Bahati ya Mtende: Magufuli amteua tena Mwigulu kuwa waziri
- Ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi ya Dk Augustine Mahiga.
- Aliwahi kufutwa kazi na Rais Magufuli Julai mwaka 2018.
Dar es Salaam. Dk Mwigulu Nchemba ni miongoni mwa Watanzania waliobahatika kumaliza siku vizuri baada ya Rais John Magufuli kumteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria ikiwa ni mara ya pili kwa mwanasiasa huyo kuingia kwenye baraza la mawaziri la Serikali ya awamu ya tano.
Dk Nchemba ameteuliwa leo (Mei 2, 2020) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Dk Augustine Mahiga aliyefariki Mei Mosi mwaka huu baada ya kuugua ghafla nyumbani kwake Jijini Dodoma.
Dk Mahiga amezikwa leo nyumbani kwao Tosamaganga mkoani Iringa.
Kuteuliwa kwa Dk Nchemba kunamfanya kuingia kwenye orodha ya wanasiasa wachache nchini walioaminiwa na Rais Magufuli kupenyeza kwa mara ya pili kwenye baraza la mawaziri baada ya kufutwa kazi mara ya kwanza.
Mwanasiasa mwingine aliyepenyeza kwenye Baraza la Mawaziri ni George Simbachewene aliyeteuliwa tena kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Julai mwaka jana.
Simbachawene baadaye alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Kangi Lugola kung’olewa Januari mwaka huu kwa tuhuma za kuiingiza Serikali kwenye mkataba wa zaidi ya trilioni moja usio na tija kwa Taifa.
Soma zaidi: Serikali kurekebisha makosa ununuzi wa pamba Tanzania
Awali Dk Nchemba aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi lakini kibarua chake kilikoma mwanzoni mwa Julai 2018 baada ya Rais Magufuli kumfuta kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Lugola.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa inasema uteuzi wa Dk Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) unaanza leo Mei 2.
Dk Nchemba anakuwa waziri wa tatu wa Katiba na Sheria Tanzania ndani ya kipindi cha miaka minne na nusu ya Rais Magufuli madarakani.
Waziri wa kwanza kuteuliwa nafasi hiyo alikuwa ni Dk Harrison Mwakyembe aliyehamishwa wizara hiyo na kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mwishoni mwa Machi 2017.
Baada ya Dk Mwakyembe kuhamishwa wizara hiyo aliteuliwa Prof Palamagamba Kabudi ambaye alihamishwa kwenda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwanzoni mwa Machi mwaka jana.