Clouds Media yapata pigo jingine, yampoteza Ephraim Kibonde

March 7, 2019 1:02 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amekutwa na umauti katika hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.
  • Kifo hicho kinatokea ikiwa zimepita siku tu tisa tangu kampuni hiyo impoteze Mkurugenzi wake wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba na kuzikwa Machi 4, 2019 mkoani Kagera.

Kampuni ya Clouds Media Groups (CMG) imepata pigo jingine baada ya mtangazaji wa Clouds FM Ephraim Kibonde kufariki dunia alfajiri ya leo akiwa katika Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.

Kifo cha Kibonde, ambaye alikuwa mtangazaji wa kipindi cha ‘Jahazi’, kimetokea ikiwa zimepita siku tatu tangu kampuni hiyo impumzishe katika nyumba ya milele Mkurugenzi wake wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba aliyezikwa mkoani Kagera baada ya kufariki Februari 26, 2019 wakati akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini. 

Kibonde alikuwa miongoni mwa wafanyakazi wa CMG waliokwenda kwenye msiba wa Ruge mkoani Kagera na alikuwa mmoja ya Washehereshaji wa siku ya kuuaga mwili wa Ruge katika Viwanja vya Kharimjee Jijini Dar es Salaam wikiendi iliyopita akiwa na Baby Kabae. 

Habari za kifo hicho cha Kibonde zilitangazwa mapema leo asubuhi na Clouds Media katika kurasa zake za mitandao ya kijamii na kuamsha machungu mengine kwa tasnia ya habari na wapenzi wa mtangazaji huyo. 

Kupitia ukurasa wa mtandao wa akaunti yao ya Instagram, Clouds Media imeandika; “Tunamtukuza Mungu kwa maisha ya Kibonde na kumuomba yeye ampokee na kumpuzisha katika makao ya amani ya milele.Tutaendelea kuwapa taarifa zaidi kuhusiana na msiba huu.”

Kibonde pia alikuwa MC maarufu na mahiri katika shughuli mbalimbali amefariki dunia ikiwa imepita miezi saba tangu aondokewe na mke wake  aliyejulikana kwa jina la Sara Kibonde wakati anapatiwa matibabu katika hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam ambapo wameacha watoto watatu; Junior, Hilda na Illaria. 

Kufuatia msiba huo, watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa na wafanyabiashara wametoa salamu zao za pole kwa familia ya Kibonde na uongozi wa Clouds Media.

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amefika katika ofisi za kampuni hiyo leo asubuhi iliyopo Mikocheni jijni hapa kutoa salamu zake za pole huku akisema amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa na kazi ya Mungu haina makosa. 

Naye mfanyabiashara maarufu Afrika Mashariki, Mohammed Dewji ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, “Nawawaza watoto wake, wamebaki yatima Mungu awape nguvu. Pumzika kwa amani Kibonde!.”

Enable Notifications OK No thanks