Kuwa makini: Serikali yatoa kanuni kudhibiti zaidi maudhui mtandaoni Tanzania
- Ni kanuni mpya za mwaka 2020 zinazuia baadhi ya maudhui kuchapishwa mtandaoni ikiwemo uchochezi na uzushi.
- Atakayekiuka anaweza kufungwa mwaka mmoja au faini ya Sh5 milioni.
Dar es Salaam. Ni zaidi ya wiki imepita tangu kanuni mpya ya maudhui mtandaoni zianze kutekelezwa huku zikiweka wazi mambo 10 yaliyozuiliwa kuchapishwa mtandaoni ikiwemo maudhui ya uongo na yanayopotosha umma kuhusu afya na usalama wa nchi.
Kanuni hizo (Postal Communications (Online Content) Regulations, 2020) ambazo zimetungwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta namba 306 zimeanza kutumika Julai 17, 2020 baada ya kusainiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe jijini Dodoma.
Kanuni hizi ni muendelezo wa Serikali kuendelea kudhibiti maudhui ya mtandaoni baada ya zile zilizotolewa mapema 2018 zilizopingwa vikali na baadhi ya wadau wa habari na maudhui ya mtandaoni wakieleza kuwa zinaminya uhuru wa vyombo na uhuru wa kujieleza.
Kanuni hizo ambazo zinapatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zimezuia maudhui yoyote ya uongo yanayolenga kupotosha au kuudanganya umma.
Maudhui mengine ambayo chini ya kanuni hiyo ni kosa kisheria ni yale yanayochochea na kuchagiza picha za uchi, ngono kwa watoto wadogo na biashara ya ngono kwa kutumia picha, vitabu, michoro, michezo.
Pia maudhui yenye hisia za ubakaji, ukahaba, mapenzi ya jinsia moja na uhalifu wa kingono.
Kanuni hizo pia zinakataza kuchapisha au kutangaza habari zinazoingilia faragha ya mtu na utu wa mtu kwa namna yoyote ile au kuchapisha picha au video mtandaoni bila idhini ya wamiliki wa maudhui hayo ikiwa ni moja ya hatua za kulinda hakimiliki za watengeneza maudhui nchini.
“Maudhui dhidi ya Jamhuri na maelekezo kwa umma ikiwemo yanayolenga kuchapisha taarifa, habari, matamko au uvumi kwa lengo kuharibu sifa, hadhi ya Jamhuri ya Muungano, bendera ya Jamhuri ya Muungano, wimbo wa Taifa au alama au logo za Jamhuri ya Muungano,” inasomeka sehemu ya kanuni hizo kuwa aina hiyo ya maudhui yamezuiliwa.
Zinazohusiana:
- LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni.
- TCRA yakusudia kusimamisha leseni za DSTV na Zuku.
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Mtengeneza maudhui ya mtandaoni atakayechapisha habari zenye mwelekeo wa vitendo vya uharifu na biashara haramu hasa ujambazi, unyang’anyi, matumizi ya dawa za kulevya, mauaji, ubakaji, kughushi, utakatishaji fedha naye anajiweka katika wakati mgumu chini ya kanuni hii.
Tofauti na awali, kanuni hizo zimeongeza vipengele viwili zaidi vya leseni ambavyo ni vya burudani na elimu. Wamiliki wa leseni za maudhui ya burudani na elimu wanatakiwa kulipia Sh500,000 kwa mwaka ili kupata leseni zao huku viwango vya malipo kwa leseni ya kuchapisha habari mtandaoni ikimebaki kama ilivyokuwa katika kanuni za mwaka 2018.
Gharama za kuomba leseni katika uzalishaji wa habari zote na maudhui hayo ya burudani na elimu zimebaki kuwa Sh100,000.
Kanuni hizo pia zinazuia maudhui yanayochagiza watu kuandamana yanayoweza kuharatisha usalama wa nchi na sarafi zake.
Mtu yoyote atakayekiuka kanuni hiyo anaweza kuhukumiwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja au kulipa faini isiyopungua Sh5 milioni au vyote kwa pamoja.
Licha ya kuwa umuhimu wa kanuni hiyo kuwalinda watengenezaji na watumiaji wa mtandao, baadhi ya wadau wa habari za mtandaoni wamewataka Watanzania kuwa makini hasa wanapotumia mtandao kwa sababu baadhi ya vifungu vya kanuni hiyo vinaweza kuwatia hatiani.
Mwanzilishi wa mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo katika ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa kuna umuhimu wa watu kuelimishwa kuhusu kanuni hiyo na pale ambapo inaminya uhuru wa kujieleza ni vema mamlaka zikabadilisha baadhi ya vipengelea.
MABADILIKO YA SHERIA: Kanuni za Maudhui Mtandaoni (2020)
Zingatia: Maudhui ya namna hii (b – f) yanaweza kusababisha maisha yako kuwa magumu. Tafuta namna ya kujiepusha nayo!
Mimi nafanya kukutahadharisha tu… pic.twitter.com/HBjAEFUyMP
— Maxence M. Melo (@macdemelo) July 30, 2020