Facebook yaja na tovuti ya 'usiri' kuwasaidia wafanyabiashara kuelewa sera zake

Daniel Samson 0125Hrs   Januari 31, 2019 Teknolojia
  • Itakuwa na taarifa muhimu za sera na kanuni zinazosimamia matumizi ya taarifa za siri, matangazo na watumiaji wa mtandao huo. 
  • Pia itawasaidia watumiaji kujiongezea ulinzi wanapokuwa mtandaoni.
  • Bado ina kibarua kigumu cha kujiondoa katika kashfa mbalimbali za kuvujisha na udukuzi wa taarifa za wafuasi wake. 

Ikiwa zimepita siku mbili tangu dunia iadhimishe Siku ya Usiri wa Data (Data Privacy Day), Mtandao wa Facebook umeanzisha tovuti mpya inayorahisisha upatikanaji wa sera za matumizi ya data na marejeo yatakayowasaidia wafanyabiashara kulinda na kuheshimu taarifa za wateja wao. 

Siku ya Usiri wa Data ilianza kuazimishwa Marekani na Canada mwaka 2008 ikiwa ni mwendelezo wa Siku ya Kulinda Data ambayo inazimishwa Januari 28 kila mwaka.

Siku hiyo ni mahususi kuwaelimisha watumiaji wa mitandao na mashirika juu ya matumizi sahihi ya data katika shughuli mbalimbali za mawasiliano na maendeleo. 

Tovuti hiyo inajumuisha viunganishi vyote vya sera zinazosimamia matumizi ya data na vidokezo muhimu vya matumizi ya taarifa za wafuasi wa mtandao huo. 

Lakini ni sehemu muhimu ambayo makampuni mbalimbali yanayotumia mtandao huo kuelewa namna nzuri ya kutumia taarifa za watu bila kuathiri sheria za kimataifa. 

Muonekano wa tovuti mpya iliyotengenezwa na Facebook kwaajili ya sera, kanuni za matumizi ya taarifa za wafuasi wa mtandao huo. Picha|Daniel Samson.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Facebook wiki hii, tovuti hiyo itakuwa kituo muhimu cha upatikanaji wa taarifa za kanuni za matangazo na faragha, jinsi data zinavyotumiwa katika matangazo ya bidhaa na mwongozo  wa kuyasaidia makampuni kuelewa kanuni hizo.

Sambamba na hilo, Facebook itaanza kuwafahamisha watumiaji wa mtandao huo kuhusu tovuti hiyo na jinsi wanavyoweza kufaidika na kukabiliana na uvunjifu wa seara za faragha na usiri wa taarifa.

Suala la usiri wa taarifa za watumiaji wa mitandao ya kijamii limeibua mjadala mkubwa mwaka mmoja uliopita ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakihoji nguvu ya kisheria ya makampuni ya matangazo na mitandao ya kijamii kutumia taarifa za wateja wao na haki walizonazo watumiaji hao. 

Watumiaji wa Facebook nao watapata fursa ya kupitia sera zinazosimamia faragha ili kuboresha usalama wao mtandaoni. Picha| Mtandao.

Wakati Facebook ikitumia mbinu mbalimbali kuboresha na kulinda taarifa za watumiaji wake, kampuni ya Apple inayotengeneza simu za Iphone imeiondoa programu tumishi (App) ya Onavo  inayomilikiwa na Facebook katika duka lake la Apple Store kwa madai kuwa imekiuka masharti ya sera za usiri za duka hilo la mtandaoni.  

Onavo imekuwa ikiwasaidia wafuasi wa Facebook kutunza taarifa zao na kuzuia tovuti hatarishi zinazodukua data za watumiaji. 

Hii itakuwa ni kashfa nyingine kwa Facebook ambayo inafanya kila jitihada za kupambana na wadukuzi wa taarifa za wateja wake ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani wa mitandao ya kijamii.


Zinazohusiana:


Wachambuzi wa masuala ya usalama mtandaoni wanasema hatua hiyo ya Facebook ni kujaribu kurudisha imani kwa wateja ili kufuta kashfa ya kuvujisha taarifa muhimu za watumiaji wa mtandao huo kwa washirika wake wa biashara.

Kashfa hizo zinamuweka katika wakati mgumu mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Facebook, Mark Zuckerberg kujisafisha kwa watumiaji wa mtandao huo ambao mara kwa mara wamekuwa wakihamasishana kuachana na Facebook wakidai siyo mahali salama.

Ni wajibu kwa watumiaji kuzielewa vizuri sera za Facebook zinazosimamia faragha  ili kuepuka changamoto za usalama wakati wakitumia mtandao huo.

Hata hivyo, hatua hizo zinazotekelezwa na mtandao huo, haziwezi kumaliza mjadala wa usalama wa watumiaji wa mitandao, wakati huo ambao nchi mbalimbali zinatunga sheria ili kuwalinda watu wao wasipate madhara wanapokuwa mtandaoni.  

Related Post