Huu ndiyo mwisho wa tembo, simba duniani?

July 15, 2020 5:55 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Imetabiriwa kuwa ndani ya miaka 10, wanyama hao wenye sifa za kipekee watakuwa wametoweka duniani endapo hatua stahiki hazitochukuliwa.
  • Zaidi ya asilimia 90 ya wanyama hao wameshatoweka duniani huku waliosalia wakiendelea kuwindwa na majangiri.
  • Wadau washauri kuondolewa kwa mitego na kuimarisha ulinzi mbugani kwa kuongeza idadi ya askari wa mbugani.

Dar es Salaam. Bila shaka huwa unastaajabu kila umuonapo simba na masikio yako husisimka pale usikiao muungurumo wake unapokuwa mbugani.

Macho yako pia hustaajabu kumuona tembo ambaye ni mnyama mkubwa zaidi anayetembea ardhi ya dunia huku faru na mtindo wa maisha yake akikuacha na maswali.

Itakuwaje pale watatu hao wote wakitoweka ndani ya miaka 10 kama ilivyoainishwa na Taasisi ya Kuokoa Hifadhi za Taifa iliyosajiliwa nchini Uingereza na tawi lake nchini Zimbabwe?

Taasisi hiyo inayojihusisha na kushughulikia usalama wa wanyamapori na utunzwaji wa hifadhi za barani Afrika pamoja na kuwajengea mafunzo wanajenshi wa mbugani ili kulinda wanyamapori na kupambana na ujangiri.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, hadi sasa, asilimia 97 ya simba wote duniani wametoweka. Taasisi ya Kuokoa Hifadhi za Taifa imesema simba 975,000 wameuliwa ndani ya miaka 100.

Inasikitisha kuwa hadi sasa ni simba dume 350,000 tu wamebaki huku zaidi ya simba 600,000 wakiuliwa kila mwaka.

Kwa upande wa vifaru, shirika hilo limesema asilimia 94 ya wanyama hao wamepotea ndani ya masaa 12, faru mmoja huuwawa.

Baada ya faru 471 kuuwawa ndani ya miaka 100, jumla ya faru 29,000 ndiyo wanakadiriwa kutembea kwenye ardhi ya dunia.

Inakadiriwa kuwa ndani ya miaka 10, simba, tembo na vifaru watakuwa historia. Picha| Peta.

Haata wakati tembo 350,000 wakibakia duniani, shirika hilo limesema kila mwaka, tembo 35,000 wanakadiriwa kuuwawa ikiwa ni matokeo ya ujangiri, mitego na migogoro kati ya wanyama hao na wanadamu.

Ndani ya miaka 100, jumla ya tembo 4.65 milioni wameuliwa.

Kwa takwimu hizo, shirika hilo limetabiri kuwa huenda mtoto atakayezaliwa miaka 11 ijayo, akamsoma tembo, simba na faru kwenye somo la historia bila uwezo wa kumuona bayana.

Jambo hilo mbali na kubakiza wanyama hao kuwa historia, huenda likasababisha athari katika shughuli za kitaliikwani wanayama hao ni muhimu katika shughuli hizo kutokana na upekee wao.

Shirika hilo linashauri ili kuendelea kuwahifadhi wanyama hao katika uso wa dunia, ni muhimu kuharibu mitego yote iliyowekwa na majangiri kwa ajili ya kukamata wanyama hao kwani hata wasipowapata, mitego hiyo inaishia kuwaacha walemavu na hivyo kufa.

Pia, shirika hilo limeshauri kuimarishwa kwa doria za askari wanyamapori katika hifadhi za Taifa kwa kuwawezesha kupata usafiri wa uhakika utakaowawezesha kufanya kazi zao kirahisi.

“Kwa pungufu ya miaka 10 hadi kutoweka kwa tembo, faru na simba, hatuna budi kukubali kuwa suluhu zinazotumika sasa zimeshindwa kufanya kazi.

Hifadhi za Taifa za Afrika zipo kwenye mashambulizi na dunia imeshindwa kuitikia wito,” imesomeka sehemu ya taarifa ya shirika hilo.


Zinazohusiana


Tanzania bado iko juu

Hata wakati wayama hao wakipungua duniani, nchini Tanzania kumeripotiwa kuwepo kwa ongezeko la wanyama hao jambo linaloifanya iendelee kufaidika na mapato yatokanayo na shughuli za utalii wa wanyamapori. 

Kwa mujibu wa Rais John Magufuli wakati akifunga Bunge la 11, Juni 16 mwaka huu, idadi ya tembo na faru wameendelea kuongezeka nchini ikiwa ni matokeo ya juhudi za kupambana na ujangiri dhidi ya wanyama hao.

Dk Magufuli alisema,  idadi ya faru imeongezeka kutoka 162 mwaka 2015 hadi 190 mwaka 2019 huku tembo wakiongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 51,299 mwaka 2019.

“Kufuatia hatua hizo, idadi ya watalii na mapato yameongezeka. Kwa mfano, mwaka 2019 tulipokea watalii milioni 1.5 kutoka watalii milioni 1.2 mwaka 2015,” alisema Dk Magufuli.

Zaidi, nchi ya Tanzania imetenga asilimia 32 ya ardhi yake kwa ajili ya shughuli za utunzaji wa rasilimali zikiwemo wanyamapori.

Habari hii imeboreshwa kwa kuongezewa infografia Julai 15, 2020. 

Enable Notifications OK No thanks