Majaliwa awashawishi Warusi kuwekeza Tanzania

October 25, 2019 6:50 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanakusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji.
  • Autaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi kuratibu vizuri zoezi la wafanyabiashara kuja nchini.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi kuratibu mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja nchini kuwekeza kwa kuwaunganisha na taasisi na wizara husika ili Taifa lifaidike na uwekezaji huo.

Ametoa agizo hilo baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanaokusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa Tanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

“Tayari miadi imekwishawekwa ya kuwakaribisha wawekezaji wa Urusi kuja Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo,” amesema Majaliwa akiwa nchini Urusi.

Majaliwa alikuwa anahudhuria mkutano baina ya wakuu wa nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika jana (Oktoba 24, 2019) uliolenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi kati ya pande zote mbili.


Zinazohusiana: 


Akizungumza baada kumalizika kwa mkutano huo kwenye ukumbi wa Olympic Park wa jiji la Sochi,Majaliwa  amesema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

“Maeneo hayo ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, Ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo,’” inaeleza taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Tanzania imejinadi vizuri ikingozwa na yeye mwenyewe kwani alifanya mazungumzo na viongozi wa kampuni zaidi ya nane za Urusi ili kuyashawishi yawekeze nchini na yote yalikubali kufika Tanzania mapema iwezekanavyo.

“Viongozi wa makapuni yote niliyopata nafasi ya kuzungumza nao wamesema wako tayari kuja nchini ili waweze kufanya mazungumzo na Serikali pamoja na wafanyabiashara wazalendo ambao wako tayari kuungana na wafanyabiashara hao katika kuwekeza nchini Tanzania,” amesema Majaliwa katika taarifa hiyo. 

Leo Oktoba 25, 2019, Majaliwa ataondoka nchini Urusi kwenda nchi ya Azerbaijan ambako pia atamwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano wa nchi zisizofungamana na upande wowote. Mkutano huo ni wa siku mbili.

Enable Notifications OK No thanks