Malengo: Njia rahisi kuwasaidia wanafunzi kuweka akiba ya fedha
- Ni pamoja na kutengeneza vibubu nyumbani, kufungua akaunti ya benki na kuhifadhi pesa kwa mzazi wako.
- Akiba inaweza kukusaidia katika kufikia malengo yako na pia kuwa msaada katika kipindi cha dharura.
Dar es Salaam. Asubuhi ya leo wakati nikiperuzi katika mitandao ya kijamii, nilikutana na kibonzo kinachosema “Ningelikuwa najua maisha yatakuwa magumu hivi, ningeanza kusevu mapema.”
Kama kawaida, nilicheka lakini baadaye kibonzo hicho kilinifikirisha.
Nilianza kuwaza pesa ambazo nilikuwa nikipewa na wageni waliotutembelea nyumbani, pesa ambazo niliishia kuzimaliza nikiyaharibu meno yangu kwa pipi na lambalamba.
Niliwaza juu ya pesa ambazo baba yangu alinipatia kwa ajili ya matumizi, pesa ambazo ni kweli nilizitumia pasi na kufahamu kuna kesho.
Ni ukweli thabiti kuwa pesa hizo endapo ningezitunza, huenda zingenipatia hata kodi ya kuanzia maisha baada ya kuhitimu masomo yangu ya chuo kikuu, ama zingenisaidia kama mtaji wa kuanzisha biashara. Lakini hazipo. Nilizitumia kweli kweli.
Kwa wanafunzi ambao bado wapo shuleni, bado hawajachelewa kuchukua hatua ya kujiwekea akiba hata kwa kiasi kidogo cha pesa wanachopata.
Ufanye nini ili kuweka akiba kwa ajili ya malengo ya muda mfupi na muda mrefu hasa kama wewe ni kijana:
Fungua akaunti ya mwanafunzi benki
Baadhi ya wazazi na wanafunzi hawaoni umuhimu wa akaunti za benki za kuweka akiba. Na wengi wao hufungua akaunti wakifika chuo kikuu kwa sababu zina umuhimu mkubwa. Utamaduni huu wa kutokuwa akiba ni zao la jamii na masuala kama umaskini.
Baadhi ya benki zinaruhusu wazazi kufungua akaunti kwa ajili ya watoto wao hivyo unaweza kuongea na mzazi wako akakufungulia akaunti hiyo au kufika katika benki ya chaguo lako kwa ajili ya kupata maelekezo sahihi.
Unapoanza kuweka akiba mapema, itakuwa msaada kwako pale unapopatwa na dharura ambayo mzazi huenda asiitatue ndani ya muda muafaka.
Katika kipindi cha uanafunzi, kupata fedha ya mzazi ni kitu cha kawaida lakini zina ukomo.
Unapoanza kuweka akiba mapema, itakuwa msaada kwako pale unapopatwa na dharura ambayo mzazi huenda asiitatue ndani ya muda muafaka. Picha| Access bank.
Njia ya kibubu nyumbani
Vipo vibubu vya kutengenezwa na mafundi seremala na vipo ambavyo ni maalumu vinauzwa madukani. Vingine huja na funguo na teknolojia ya neno siri kwa ajili ya usalama hivyo una uwanda mpana wa kuchagua.
Unaweza kununua mwenyewe au kuongea na mzazi wako akakutafutia kimoja kwa ajili ya kuanza kuweka akiba yako. Inaweza kuwa mpango wa mwaka mmoja, miwili, mitano na kadhalika.
Pia endapo kibubu chako kitajaa, unaweza kuhamishia pesa hizo katika akaunti ya benki au kupata kibubu kikubwa zaidi.
Mashindano ya malengo
Unaweza kukubaliana na rafiki zako kadhaa kuanza mashindano ya kuweka akiba kwa ajili ya malengo ya mbeleni. Mfano endapo una rafiki wa karibu wawili, mnaweza kukubaliana kuweka akiba.
Sio kwa akaunti moja au kibubu kimoja, kila mtu anaweza kuweka fedha zake tofauti tofauti na kisha kuzihesabu kila baada yamuda fulani ili kufahamu kiasi ulichohifadhi.
Hilo halitodumisha tu urafiki wenu bali litawajengea tabia ya kuhifadhi na kuwa na nidhamu ya fedha.
Soma zaidi:
- Binti fanya haya kumsaidia mpenzi wako kutimiza malengo yake
- Namna akiba inavyoweza kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo
- Unayoweza kumfundisha mtoto kutumia vizuri fedha
Hifadhi kwa mzazi wako
Hii inategemeana uhusiano na mzazi wako lakini mara nyingi una uhakika wa kupata pesa yako pale unapompatia mzazi wako akuhifadhie.
Kwa kila pesa ambayo unaipata iwe kwa njia ya mzazi, malipo, zawadi na kadhalika, unaweza kutenga kiasi ambacho unaweza kumpatia mzazi wako akuhifadhie kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Jambo hilo pia huenda likamfanya mzazi wako aanze kuongeza pesa katika akiba yako endapo ataona nia yako njema.
Mtu ambaye anaweka akiba naweza kunufaika kwa mengi ikiwemo kufikia malengo fulani yakiwemo ya kibiashara, kimasomo na kadhalika endapo akiba yake itatosheleza.
Pia kuweka akiba kutakusaidia kutokuhangaika sana pale unapofikiwa na changamoto. Unasubiri nini? Anza leo kuijenga kesho yako.