'Maisha Package' kifurushi kinachowakinga wasichana dhidi ya mimba zisizotarajiwa

TULINAGWE MALOPA 0742Hrs   Agosti 31, 2018 Habari
  • Kifurushi hicho kinampatia msichana uhakika wa afya bora kwa kumuondolea hatari ya kupata VVU na mimba zisizotarajiwa.
  • Mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike.

Dar es Salaam. Mimba za utotoni zimeendelea kuwa changamoto kubwa inayowakabili watoto wa kike nchini  licha ya kuwepo sera na mipango mbalimbali ya kuwalinda ili watimize ndoto zao za kimasomo na kimaisha.

Pamoja kuwepo kampeni mbalimbali za kuwanusuru watoto hao, Ripoti ya Matokeo Muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Malaria ya Tanzania (TDHS 2015/2016 inabainisha kuwa bado zaidi ya robo au asilimia 27 ya watoto wa kike nchini wanapata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18 huku wengi huishia kuolewa na kupata matatizo ya afya.

Hali hiyo imezidi kuwanyima usingizi baadhi ya wazazi na walezi ambao hujikuta wakisaka njia mbadala ya kuwanusuru wasichana hao dhidi ya mimba na ndoa za utotoni ili wasome na kutimiza ndoto zao.

Hata hivyo, huenda wazazi na walezi hao wakawa wamepata sehemu ya suluhisho la tatizo hilo baada ya Gilda Given Silayo (24) wa kampuni ya Life Package Solutions kubuni bidhaa yenye taarifa muhimu kuwasaidia wasichana kuboresha afya zao ili kuepuka vishawishi vitakavyowatumbukiza kwenye mimba za utotoni.  

Bidhaa hiyo iitwayo 'Maisha Package', ni kifurushi maalumu chenye taulo la uzazi na taarifa muhimu za afya ya jinsia na uzazi salama kwa lengo la kupunguza mimba za utotoni kwa njia ya kutoa taarifa zilizo sahihi na huduma rafiki.

Gilda na timu yake wanashirikiana kwa karibu na kampuni ya Sahara Sparks, Shirika la Misaada la Uingereza (UKaid)Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) ambapo hutoa elimu ya uzazi na vifaa vya kujikinga na mimba kwa wasichana wenye umri mdogo hasa wanaoishi katika mazingira hatarishi.  

Kupitia Maishapackage, msichana anayejithamini na kujitambua atapata taarifa muhimu za afya ya jinsia na uzazi, pedi (Taulo za kike), kipimo cha mkojo, nguo ya ndani na kondomu ya kike ambayo anaweza kutumia kama anashiriki mapenzi. 

“Lengo kuu la kuanzisha kifurushi hiki ni kwa ajili ya kupunguza tatizo kubwa la mimba za utotoni, na kutoa elimu kwa vijana na mabinti wengi ili kupunguza tatizo hili la mimba za utotoni,” anasema Meneja Masoko wa Life Package Solutions, Kelisa Bernard.

Kifurushi cha Maisha Package kinampatia msichana uhakika wa afya bora. Picha| Maisha Package.

Matumizi ya 'Maisha Package' hutegemea zaidi uelewa wa msichana kuhusu afya ya uzazi, lakini hilo haliwazuii kukutana na wasichana waliopo shuleni na kuwaelimisha njia sahihi za kujikinga na mimba ikiwemo taulo za kike kujikinga na maambukizi  katika njia za uzazi.

Kelisa anaamini kuwa jamii inapaswa kuambiwa ukweli juu ya tatizo la mimba na kuchukua hatua ikiwemo kutumia teknolojia ya mawasilino kuwaongezea wasichana maarifa na ujuzi wa kujikwamua kimaisha.

"Tofauti kubwa ya pedi tulizonazo na pedi zingine ni kwamba pedi zetu ni za pamba ambayo inapendelewa na watu wengi kama kitu cha asili, lakini pedi zingine ni za plastiki. Huu ni utofauti mmoja mkubwa tu,” amesema Kelisa.

Licha ya Maisha Package kuwa msaada kwa wasichana wengi nchini, bado inatumika kama njia ya kutengeneza ajira kwa wasichana ambapo mpaka sasa kampuni hiyo ina wafanyakazi waanzilishi wasiopungua wanne na wasambazaji mbalimbali wa biadhaa hiyo.  

Kukubalika kwa Maisha Package katika jamii hasa watoto wa kike kutaongeza wigo wa ajira kwa wasichana na wanawake na kuwapunguzia mzigo wa utegemezi.  

Kelisa anabainisha kuwa bado wana safari ndefu ya kuwafikia wasichana wengi zaidi ikizingatiwa kuwa kampuni yao ni changa inahitaji wawekezaji watakaotambua thamani na huduma wanayotoa katika jamii kwa kuwa kwa sasa hawana mtaji wa kutosha kuongeza uzalishaji na masoko. 

Related Post