Ifahamu nje, ndani simu ya OnePlus 8

July 8, 2020 11:54 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni simu iliyozinduliwa miezi ya hivi karibuni. 
  • Uwezo wa uhifadhi wake ni mzuri lakini huenda isiwafurahishe wanaopenda kutumia memori kadi.
  • Ni simu inayohitaji kutunzwa kama yai, mdondoko mmoja, utapasua kioo cha mbele au cha nyuma.

Dar es Salaam. Hakuna asiyependa kutumia simu nzuri na inayomtosheleza mahitaji yake. 

Mbali na uwezo wa kuwasiliana na ndugu pamoja na jamaa, kuwa na simu janja ni kujisogezea teknolojia lukuki zikiwemo kamera, redio, tochi na programu mbalimbali muhimu katika kutimiza majukumu mbalimbali ya kazi na biashara.

Hata hivyo, kutokana na wingi wa bidhaa hizo sokoni, imekuwa ni ngumu kufanya uchaguzi pale unapohitaji kununua kwa kuwa njiapanda ya ni aina gani ya simu itakufaa. Leo, jifunze kuhusu toleo jipya la simu ya OnePlus 8 kabla ya kwenda kuinunua iwapo itakuwa imekuvutia.

Simu hiyo, iliyozinduliwa Aprili, 2020,  inatumia mfumo endeshi wa kizazi cha 10 cha Android 10 na OxygenOS 10 na ni kati ya simu chache zisizokuwa na sehemu ya kuwekea kadi ya ziada ya kuongezea nafasi (memory card). Mifumo endeshi hii ina ufanisi mkubwa kuliko matoleo ya awali.

Hali hiyo huenda isiwe chaguo la watengeneza maudhui wengi wasioridhika na nafasi inayokuja na simu. OnePlus 8 imetengenezwa na uwezo wa kati ya gigabaiti (GB) GB128 na 256GB za uhifadhi wa ndani na kati ya GB8 na GB12 za hifadhi ndani ya RAM.

Wembamba wa inchi 0.31 na uzito wa gramu 180 ukifaa mtu yeyote anayependa simu zisizokuwa mzigo. Picha| Rodgers George.

Kwa wapenda picha, simu hii ina kamera tatu nyuma na moja mbele.

Kamera za nyuma, zina uwezo wa kupiga picha za mapana kwa megapikseli (MP) 48, mapana zaidi kwa MP 16 na kamera ya kupiga picha vitu vidogo kwa ukaribu (macro photography) kwa MP 2.

Kwa kamera ya mbele, OnePlus 8 ina kamera yenye MP 16 ambayo ina uwezo wa kupiga picha huku ikiweka usawia wa rangi, vivuli na mwanga kwenye picha ama kwa kifupi unaweza kuiita ‘HDR automatic’.

Kitakachokufanya uipende zaidi simu hii, ni kioo chake ambacho kina teknolojia ya “Fluid AMOLED” na ukubwa wa inchi 6.55 kikikuwezesha kuona video kwa mng’ao wa tofauti. 

Unapenda kuangalia filamu kupitia simu? Baadhi ya wachambuzi wanaona simu hii itakuwa rafiki kwa watazama filamu kutokana na ukubwa wake.

Ukubwa wake wa inchi 6.31 (urefu) na inchi 2.87 (upana) unaipatia simu hii muonekano mzuri huku wembamba wa inchi 0.31 na uzito wa gramu 180 ukifaa mtu yeyote anayependa simu zisizokuwa mzigo.


Zinazohusiana


Nyeusi kuhusu simu hii

Hata hivyo, simu hiyo haina sehemu ya kuchomekea “earphones” zilizozoeleka ambazo zina pini ya milimita 3.5 (AUX) na haiji na kifaa hicho kwenye boksi lake.

Unapoinunua, tarajia kuwa na pesa nyingine ya kununua kifaa hicho chenye kichomekeo cha “type C” mbali na Sh1.62 milioni ambayo ni bei yake ya kiwandani nje ya kodi.

Kama huwezi kuagizia, kwa Tanzania baadhi ya watoa huduma kama @techovers anaeiuza kwa Sh2.5 milioni, wanaweza kufanikisha upatikanaji wake. 

Hata hivyo, sauti yake siyo haba kwani ina spika mbili licha ya kuwa simu hiyo haijaambatana na teknolojia ya redio. Kama ukirudi kijijini kuhesabiwa, itabidi ukubaliane na kukosa habari endapo hautokuwa na mtandao.

Pia, simu hiyo imeundwa na fremu ya aluminiamu huku ikiwa na kioo mbele na nyuma.

Enable Notifications OK No thanks