CAG aibua madudu yanayotishia uhai sekta ya utalii Tanzania
- Ni pamoja vifo vya kutisha vya wanyamapori na mimea vamizi.
- Ukosefu wa bajeti ya taasisi zinazosimamia utalii.
- Changamoto hizo zinaweza kuathiri mapato ya utalii.
Dar es Salaam. Wakati mjadala mpana ukiendelea Tanzania kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/21, mambo mbalimbali yameibuliwa na rpoti hyo katika sekta ya utalii ikiwemo mauaji ya wanyamapori ya kiwango cha juu katika hifadhi za Taifa.
CAG Charles Kichere katika ripoti yake kwa mashirika ya umma amesema amebaini vifo vya wanyamapori kutokana na ajali za barabarani ni vya kiwango cha kutisha katika hifadhi za taifa.
Mwaka 2020/21, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi pekee ilirekodi mauaji ya wanyamapori 535 kutokana na ajali za barabarani sawa na ongezeko la asilimia 405 ikilinganishwa na vifo vya wanyamapori 106 kwa mwaka 2019/20.
Pia wanyamapori 50 waliuawa katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hifadhi ya Taifa ya Tarangire (18); na wanyama 11 waliuawa katika hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Vifo vya wanyamapori vimekuwa vikitishia uhai wa sekta utalii kwa sababu, wanatumika kwa sehemu kubwa katika kuvutia watalii wa kimataifa kuja nchini.
Hata hivyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali kudhibiti vifo vya wanyamapori katika hifadhi za Taifa ikiwemo kuweka alama, vizuizi na kutoza faini kwa wanaosababisha ajali.
Aidha, CAG amebaini masuala mengine yanayoweza kuwa na athari za muda mrefu katika uendelevu wa hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, iwapo Serikali haitachukuwa hatua za dhati kurekebisha hali hiyo.
“Kwa mfano, kutotoa ruzuku ya kutengeneza miundombinu na miradi ya maendeleo, ambapo mwaka 2020/21 bajeti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ilikuwa Sh31.2 bilioni lakini Serikali ilitoa Sh10.3 bilioni (asilimia 33) tu,” amesema CAG katika ripoti hiyo.
Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo wanyamapori na Mlima Kilimanjaro. Picha| Mwananchi.
Bajeti ya maendeleo ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa mwaka 2020/21 ilikuwa Sh69.52 bilioni lakini ni Sh26.51 tu, sawa na asilimia 38 ndiyo ziliidhinishwa kutolewa.
“Kutolewa kwa fedha chini ya bajeti kulichangia kutotekelezwa kwa shughuli za maendeleo ya hifadhi zinazohusiana na miundombinu, uhifadhi, na huduma za utalii,” amesema CAG.
CAG Kichere katika ripoti hiyo amebaini zaidi kuwa watumishi 10 wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) wanakaimu nafasi za wakuu wa idara na vitengo kwa zaidi ya miezi sita hadi mwaka mmoja kinyume na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 zinazotaka mtumishi wa umma kukaimu nafasi iliyo wazi kwa kipindi kisichozidi miezi sita.
Kutangaza utalii bado bado
Ripoti ya CAG imeeleza zaidi kuwa mkakati kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania haujawahi kupitiwa na kutathminiwa na TTB tangu mwaka 2008.
“Kwa maoni yangu, mkakati kwa ajili ya kutangaza utalii unatakiwa uangaliwe upya kutokana na mabadiliko yaliyopo katika sekta ya utalii,” imeeleza ripoti hiyo.
Zinazohusiana:
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
Licha ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro kukumbwa na matukio ya moto kwa nyakati tofauti likiwemo la mwaka 2020 ambalo liliteketeza kilomita za mraba 96.07 za eneo la hifadhi, bado haikuwa na vifaa vya kisasa vya kuzimia moto kama vile ndege za kuzima moto.
Pia, maofisa wake hawakuwahi kupewa mafunzo sahihi ya zimamoto ili kuweza kuwaweka sawa kwa ajili ya kukabiliana na kudhibiti majanga ya moto.
“Ninapendekeza Serikali, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) itathmini athari za milipuko ya moto na irejeshe miundombinu na uoto wa asili katika maeneo yaliyoathiriwa na moto, itumie satellite katika kubaini matukio ya moto na ianzishe kikosi kazi cha kupambana na majanga ya asili,” imeshauri ripoti hiyo.
Bajeti itengwe ya kununua vifaa vya kisasa vya kuzima moto ikiwa pamoja na helikopta kwa ajili ya kukabiliana na milipuko ya moto, na ambayo itatumika kwa shughuli za doria na uokoaji hifadhini.
Mimea vamizi bado shida hifadhini
Ukaguzi wa CAG katika hifadhi za Taifa na maeneo mengine tengefu umebaini kuwa bado kuna haja ya Serikali kuingilia kati udhibiti wa mimea vamizi.
Kukosekana kwa jitihada na uratibu jumuishi kutoka kwa wadau wote ikiwa pamoja na Serikali za kupambana na mimea vamizi, malisho ya wanyamapori yako hatarini kutoweka hivyo kusababisha wanyamapori kupotea kutokana na kukosa malisho.
Fukwe za bahari na maziwa ni rasilimali muhimu kuvutia wawekezaji kuja nchini. Picha| Muungwana.
Athari za muda mrefu
Huenda mapungufu yaliyoibuliwa na CAG katika ripoti hiyo yakawa na athari za muda mrefu kwa uhifadhi wa rasilimali na sekta ya utalii ikiwemo kutofikia matarajio ya kuongeza idadi ya watalii na kuongeza mapato ya utalii.
Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) umejielekeza katika mambo yanayoweza kufanyika ili kuanzisha vivutio vipya vya utalii vitavyowezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa katika sekta hii ili kuchangia katika pato la Taifa na kutoa fursa za ajira.
Mpango huu unaonesha kuwa ifikapo mwaka 2026, idadi ya watalii inatarajiwa kufikia milioni tano wakati huohuo mapato yanatarajiwa kufikia Sh13/9 trilioni. Juhudi hizo zinalenga pia kuchangia kwa asilimia 11 kwenye pato la Taifa ifakapo mwaka 2025/26 kutoka asilimia 6 ambayo ilichangiwa na sekta ya utalii kwenye pato la Taifa mwaka 2019/20.