi wakiwa darasa la 12 wakitamani kupata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na atafurahi zaidi kama ataona wasichana wengi zaidi wakijiunga na masomo chuo kikuu.
Raba alizaliwa na wazazi wakimbizi nchini Ethiopia. Alianza shule katika kambi ya wakimbizi ya Sherkole ambapo masomo yalikuwa yakifundishwa kwa lugha ya Kiingereza.
Akiwa na umri wa miaka nane, familia yake ilimrudisha nyumbani katika kijiji chao kilichopo katika Mji wa Blue Nile, Sudan. Akiwa huko alianza upya kusoma darasa la kwanza kwa sababu mtaala ulikuwa kwa lugha ya Kiarabu.
Baada ya kijiji chao kushambuliwa na mabomu ya waasi walikimbilia Ethiopia ambako aliendelea na masomo ya sekondari kabla hajapata fursa ya kujiunga na elimu ya juu mwaka huu.
Katika muda wake wa ziada, Raba anafanya kazi ya kujitolea ya ushauri kwa wanawake na wasichana waliopo kambini, programu inayoendeshwa na Kamati ya Kimataifa ya Uokozi (IRC)
Wakati huu akijiandaa na masomo mapya, ameanza mafunzo ya mtandaoni ya kupata uzoefu wa shughuli za chuo huku watu mbalimbali wakijivunia mafanikio aliyopata na kuvishinda vikwazo vya kupata elimu.
“Raba ni mfano wa kuigwa kwa wanawake na wasichana wengine kambini,” anasema Afisa Programu wa IRC katika mji wa Tongo, Mistre Teklesilassie.
Latest



