Ilemela yapitisha bajeti ya 2022-23, ikibuni vyanzo vipya vya mapato

January 28, 2022 11:18 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Halmashauri hiyo imepitisha bajeti  ya Sh77.1 bilioni kwa mwaka 2022/23.
  • Yabunifu vyanzo vipya ikiwemo machinjio ya ngurume kutunisha bajeti.
  • Watendaji watakiwa kuongeza uwazi, uwajibikaji katika matumizi. 

Mwanza. Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imeanza kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwa ni pamoja na ujenzi wa machinjio ya nguruwe utakaosaidia katika kukusanya mapato na kufikia lengo la bajeti ya mwaka 2022/23.

Halmashauri hiyo imepitisha mpango wa bajeti kwa mwaka 2022/23 wa kukusanya Sh77.1 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh3 bilioni ya bajeti ya mwaka 2021/22  ambapo halmashauri ilipitisha kukusanya zaidi ya Sh74 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh 19.1 bilioni sawa na asilimia 24.7 ya bajeti yote ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kiasi kilichobaki kitatumika kulipa mishahara.

Katika mgawanyo wa bajeti hiyo iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Sh1.7 bilioni itakuwa ni ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka Serikali Kuu, na Sh13.5 bilioni ni mapato ya ndani.

Hata hivyo, ili kufikia lengo la makusanyo ya halmashauri hiyo imelazimika kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwemo kujenga machinjio ya nguruwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Manispaa ya Ilemela, Modest Apolinary  akizungumza kwenye kikao cha kupitisha mpango huo leo Januari 28, 2022 amesema vyanzo vingine vipya vya mapato ni pamoja na ujenzi wa kituo cha biashara (Buzuruga Commercial Center) kitakachojengwa eneo la Buzuruga na kuimarisha miundombinu ya Barabara eneo la mradi wa viwanda Nyamhongolo (Nyamhongolo industrial park).

“Pamoja na kuanzisha vyanzo hivyo pia Halmashauri itaongeza nguvu katika ufuatiliaji wa mapato na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza ili kubaini mianya inayovujisha mapato,” amesema Apolinary.

Mkurugenzi huyo amesema, halmashauri imejipanga kuimarisha mradi wa mashine za ufyatuaji tofali ili uweze kuzalisha tofali kwa tija sambamba na kuanza kutumia sheria ndogo za halmashauri za mapato ya ndani ili kufanya marekebisho ya viwango vya ushuru na kodi ya taka ya asilimia 30.

Pia Halmashauri itaanza kuchukua hatua za kisheria kwa wanaoshindwa kulipa ada na tozo mbalimbali za halmashauri.


Zinazohusiana:


Kupitia mpango huo wa bajeti, Mkurugenzi aliomba kiasi cha Sh30.1 bilioni kwa ajili ya kujenga kituo kipya cha afya katika eneo la Kabusungu kitakachogharimu Sh16 bilioni, Sh14 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha biashara huku Sh10 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara eneo la mradi wa Nyamahongolo.

Wakizungumza baada ya bajeti hiyo kusomwa baadhi ya madiwani wameunga mkono bajeti hiyo huku wakiomba suala la kuanzisha vyanzo vipya vya mapato lipewe kipaumbele kwenye maeneo yao.

“Hapa tumeshuhudia vyanzo vitakavyoanzishwa na halmashauri katika kukusanya mapato, lakini kwenye kata zetu vipo vyanzo vingi vya mapato vinapaswa kuibuliwa,” amesema Maganiko Ngaka, diwani kata ya Nyamanoro.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amesema atashirikiana na madiwani kuhakikisha bajeti hiyo inafikiwa na kuwataka madiwani kuwa makini na kufuatilia miradi ya Maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Amesema kumekuwepo na mianya ya upotevu wa fedha na zingine kutumika ndivyo sivyo na kwamba suala hilo atalisimamia ili kuhakikisha kila fedha inayotolewa kwa ajili ya Maendeleo inafanya kazi.

Enable Notifications OK No thanks