Kabila la Bodi: Wanaume wanavyoshindana kupata unene
- Kabila hili linapatikana Kusini mwa nchi ya Ethiopia katika bonde la mto Omo.
- Wanaume wa kabila ambao hawajaoa hushindana kuongezeka mwili ndani ya miezi sita.
- Katika kipindi hicho, wanakunywa kinywaji maalumu huku wakiwa hawana ruhusa ya kutembea kwenda kokote na kujamiiana.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa mtandao wa WhatsApp na Instagram, huenda umekutana na picha inayomuonyesha mwanaume mnene ambaye anashiriki shindano kuongezeka mwili yaani unene.
Picha hiyo imeambatana na maneno kwa lugha ya Kiingereza yanayosema, “In the Odi tribe in Ethiopia, the most desired men are those with the largest bellies. The more belly you have, the more attractive you are. I show you so you can see that you are not fat, you’re just in the wrong tribe.”
Maneno hayo kwa Kiswahili yanamaanisha “katika kabila la Odi nchini Ethiopia, Wanaume wanaopendwa zaidi ni wale walio na matumbo makubwa. Unavyokuwa na tumbo kubwa, ndivyo unavyokuwa na mvuto zaidi. Ninakuonyesha hilo ili ufahamu kuwa wewe siyo mnene bali upo katika kabila ambalo siyo sahihi.”
Hata hivyo, huenda unahaitaji kujua mbali zaidi ya kuwa na tumbo kubwa ni nini sababu za wanaume wa kabila hilo kutaka maumbile hayo na wanayapataje?
Hiki ndicho tunachokifahamu kuhusu kabila hilo
Kabila hilo lina majina kadhaa wengine huliita kabila la Bodi na wengine huiita Odi. Makazi yake ni katika bonde la mto Omo uliopo kusini mwa nchi ya Ethiopia.
Tofauti na maelezo ya picha inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, wanaume wa kabila hilo hawashindani kuwa na matumbo makubwa bali wanashindana kupata mwili mkubwa likiwemo na tumbo.
Kwa muhibu wa Mpiga picha Eric Lafforgue wa shirika lahabari la Daily Mail, aliyewahi kutembelea kabila hilo na kuishi nao kwa muda, mashindano hayo huchukua miezi sita kufikia kilele chake kinachojulikana kama Ka’el.
Wanaume wa kabila hilo hukutana na kuongozana kufika katika mti maalum wakionyesha ni kwa kiasi gani wameweza kunenepa ndani ya miezi sita.
Mwanaume ambaye ni mnene zaidi, huvikwa taji la ushindi na hutambulika kama shujaa kwa maisha yake yote. Picha| Daily Mail.
Safari kuelekea kilele cha Ka’el
Safari ya miezi sita huanza kwa familia kumchagua mwanaume ambaye hajaoa ili kuingia katika kinyang’anyiro cha taji la mwanaume mnene zaidi wa mwaka.
Baada ya kuchaguliwa, mwanaume huyo hulazimika kuishi nyumbani kwake kwa miezi sita akiwa hana ruhusa ya kutembea kwenda kokote wala kujamiiana ndani ya kipindi chote.
Chakula anachokula mwanaume huyu ni mchanganyiko wa damu na maziwa ya ng’ombe ambapo anatakiwa kunywa mchanganyiko wa lita mbili kwa siku na kikombe cha kwanza hunyweka asubuhi wakati jua linachomoza na analazimika kuinywa haraka ili isigande.
Lafforgue anaeleza kuwa, wanawake huwa kiungo muhimu katika mashindano haya kwani ndio hupeleka chakula kwa washindani hawa na bado huwahangaikia washindani hawa hadi siku ya kilele cha mashindano.
Soma zaidi:
- Kiswahili kinavyotumika kukuza utalii Marekani
- Yatakayosaidia kupunguza vifo vya wanyamapori Tanzania
- Tanzania yaweka tozo mpya kwa watalii 2020-21
Siku ya kilele inakuaje?
Katika siku hii, wanaume hupakwa mchanganyiko wa udongo mweupe na majivu na kisha huvalia shanga zenye rangi mbalimbali. Baadaye hukutana na kuandamana kuelekea katika mti mtakatifu na kuuzunguka huku shughuli zingine kama ngoma na kucheza zikiendelea.
Kutembea siku hiyo hugeuka mtihani kwa baadhi yao kwani tumbo huwa kubwa kiasi cha kulazimika kutembea na mti ili kujipatia msaada.
Wanawake huwasaidia wanaume hao kwa kuwafuta jasho, kuwapatia maji na pombe ili waweze kufikia adhimio la mashindano yao huku kila msichana akiwa makini kuona yupi anafaa kuwa mumewe.
Wavulana wadogo nao huitumia siku hiyo kuwatazama kwa makini ili siku yao ikiwadia wanenepe, wafanane na wakubwa wao waliowatangulia.
Hata baada ya mshindi kujulikana, ngo’mbe huchinjwa na wazee wa kabila hufanya utabiri kwa kuangalia damu ya ng’ombe huyo na kisha maisha hurudi katika hali ya kawaida ambapo wale wote waliokuwa wamenenepa hurejea katika miili yao ndani ya wiki mbili tu.
Hivyo kwa kuwa na mwili mkubwa katika kabila hili, ni sifa mojawapo ya kukuongezea mvuto kwa mabinti wa kabila la Bodi na endapo mwili wako ukiwazidi wote, basi wewe ni shujaa wa maisha.
Katika kabila lako mwili mkubwa unaashiria nini? Unajivunia kua na mwili mkubwa? Vipi kuhusu athari za kuwa mnene kupitiliza? Haya ni mambo ya msingi unayotakiwa kuyafikiria na kukutumia majibu kupitia namba yetu ya WhatsApp ya +255 677 088 088.