Magufuli aagiza Selous igawanywe kuwa hifadhi mpya ya Taifa
- Amesema hifadhi hiyo itatumika kwa ajili ya shughuli za utalii.
- Aagiza ipewe jina la Mwalimu Julius Nyerere ili kuenzi mchango wake wa kuanzisha mpango wa kujenga mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuligawanya Pori la Akiba la Selous ili ipatikane hifadhi mpya ya Taifa kwa ajili ya utalii utakaoifaidisha Serikali na wananchi wa eneo hilo kiuchumi.
Selous yenye ukubwa wa kilomita za mraba 54,600 inapatikana Kusini Mashariki mwa Tanzania kwenye Mto Rufiji na kupakana na mikoa ya Morogoro, Pwani na Ruvuma.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Julai 26, 2019) wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kufua umeme kwenye mto Rufiji mkoani Pwani utakaozalisha megawati 2,115, amesema pori hilo likigawanywa litatoa fursa kwa watu kutalii badala ya kutumika kwa shughuli za uwindaji wanyama pekee.
“Kutokana na hii hali, nashukuru Waziri (Dk Hamis Kigwangalla) yuko hapa, nataka hii Game Reserve (Pori la Akiba) ya Selous ikatwe tuibadilishe iwe Hifadhi ya Taifa, ili watalii wawe wanakuja kutalii hapa wanaingia humo badala ya watu kuja kuwinda wanyama wetu,” amesema Rais Magufuli na kuongeza,
Amesema kwenye vitalu vya uwindaji katika nchi zingine duniani hawatumii utaratibu kama wa Tanzania badala yake wanaanzisha ranchi kwa ajili ya shughuli za uwindaji.
“Siyo unachukua eneo la Serikali linakua la kuwinda, nchi zingine hili linatakiwa liwe National Park (hifadhi ya Taifa). Na ikiwa National Park hakuna hunting block (vitalu vya uwindaji). Kwa hiyo watu watakua wanakuja humu wanakuja kutalii, wanaenda Songea, wanaenda Morogoro, wanaenda Pwani, wananchi wa hapa wanafanya biashara,” amesema Rais.
Katika mgawanyo wa eneo hilo, amesema ipatikane hifadhi ambayo inatakiwa iwe kubwa na vitalu vya uwindaji ili kuendelea kufaidika na rasilimali za eneo hilo ambalo liko miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini kutoweka.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Rais Magufuli akosoa ripoti ya mazingira Stiegler’s Gorge.
Amesema mradi wa uzalishaji umeme wa maji utakaojengwa katika mto Rufiji hautaathiri mazingira ya Selous kwa sababu ni asilimia tatu ndiyo itakayotumika.
Amebainisha kuwa bwawa litakalojengwa litatoa faida nyingi na huenda likawa mali ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sababu litatumika na wanyama waliopo kwenye pori la Selous.
“Lile bwawa likishamalizika kupatikana litakuwa bado ni mali ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa hiyo wanyama watakuwa wanakuja kunywa maji kwa wingi, ndege watatengeneza viota vya kutosha.
“Kwa hiyo maji yatakuwa mengi, watu watavua samaki huo ni uchumi wa aina yake nyingine,” amesisitiza Magufuli.
Amesema hifadhi hiyo mpya inaweza kupewa jina la Hayati Mwalimu Julius Nyerere ili kuenzi mchango wake wa kuanzisha mpango wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa Stigler’s Gorge katika mto Rufiji zaidi ya miaka 40 iliyopita.