Kadi ya mpiga kura haitatumika uchaguzi Serikali za mitaa-Nec

October 10, 2019 10:26 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2019/2020 linaloendelea nchini halihusiani na uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
  • Nec imesema mwananchi asipojiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za mitaa hataweza kupiga kura.
  • Zoezi la kujiandikisha linafanyika kati ya Oktoba 8-14 kabla ya uchaguzi utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema kitambulisho cha mpiga kura kinachotolewa na tume hiyo hakitatumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu, badala yake wananchi wanatakiwa kujiandikisha ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi wao.

Imesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2019/2020 linaloendelea nchini halihusiani na uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mkurugenzi wa Nec, Dk  Wilson Mahera aliyekuwa akizungumza leo (Oktoba 10, 2019) Jijini Dar es Salaam , amesema kuwa uandikishaji unaoendelea ulioanza Oktoba 8, 2019 unahusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa hausimamiwi na Nec na wananchi wanapaswa kufuata utaratibu uliowekwa.

 “Uandikishaji huo (wa Tamisemi) ni tofauti na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaofanywa na Tume kwenye mikoa mbalimbali nchini. Uboreshaji huu unahusu uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani wa Tanzania Bara utakaofanyika mwakani 2020.

“Mwananchi asipojiandikisha hataweza kupiga kura katika uchaguzi huo,” amesema Dk Mahera.

Zaidi, Dk mahera ameongeza kuwa mwananchi ambaye hatajiandikisha kwenye uandikishaji unaofanywa na Tamisemi hatapata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa hata kama atakuwa na Kadi ya Mpiga Kura kwa sababu uchaguzi hausimamiwi na Nec.


Soma zaidi: 


Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo la kujiandikisha ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi wa mitaa yao siku hiyo ya Novemba 24, 2019.

Aidha, Mahera amesema Tume kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ina jukumu la kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea kwa sasa katika mikoa ya Tabora, Katavi na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambako uboreshaji utafanyika kuanzia Oktoba 14 hadi 20 mwaka huu.

Ameongeza kwamba zoezi hilo litaendelea kwenye mikoa ya Songwe, Dodoma na Singida kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 1, 2019.

“Wanaostahili kujiandikisha ni wale ambao wana miaka 18 na wale ambao watafikisha miaka 18 mwakani (2020) kabla ya uchaguzi, lakini pia zoezi linawahusu wale ambao kadi zao zimeharibika au zimepotea ili wapate fursa tena ya kuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” amesema Dk Mahera.

Enable Notifications OK No thanks