Kamwelwe: Serikali haijasitisha ujenzi wa bandari ya Bagamoyo

May 13, 2019 3:04 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Ujenzi wa mradi huo umekuwa ukipigwa kalenda mwaka hadi mwaka kutokana na kuendelea kwa majadiliano na wawekezaji. Picha|Mtandao.


  • Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema mradi huo haujasitishwa bali majadiliano yanaendelea na wawekezaji.
  • Amesema ni kweli majadiliano yamechelewa kutokana na kuwepo masharti ambayo hayana manufaa kwa upande wa Tanzania.

Dar es Salaam. Baada ya kuwepo mjadala mzito bungeni juu ya hatma ya Bandari ya Bagamoyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema mradi huo haujasitishwa na majadiliano yanaendelea na wawekezaji baada ya “kuwepo masharti yasiyokuwa na maslahi kwa Taifa”.

Akijibu hoja za wabunge wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake, Kamwelwe amesema hadi sasa Serikali inaendelea na mazungumzo na wawekezaji wa mradi huo unaotarajia kugharimu Dola za Marekani bilioni 10 sawa na Sh22.3 trilioni.

“Kuna baadhi ya wabunge walisema Serikali imekataa kuendelea na mradi sina taarifa hiyo…majadiliano yanaendelea ila ni kweli yamechelewa kutokana na kuwepo masharti ambayo hayana manufaa kwa upande wa Tanzania,” amesema waziri huyo bila kuanisha masharti hayo.

“Pale itakapofikia ukomo wa majadiliano, Serikali itatoa taarifa kwa Bunge ili na wabunge nao watoe mchango wao,” ameongeza wakati akiomba wabunge wapitishe bajeti ya wizara hiyo ya takriban Sh5 trilioni.


Soma zaidi: Bunge lahoji kutojenga bandari ya Bagamoyo


Ujenzi wa mradi huo umekuwa ukipigwa kalenda mwaka hadi mwaka kutokana na kuendelea kwa majadiliano na wawekezaji.

Mwishoni mwaka 2017 Serikali ilieeleza kuwa ujenzi wa mradi huenda ungeanza Januari 2018 na kukamilika 2022 lakini hadi sasa bado haujaanza.

Enable Notifications OK No thanks