Bei ya maharage yazidi kuchanja mbuga Dar

February 26, 2020 3:43 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Gunia la kilo 100 la maharage linauzwa kwa Sh300,000 kutoka Sh270,000 ya wiki iliyopita. 
  • Bei hiyo ya maharage ni ya juu zaidi kuliko mazao yote ya chakula yanayouzwa leo katika masoko mbalimbali nchini. 
  • Bei ya chini kabisa ya maharage imeshuhudiwa katika masoko ya Halmashauri ya Musoma mkoani Mara ambapo gunia la kilo 100 limeuzwa kwa Sh100,000.

Dar es Salaam. Huenda leo ikawa ni tabasamu kwa wafanyabiashara wa maharage jijini Dar es Salaam baada ya zao hilo kuuzwa bei ya juu zaidi kuliko mazao mengine makuu ya chakula nchini Tanzania. 

Mazao makuu ya chakula hujumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano.

Kwa mujibu takwimu za Wizara ya Viwanda na Biashara zilizotolewa leo (Februari 26, 2020) zinaonyesha kuwa gunia la kilo 100 la maharage linauzwa kwa Sh300,000 katika soko la Tandale la jijini Dar es Salaam ikiwa imepanda kutoka Sh270,000 iliyorekodiwa Jumatano Februari 19 ya wiki iliyopita katika soko la Tandika. 

Kwa kiwango hicho cha bei, wafanyabiashara wa jiji hilo linalokuwa kwa kasi wameweka kibindoni Sh30,000 kwa kila gunia la kilo 100.  

Bei hiyo iliyorekodiwa leo ya Sh300,000 ni ya juu zaidi kuliko mazao yote ya chakula yanayouzwa leo katika masoko mbalimbali nchini Tanzania.

Hata hivyo, bei ya chini kabisa ya maharage imeshuhudiwa katika masoko ya Halmashauri ya Musoma mkoani Mara ambapo gunia la kilo 100 limeuzwa kwa Sh100,000.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa viazi mviringo ndiyo vinauzwa kwa bei ya chini kabisa kuliko mazao yote makuu ya chakula yaliyopo sokoni leo. 

Bei hiyo imeshuhudiwa katika soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya ambapo gunia la kilo 100 linauzwa kwa Sh46,000, wakati bei ya juu ya zao hilo ikiwa ni Sh120,000 katika mkoa wa Lindi.

 

Enable Notifications OK No thanks