Ijue filamu itakayokufundisha umuhimu wa maadili katika kuzipata ndoto zako

August 14, 2020 9:29 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inamhusu binti ambaye analazimika kujifunza maadili kwa njia ngumu.
  • April ambaye ni Ballerina mwenye ufundi wake, anajikuta katika njia mpya baada ya mipango yake kuharibika.
  • Unadhani inachukua kipaji pekee kufanikiwa? Tazama filamu hii kupata mwelekeo mpya.

Dar es Salaam. Mwanadada mahiri kwa kudansi Ballet (aina ya dansi inayopima umahiri katika usahihi, na wepesi wa mtu anayecheza dansi hiyo) anajikuta kwenye sintofahamu baada ya ndoto yake ya kutumbuiza kwa kuonyesha umahiri wake mbele ya maelfu kuingia dosari.

Haikutokea hivi hivi. Dosari hiyo ilitokea  baada ya kumtelekeza mwanamke aliyeshikilia nafasi ya juu kwenye njia ya kufika katika ndoto yake kwenye mvua wakati akiwahi udahili wa mashindano hayo. Lakini Loh! Anastaajabu baada ya kumkuta mwanamke huyo kuwa ndiyo mwamuzi mkuu wa udahili huo. Kwa kifupi ni kuwa, “alikata tawi alilokalia”.

Baada ya mipango yake kuharibika, April alilazimika kurudi nyumbani ambapo aliamua kufundisha watoto kucheza kama yeye. Picha| Pinterest.

Licha ya kuwa binti huyo alikuwa na kila kitu cha kumfikisha kwenye ndoto zake, yaani jitihada, nguvu, bidii na kila kitu, alikosa maadili na nidhamu na hapo ndipo njiapanda ilipoanzia.

“Huwezi kunidanganya, rudi nyumbani,” ni ujumbe wa Frank ambaye ni baba mzazi wa April akimwambia mwanaye kurudi nyumbani baada ya video yake ya udhalilishaji kusambaa mtandaoni.

Akiwa nyumbani, April binti ambaye jina lake utalisikia sana utazamapo filamu ya “Feel the Beat” anarudi nyumbani baada ya mipango yake kuparanganyika,na anaishia kuvaa jukumu la kuwafundisha watoto jinsi ya kuwa wachezaji kama yeye.


Zinazohusiana


Hata hivyo, wakati akifanya hayo, analazimika kuishi maisha ya uongo kwani jamii inamfahamu kama mwanadada aliyefanikiwa kumbe hata senti ya mafanikio hajaionja.

Vipi, siri itafichuka? Watoto wataweza kufikia viwango vyake? 

Jibu maswali hayo kwa kuitazama filamu hiyo kupitia mtandao wa Netflix. Kama bado, unaweza kuangazia burudani nyingine kupitia ving’amuzi na njia ya mtandao.

Enable Notifications OK No thanks