Jiandae kufanya utalii Hifadhi mpya ya Taifa ya Chato
- Rais Magufuli ameridhia mapendekezo ya kuanzisha Hifadhi mpya ya Taifa ya Chato.
- Uwanja wa Ndege wa Chato unatarajiwa kuchangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa utalii katika hifadhi hiyo.
- Hifadhi hiyo ni matokeo ya kupandishwa hadhi mapori matano ya akiba katika eneo hilo la Kanda ya Ziwa.
Dar es Salaam. Tanzania sasa inatarajiwa kuwa na hifadhi za taifa 17 baada ya Rais John Magufuli kuridhia mapendekezo ya kuanzisha hifadhi mpya ya Chato.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla alieleza wakati akifungua Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi hivi karibuni kuwa hifadhi hiyo itakayojulikana kama Chato National Park imeundwa baada ya Rais kuridhia kupandisha hadhi mapori matano ya akiba kuunda hifadhi ya Taifa.
Dk Kigwangalla anasema kuwa Serikali ya awamu ya tano imefanya jitihada za kuhakikisha watalii wanaongezeka zaidi. Miongoni mwa jitihada hizo ni kulifufua na kuboresha Shirika la Ndege ( ATCL) na ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR).
“Napenda kumshukuru sana Mhe. Rais, Dk John Pombe Magufuli kwa kuridhia mapendekezo yetu ya kupandisha hadhi mapori matano ya akiba kuwa Hifadhi ya Taifa ambayo itaitwa Chato National Park, ‘Tunatake pia advantage’ ya uwepo wa uwanja wa ndege wa Chato ambao unajengwa katika kiwango cha kutua ndege kubwa zitakazowawezesha watalii kufika katika hifadhi hiyo,” alinukuliwa Dk Kigwangalla katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara hiyo.
Tangu mwaka 2014 Tanzania imekuwa na hifadhi za Taifa 16 zenye ukubwa wa kilomita za mraba 57,024 zinazosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) yenye makao yake makuu jijini Arusha. Zaidi ya theluthi au asilimia 35.6 ya eneo lote la hifadhi za Taifa nchini ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Ili kuendeleza kukuza utalii nchini, Dk Kigwangalla ameomba ushirikiano miongoni mwa wadau wote wa sekta hiyo zikiwemo taasisi za serikali, jamii na sekta binafsi.
Dk Kigwangalla anasema ushirikiano huo utasaidia kuongeza mapato kwa kuwa kwa sasa kinachopatikana ni kidogo ukilinganisha na aina na idadi ya vivutio vilivyopo hapa nchini.
Mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa umezidi kupaa mwaka hadi mwaka ambapo kwa sasa inachangia takriban asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 24 ya mapato yote ya fedha za kigeni.
Pia, sekta hiyo inachangia zaidi ya asilimia 10 ya ajira zote nchini ambapo ajira za moja kwa moja ni 500,000 na ajira takribani millioni moja zisizo za moja kwa moja.
Waziri Kigwangalla akiangalia moja ya gari la kitalii la wazi katika maonesho hayo. Picha|Wizara ya Maliasili na utalii.
Maonyesho hayo ya kimataifa ya utalii ya mwaka 2018 yameshirikisha kampuni na wadau wa utalii zaidi ya 350 kutoka nchi zaidi ya 12 duniani na kuvutia watu zaidi ya 4,000.
Dk Kigwangalla amesema maonyesho hayo ni muhimu katika sekta hiyo na yanasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaoingia Tanzania.
‘’Serikali ya awamu ya tano imefanya jitihada za kuhakikisha watalii wanaongezeka zaidi. Kwa sasa Rais ameridhia mapendekezo ya kupandisha hadhi mapori matano ya kiba kuwa hifadhi ya Taifa itakayo julikana kama Chato National Park sambamba na kulifufua na kuboresha shirika la ndege la ATCL na ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge,” anasema Dk Kigwangwalla.
.