Bosi wa Safaricom afariki kwa saratani Kenya

July 1, 2019 7:29 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Afisa Mtendaji Mkuu, Robert (Bob) Collymore aliyeanza kupata matibabu tangu Oktoba 2017.
  • Amefariki nyumbani kwake jijini Nairobi akiacha mke na watoto wanne.
  • Alikuwa ni moja ya maofisa watendaji wakuu mashuhuri wa sekta binafsi Afrika Mashariki. 

Dar es Salaam. Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya huduma za simu ya Safaricom nchini Kenya, Robert (Bob) Collymore amefariki duniani nyumbani kwake jijini Nairobi leo asubuhi baada ya kuugua saratani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Safaricom, Nicholas Nganga amesema Oktoba 2017 Bob alienda Uingereza kupatiwa matibabu ya saratani ya damu ijulikanayo kitaalamu kama Acute Myeloid Leukemia (AML) na kurejea Agosti 2018 kuendelea na majukumu yake.

“Amekuwa akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali tofauti na hivi karibuni katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi. Hali yake ilizidi kubadilika wiki za hivi karibuni na amefariki kwa saratani leo Julai mosi, 2019 nyumbani kwake,” amesema Nganga katika taarifa kwa umma iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kampuni hiyo.

Amesema kigogo huyo raia wa Uingereza ameacha mke na watoto wanne.

Bob Collymore enzi za uhai wake. Bob atakumbukwa kwa uongozi wake mahiri katika kuikuza Safaricom. Picha|Aptantech.com

Bob (61) alikuwa ni moja ya maofisa watendaji mashuhuri wa sekta binafsi Afrika Mashariki na aliyechagiza mafanikio makubwa katika kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE).

“Kwa niba ya Bodi ya Wakurugenzi ya Safaricom PLC, tunatoa pole kwa familia yake, wafanyakazi wa Safaricom, washirika wetu na kwa taifa alilojitolea kwa hali na mali kufanikisha maendeleo,” amesema Nganga.

Enable Notifications OK No thanks