Kizwalo Simbila: Kijana aliyefungua fursa kwa vijana kupitia mtandao

August 7, 2019 4:05 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfumo huo uliojikita katika masuala ya elimu na uchumi unakutanisha vijana ili kusaidiana kupata fursa mbalimbali.
  • Tayari vijana 20 wameshafanikiwa kuanzisha biashara zao kutokana na jukwaa hilo changa.

Dar es Salaam. Ni ukweli usiopingika kuwa vijana wengi hupata wakati mgumu katika kutafuta shughuli mbalimbali za kufanya pindi wanapomaliza shule au hata wakiwa katika mazingira ya shule.

Hali hiyo huwapelekea vijana wengi kufanya shughuli ndogo ndogo za kuwaingizia kipato.

Hata hivyo, kuna baadhi ya vijana walioamua kutatua tatizo hilo kwa kuwapatia fursa vijana wenzao akiwemo Kizwalo Simbila (27). Kijana huyo ni mjasiriamali na mwanzilishi wa mtandao wa Schoolbiz unaowakutanisha vijana mbalimbali katika kujadili fursa za kibiashara na kiuchumi zitakazowasaidia katika kuwakuzia kipato.

Mtandao huo unahusisha wanafunzi na vijana wanaotafuta fursa zitakazowasaidia kimaisha na kuwakuzia kipato kwa namna tofauti tofauti, bila kuzingatia historia ya kijana husika.

Schoolbiz unafanya kazi kwa njia ya mtandao ambapo humuhitaji mwanafunzi kuingia katika kiunganishi (link) kitakachomsaidia kukutana na vijana wenzake waliojiunga kwa muda huo na kupata nafasi ya kujadili mambo mbalimbali yatakayowasaidia katika soko la ajira na maisha kwa ujumla.

“Nilianzisha mfumo huu baada ya kuona na kuamini uwezo mkubwa walionao vijana katika kufanya shughuli zinazoweza kukuza uchumi wa nchi kwa kujadiliana na kujifunza fursa zilizopo nchini,” amesema Kizwalo.

Mfumo huo umejikita zaidi katika masuala ya kielimu na kiuchumi ili kukuza ufahamu na uwezo walionao vijana katika kutatua changamoto zinazowakabili kwenye nyanja mbalimbali ili kuleta maendeleo.

Hata hivyo, mfumo huu haujaweza kuwafikia vijana wote kwa kuwa ni dhahiri kuwa sio vijana wote wamefikiwa na simu janja na intaneti nchini jambo litakalomfanya kijana huyo kubuni mbinu za ziada kuwafikia waliopo nje ya huduma hizo.

“Bado sijawaza kuanzisha mijadala nje ya mtandao kwani niliamini kwa ulimwengu tuliopo sasa ni ulimwengu wa kidigitali na vijana wengi wamejikita katika shughuli za kimtandao japo nina waza kuweka mfumo mbadala nje ya ule uliopo,” ameeleza.

Takriban vijana 50 kwa muda wa mwaka mmoja  tangu kuanzishwa kwake wamekua watumiaji wa mara kwa mara katika mtandao huo, na kusaidia zaidi ya vijana 20 katika kuanzisha biashara zinazowaingizia kipato. 

Licha ya kuwa tayari vijana 20 wameshaanzisha biashara, Kizwalo atakuwa na kazi ya kuvutia vijana wengi zaidi kutumia jukwaa lake ili kupata manufaa zaidi.

Kwa sasa mfumo huo hufanya kazi kwa njia ya kiunganishi bila ya gharama zozote atakazotakiwa kugharamikia kijana ili apate huduma hio. Jukwaa hilo la Schoolbiz linafanya kazi kama mtandao maarufu wa JamiiForums lakini umeegemea zaidi kwa ajili ya fursa kwa vijana pekee. 

Katika jukwaa hilo, mtu huchapisha jambo linalohusu fursa na wengine huchangia kubainisha zaidi kuhusu jambo hilo ama kuongeza fursa nyingine zinazohusiana. 

“Mfumo huo umenipa (credit) sana kwenye baadhi ya “presentations” ambazo nimeshafanya na imekua na manufaa makubwa sana kwa vijana na umewasaidia  kujua ni kwa namna gani wanatakiwa kuhangaika ili kukuza kipato chao,” amesema.

Enable Notifications OK No thanks